Wananchi wafurahia utaratibu wa ofisi ya Makamu wa Rais

Muktasari:

  • Ni kuhusu kampeni ya kuzungumza nao na kuwajengea uwezo kuhusu utunzaji mazingira

Dar es Salaam. Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamepongeza utaratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kuzungumza nao na kuwajengea uelewa wa utunzaji wa mazingira, wakieleza kuwa jambo hilo litasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira.

 

Wametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 3, 2018 katika viwanja vya Zakhem Mbagala katika kampeni ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi kuhusu utunzaji ya tulonge mazingira, ikiwa ni mwendelezo wa wiki ya mazingira.

 

Mkazi wa kata ya Kibonde Maji, Alafa Boko amesema utaratibu huo ni mzuri na unawajengea uwezo wa kujua umuhimu wa utunzaji wa mazingira.

 

"Leo watendaji wa Serikali  wakiongozwa na Makamba (January-Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira) wametujengea uwezo kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kwa manufaa ya maisha yetu. Kwa kweli tumefarijika  sana kwa niaba ya kina mama wenzangu," amesema Boko.

 

Ameshauri utaratibu huo usiishie kwa wananchi, kutaka uende hadi kwa viongozi wa serikali za mitaa ambao wapo karibu zaidi na wananchi.

 

Mkazi wa Kinondoni,  Rashid Ally amesema kinachofanywa na ofisi hiyo ni ubunifu wa aina yake.

 

"Walianza kutoa elimu kwa wajasiriamali  kuhusu umuhimu wa utunzaji mazingira , wakaitisha kongamano la juu la wadau wa mazingira, kisha wakazungumza na viongozi  wa kiroho na leo wamezungumza na wananchi wa Dar es Salaaam. Hili ni jambo la kipekee la kuigwa,"amesema Ally.

 

Kwa upande wake Makamba amesema lengo la kampeni hiyo ni kuwajengea uwezo wakazi wa mkoa huo kuhusu umuhimu  wa kutunza mazingira na kufanya uhamasishaji kuhusu matumizi bora ya nishati mbadala ili kuokoa misitu.

 

Mbunge huyo wa Bumbuli amesema kampeni hiyo itakuwa endelevu na itaongezewa ubunifu, kwamba wameanzia Dar es Salaam kwa sababu ndio mkoa unaoongoza kwa matumizi ya mkaa wa kuni kwa asilimia 70.

 

"Tukimaliza Dar es Salaam tutakwenda Tabora ambako ndio mkaa mwingi unatoka. Tunataka twende tukazungumze na wanaokata miti na kuzalisha mkaa kuhusu umuhimu wa kutunza maliasili,” amesema Makamba.