Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo: Wanaosusa uchaguzi wajifunze kwa wazee

Muktasari:

  • Chama cha ACT Wazalendo kimesema ni muhimu kupiga kura na kuzilinda ili kupata hatma wanazotarajia, badala ya kususa kushiriki uchaguzi.

Kigoma. Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema kususia uchaguzi si mbinu stahiki ya kukabili ukiukwaji haki na sheria wowote unaofanywa nchini, badala yake kunahitajika ushirikiano na mshikamano katika harakati za kufanikisha mapambano hayo.

Ameijenga hoja hiyo, huku akirejea historia ya harakati zilizofanywa na wazee wakati wa kuiondoa Serikali ya kikoloni, akisema hawakususa walishirikiana na hatimaye kuyafikia mafanikio ya kulikomboa Taifa.

Mchinjita ametoa kauli hiyo, katikati ya mkakati wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuzuia kufanyika kwa uchaguzi, iwapo hakutafanyika mabadiliko ya sheria 'No reforms no election'.

Hoja na misimamo hiyo, ni sehemu ya rasharasha za kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mchinjita ameyasema hayo, leo Jumanne Julai 1, 2025 alipozungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kalinzi Sokoni ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya Operesheni Majimaji Linda Kura Yako.

Kiongozi huyo, amesema historia inaonyesha kususia uchaguzi ni hatua inayowafariji watu kwa muda, lakini ushahidi unaonyesha hakukuwahi kuwa na manufaa ya hilo.

"Ingawa wazo hili linaweza kuvutia baadhi ya watu na kuwapa faraja ya muda, halina ushahidi wa kihistoria wa kuleta manufaa popote duniani," amesema.

Mchinjita amesema wazee walikabiliana na Serikali ya kikoloni kwa kuhamasisha mapambano ya raia, walishirikiana kuwaondoa madarakani wakoloni waliotawala kwa mabavu na kutumia vyombo vya dola.

Katika mazingira hayo, amesema wazee walihamasishana kupigana na Serikali ya kikoloni, akiwemo Abushiri bin Salim waliopigana huko Saadani, Pangani, hadi Pwani ya Bagamoyo.

Amewataka wengine ni Chifu Mkwawa wa Iringa aliyeongoza Watanganyika kupinga Serikali ya Wajerumani na hata Kusini mwa Tanzania, wazee walianzisha vita ya Maji Maji, ambayo iliyowaunganisha wananchi wasio na silaha kukabiliana na Serikali ya kikoloni.

"Ukatili wa wakoloni haukuwavunja moyo wazee wetu. Walikabiliana na ukatili huo kwa kuhamasisha vuguvugu la umma dhidi ya Serikali ya kikoloni. Hata pale walipokabili kifo, maneno yao yalikuwa ya kuhamasisha, sio kukatisha tamaa," amesema.

Amemrejea mmoja wa makamanda wakati wa vita hiyo, Suleyman Mamba, alipokamatwa na Wajerumani na kupelekwa Mwembe Kinyonga, Kilwa Kivinje, kwa ajili ya kunyongwa ili kuwa fundisho na hofu kwa wengine alisema: “Bora nife, mimi Suleyman Mamba, kuliko kutawaliwa na ninyi washenzi. Bora nife ili nchi yangu ishuhudie kuwa niliipigania.”

Amesema wakati huo haki ya kuchagua na kuchaguliwa ilidhibitiwa na masharti yasiyofaa kama kupiga kura tatu yaliwekwa.

Baadhi yao, amesema walipendekeza kususia hadi mifumo bora ya uchaguzi iwekwe.

Hata hivyo, amesema wazee waliona kuwa busara ya mapambano iko katika kushiriki, si kususa, hawakuamini Serikali ingeweza kusalimu amri kwa kususiwa.

"Leo, nchi yetu inajivunia uhuru wake kutokana na uzalendo na kutokata tamaa kwa wazee wetu. Hawakususia, bali walitumia kila fursa kukabiliana na Serikali inayokandamiza matakwa ya raia," amesema.

Ameeleza hakuna ushahidi wa kihistoria unaoonyesha jamii iliyomuadhibu mtawala katili kwa kumsusia.

"Jamii ilijiongoza kwa kukabiliana na dhulma na kupigania haki yake ya kuamua viongozi wake. Mapambano haya hayakuisha hadi kiongozi mwenye ridhaa ya umma alipochaguliwa," amesema.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Kiza Mayeye amewataka wananchi wa eneo hilo, wasihadaike na fedha wanazopewa na baadhi ya wanasiasa, wanapaswa kuwachagua viongozi bora.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, amesema tayari kumejitokeza wanasiasa wanashindana kutoa fedha kwenye misiba na harusi ili kujenga ushawishi.

"Tunataka wabunge watakaokwenda bungeni kusimama na changamoto za wananchi, badala ya wale wanaopiga makofu na kusema mama anaupiga mwingi, kujipendekeza ili warudi kupendekeza," amesema.

Amelisihi jeshi la polisi kuzingatia jukumu lake la kulinda raia na mali zake, badala ya kura feki za chama tawala.

"Tunataka uchaguzi huru na haki, tukishindwa tutasema tumeshindwa, tukishindwa ujinga ni kwenda, ujanja kurudi, ubaya ubwela tutatangazwa," ameeleza.

Hoja hiyo imeungwa mkono na kada wa chama hicho, Peter Madeleka aliyewataka wananchi kuwakataa wanasiasa wanaoshinikiza kuzuiwa kwa uchaguzi, kwa kuwa sio suluhu ya kukomesha dhuluma.

"Kuna wenzetu wanapita huko mtaani wanasema watazuia uchaguzi, hivi tangu mzaliwe mmewahi kuona nchi yoyote imezuiwa uchaguzi imefanikiwa?" amehoji.

Ameisisitiza hoja hiyo, akisema wanasiasa hao hao wanaodai kushiriki uchaguzi ni usaliti, waliowahi kuyakataa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kugoma kupokea ruzuku, lakini baadaye wakaipokea.

Madeleka ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria wa chama hicho, amesema ACT Wazalendo haioni sababu ya kuzuia uchaguzi, kwa sababu ukikimbia CCM haukuwahi kuondoka badala yake inachukua ushindi kwa njia rahisi.

"Mtu akikwambia zuia uchaguzi mkatae kama unavyomkataa shetani," amesema.

Kwa upande wa Emmanuel Ntobi amesema kwa hali ilivyo tayari chama tawala hakina nguvu tena, kinachopaswa kufanywa ni wananchi kujitokeza kupiga kura na kuzilinda ili hatimaye kushinda.

Ameliambatanisha hilo na kuwataka wanachama wa vyama vingine vyote kujiunga na ACT Wazalendo kwa kuwa ndilo jukwaa sahihi la mabadiliko ndani ya nchi.

"Sisi hatususi kwa sababu muhuni hasusiwi. Chukulia wewe ni kijana unamtaka mwenza halafu unasusa, atakuja kwako? Uliyemdusia atamchukua, hivyo muhuni hasusiwi," amesema.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Abdul Nondo amewasisitiza wananchi kujitokeza kupiga kura na kuzilinda ili kuepuka changamoto za ugumu wa maisha zinazowakabili.

"Kura yako ndiyo inayokwenda kusimamia ustawi wa maisha yako. Kuna watu wanahamasisha wananchi wasiende kupiga kura kwa kusema kwamba uchaguzi sio huru na haki, sisi tunasusa hatuendi. Hakuna historia popote ilipowahi kuandikwa kwamba ukimsusia mtawala unatatua changamoto zako," amesema.