Walemavu wa ngozi, ‘walia’ kubaguliwa katika ajira

Muktasari:

Ukosefu wa ajira ni changamoto inayowakabili wasomi wenye ualbino, wengi wao wakiamini kuwa hali yao inachangia kunyimwa nafasi.

Dar es Salaam. Watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Albino’ wamelalamikia kutengwa na mfumo wa ajira huku waajiri wengi wakiwaona watu wa kundi hilo hawawezi kufanya kazi.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha vijana wengi wenye Ualbino kuendelea kubaki mitaani bila kazi licha ya kupata fursa ya kusoma.

Hilo linalisukuma shirika linalowasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi la Under the Same Sun kuandaa programu maalum ya kuwakutanisha wahitimu wenye Ualbino na waajiri.

Katika warsha hiyo iliyowakutanisha wahitimu wa vyuo vikuu wenye ualbino kilio kikubwa ilikuwa ni ukosefu wa ajira.

Mkuu wa idara ya Ushauri na Masuala ya Ajira katika shirika hilo, Josephat Igembe amesema changamoto hiyo inaendelea kukua hivyo wameona waifanyie kazi.

Mwajiri anaona kumuajiri mtu mwenye Ualbino inaweza kuwa mkosi kwenye kampuni yake jambo ambalo halina ukweli.

“Sasa hivi tunasoma, tunafika kwenye ngazi zote za elimu, maarifa tunayo hivyo tuna sifa za kuajiriwa,” amesema.

Amesema wakati umefika kwa jamii kuachana na dhana potofu na kuwapa nafasi watu wenye Ualbino.