Walimu kortini kwa wizi wa mitihani ya darasa la saba

Muktasari:

  • Walimu watano akiwamo mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Hazina ya jijini Dar es Salaam, wameshtakiwa kwa makosa matatu ikiwamo kupata na kuutoa mtihani wa darasa la saba uliofanyika kati ya Septemba 7 na 8, 2018.

Dar es Salaam.  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hazina iliyopo Magomeni, Dar es salaam, Patrick Cheche (43) na walimu wenzake wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwa ni pamoja na  kupata mitihani na kutoa maudhui ya mitihani hiyo kwa watahiniwa wa darasa la saba isivyo halali.

Akiwasomea hati ya mashtaka leo Septemba 26, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono aliwataja washtakiwa hao kuwa ni mwalimu Laurence Ochien (30), mkazi wa Magomeni Makuti.

Wengine ni mwalimu Justus James (32) Mkazi wa Kimara Mwisho Mavurunza, Nasri Mohammed (32) Mkazi wa Magomeni Makuti.

Kombakono katika shtaka la kwanza amedai Septemba 4, 2018 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wote kwa pamoja walikula njama kwa kuingilia mitihani ya taifa ya darasa la saba isivyo halali.

Katika shtaka la pili, wakili Kombakono amedai Septemba 5, 2018 katika Shule ya Hazina, washtakiwa hao kinyume na sheria, walijipatia mitihani ya Taifa ya darasa la saba na kwa makusudi waliwapatia maudhui watahiniwa waliosajiliwa katika shule hiyo.

Katika shtaka la tatu inadaiwa Septemba 5, 2018 katika shule hiyo washtakiwa hao kwa makusudi walitoa mitihani kwa watahiniwa waliosajiliwa katika shule hiyo, wakati hawakustahili kufanya hivyo.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amedai hawana pingamizi na washtakiwa hao kupewa dhamana ila aliomba hati za kusafiria za mshtakiwa Ochien na James zisalimishwe mahakamani kwa kuwa ni raia wa Kenya.

Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Hakimu Shaidi alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho na mmoja kati ya wadhamini hao atoke katika taasisi inayotambulika na kwamba kila mdhamini asaini bondi ya Sh6 milioni.

Hata hivyo, washtakiwa hao walifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana kasoro mshtakiwa wa pili ambaye alipelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana.

Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 10, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.