Waliokutwa na meno ya tembo 210 wafungwa miaka 20 jela

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapata na hatia ya uhujumu uchumi, Peter Kabi na mkewe, Leonidia na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh2,206,611,000.

Muktasari:

  • Nyara hizo ni vipande 210 vya meno ya tembo pamoja na vipande vitano vya mifupa ya mnyama huyo ambavyo walikutwa navyo Oktoba 27, 2012 katika maeneo ya Kimara Stop Over, Dar es Salaam. Vipande vya meno ya tembo vilikuwa na uzito wa kilo 450.6 vyenye thamani ya Dola za Marekani 1,380,000 ilhali mifupa ilikuwa na thamani ya Dola 30,000 na kwamba vyote vilikuwa na thamani ya Dola 1,410,000 sawa na Sh 2,206,611,000.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapata na hatia ya uhujumu uchumi, Peter Kabi na mkewe, Leonidia na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh2,206,611,000.

Nyara hizo ni vipande 210 vya meno ya tembo pamoja na vipande vitano vya mifupa ya mnyama huyo ambavyo walikutwa navyo Oktoba 27, 2012 katika maeneo ya Kimara Stop Over, Dar es Salaam. Vipande vya meno ya tembo vilikuwa na uzito wa kilo 450.6 vyenye thamani ya Dola za Marekani 1,380,000 ilhali mifupa ilikuwa na thamani ya Dola 30,000 na kwamba vyote vilikuwa na thamani ya Dola 1,410,000 sawa na Sh 2,206,611,000.

Awali, washtakiwa walikana kutenda kosa wakidai kwamba hawazielewi nyara hizo na maelezo waliyotoa polisi yalichukuliwa baada ya kuteswa na kulazimishwa. Hata hivyo, Hakimu Huruma Shaidi aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo alisema kulingana na ushahidi wa pande zote mbili, maelezo hayo ni halali na kilichoandikwa kilikuwa sahihi na kwamba wakati chumba kilichokuwa na nyara kilipofunguliwa na polisi, Leonidia alipoteza fahamu hivyo alikuwa anajua uwepo wa nyara hizo katika nyumba yao.

Jana, akitoa hukumu kuhitimisha kesi hiyo, Hakimu Shaidi alisema amewatia hatiani kwa makosa matatu; kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kumiliki nyara za Serikali na kujihusisha na nyara za Serikali.

Alisema katika kosa la kujihusisha na mtandao wa uhalifu, watatumikia kifungo cha miaka 15 jela, shtaka la kumiliki nyara za Serikali kifungo cha miaka 20 jela na shtaka la kujihusisha na nyara za Serikali miaka 20 jela.

Kwa kuwa vifungo hivyo vitatu vitaenda sambamba, alisema washtakiwa hao watatumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Katika hukumu hiyo, Shaidi alisema vipande 210 vya meno ya tembo na vitano vya mifupa ya tembo walivyokutwa navyo vitakuwa mali ya Serikali.

Kuhusu nyumba ya wanafamilia hao ambayo ilikutwa imehifadhi nyara hizo, Hakimu Shaidi aliutaka upande wa mashtaka kupeleka maombi rasmi ili itaifishwe kama walivyoomba mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Elia Athanas.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Kadushi aliomba kutoa ushahidi wa ziada dhidi yao na aliitwa mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyama Pori Tanzania, Emmanuel Lymo (32) ambaye aliiambia Mahakama kuwa sensa ya tembo waliyoifanya inaonyesha kwamba wamepungua kwa asilimia 50.

Kwa mujibu wa sensa hiyo, Lymo alieleza kuwa mwaka 2006 kulikuwa na tembo 134,000 lakini wamekuwa wakipungua kwa kasi na kwamba mwaka 2009 walikuwapo 100,000 na mwaka 2012 walipungua hadi kufikia 43,000.

Lymo alidai kwamba kutokana na hali hiyo ilianzishwa Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo imesaidia na sasa wapo tembo 50,000 kutokana na kuwapo kwa doria na kukinga maeneo yaliyokuwa yakiwindwa kwa sehemu kubwa.

“Katika kesi hii, washtakiwa wameua tembo 93, tembo mmoja anabeba mimba kwa miezi 22 na anakuwa na uwezo wa kuanza kubeba mimba akiwa na miaka 12 na ana uwezo wa kuishi kwa miaka 60 na zaidi,” alisema.

Baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi huo, wakili wa washtakiwa hao, Mkagwa Bernard aliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu kwa sababu ni kosa lao la kwanza na wana familia inayowategemea.

Hata hivyo, Wakili Kadushi aliiomba Mahakama kupitia kifungu cha 111 cha Sheria ya Wanyama Pori namba 5 ya mwaka 2009 kutaifisha nyara na kitu chochote ambacho kilitumika saidia kosa kutendeka.

Hakimu Shaidi alisema ingawa ni mara ya kwanza kwa wakosaji, Mahakama imedhihirika ni kwa kiasi gani walifanya uharibifu kwa kuua tembo 93.

“Tunapata fedha za kigeni kutokana na hawa tembo watalii wakija kuwaangalia, hakuna mtalii atakayelipa fedha zake kuja kuona mizoga porini, uwindaji haramu unafanywa na watu wachache wenye tabia mbaya na ubinafsi jambo ambalo halikubaliki. Tanzania tumepewa utajiri tuufurahie kwa kufuata taratibu, lakini ninyi mke na mume mmeamua kula matunda ya edeni kinyume cha utaratibu hata mbinguni waliofanya hivyo waliadhibiwa.”

Mshtakiwa mwingine, polisi Simon Malisa aliachiwa huru kwa sababu ushahidi haukumgusa popote wala hakukuwa na namna ya kumuunganisha kwenye kesi hiyo.

Mkurugenzi wa mashtaka

Akizungumzia hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka, Biswalo Mganga alisema wakati meno ya tembo 210 na mifupa mitano ya tembo yanakamatwa ndani ya nyumba yao Kimara ilikuwepo Bendera ya Taifa ambayo wangeitumia kuyafunika wakati wanasafirisha kwenda Tarakea.

“Tutapeleka maombi rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kutaifisha nyumba ya washtakiwa,” alisema.