Walimu watakiwa kuzingatia mitalaa

Muktasari:

  • Aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na walimu wa shule za msingi Kata ya Kibimba baada ya kufanya ukaguzi wa utekelezaji mitalaa ya elimu nchini.
  • Augustine alisema katika utekelezaji wa mitalaa, lazima kuwapo upimaji wa kile kilichofundishwa na kufanyika tathmini kwa kubaini changamoto zilizojitokeza na kuweka mkakati wa kuboresha taaluma ngazi ya shule, kata hadi wilaya.

Ngara. Ofisa Mdhibiti Ubora wa Elimu, Joel Augustine amewataka walimu kuhakikisha wanaingia darasani kufundisha mada na kuzimaliza kwa wakati, kwa kuwapatia wanafunzi majaribio na mitihani.

Aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na walimu wa shule za msingi Kata ya Kibimba baada ya kufanya ukaguzi wa utekelezaji mitalaa ya elimu nchini.

Augustine alisema katika utekelezaji wa mitalaa, lazima kuwapo upimaji wa kile kilichofundishwa na kufanyika tathmini kwa kubaini changamoto zilizojitokeza na kuweka mkakati wa kuboresha taaluma ngazi ya shule, kata hadi wilaya.

Ofisa Elimu Maalumu katika Idara ya Msingi wilayani Ngara, Gransia Rwela aliwataka walimu wa shule za msingi kufundisha kwa kuzingatia mwongozo wa mitalaa ya taasisi ya elimu kwa madarasa ya elimu ya awali hadi la pili, ili kuhakikisha wanafunzi wanafahamu kusoma, kuhesabu na kuandika (KKK).

“Wanafunzi wafundishwe kutambua mazingira yanayowazunguka, kwa kuhimizwa kufanya usafi wa mwili na mavazi,” alisema Rwela.