Wananchi walia gharama kubwa miamala ya simu

Muktasari:

Profesa Ndulu aliyestaafu kuiongoza taasisi hiyo nyeti nchini mapema Janu-ari, alivishwa taji la gavana bora Afrika katika tuzo za Africa Banker Awards 2018 zilizotolewa jijini Busan, Korea Kusini hivi karibuni.

Wakati Gavana mstaafu wa Benki Kuu (BoT) akijivunia kufikisha huduma za fedha kwa wananchi wengi zaidi, wateja wa simu za mkononi wanalia na gharama za miamala.

Profesa Ndulu aliyestaafu kuiongoza taasisi hiyo nyeti nchini mapema Janu-ari, alivishwa taji la gavana bora Afrika katika tuzo za Africa Banker Awards 2018 zilizotolewa jijini Busan, Korea Kusini hivi karibuni.

Profesa Ndulu anasema ameipata tuzo hiyo kutokana na kushirikiana na wadau mbalimbali waliofanikisha kuimarisha huduma za fedha nchini.“Miongoni mwa sifa zilizosaidia kunipa tuzo hiyo ni kufikisha huduma za fedha kwa wananchi wengi zaidi.

Itakumbukwa, tangu uhuru mpaka mwaka 2006 ni asilim-ia 10 tu ya Watanzania walikuwa wanapata huduma za fedha lakini muongo mmoja baadaye kiasi hicho kimeongezeka mpaka asilimia 65,” anasema mchumi huyo.

Profesa Ndulu alianza kuiongoza BoT mwaka 2008 mpaka alipostaafu mwa-ka huu. Kwa miaka mitatu mfululizo, mpaka Septemba mwaka jana, alikuwa mwenyekiti wa (Shirikisho la Huduma Jumuishi za Fedha Duniani) Alliance for Finacial Inclusion.

Kwenye uongozi wake, Profesa Ndulu alifanikiwa kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa uchumi nchini. Alidhibiti mfumuko wa bei ambao mara nyingi ulikuwa tarakimu moja huku tha-mani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani ikiendelea kuimarika.

Huduma za fedhaMpaka mwanzoni mwa mwaka 2008, Profesa Ndulu alipochukua mikoba ya kuiongoza BoT, wananchi wengi walikuwa wanapata huduma za fedha kutoka benki za biashara na taasisi za fedha zilizopo nchini.Aprili mwaka huo, kwa mara ya kwanza, kampuni ya Vodacom ilizindua huduma za M-Pesa ambazo mpaka Desemba zilikuwa zinahudumia wateja 599,884.

Desemba 2008 Airtel ilianza kutoa huduma za fedha zilizoitwa Zapu kabla ya kufanya maboresho mwaka 2011 na kuziita Airtel Money.Mwaka 2009 Zantel ilizindua huduma zake za Ezy Pesa na ikazifanyia maboresho na kuzizindua tena mwaka 2012.

Miaka miwili tangu kuanza kutolewa kwa huduma hizo ushindani uliongezeka sokoni baada ya Tigo nao kuanzisha hudu-ma za Tigo Pesa iliyozinduliwa Septemba 2010.

Ikiwa na mwaka mmoja tangu ianze kutoa huduma za mawasiliano nchini, Oktoba 2016, Halotel ilizindua Halo Pesa ili kutoa huduma za fedha kwa wateja wake. Kwa miaka miwili sasa kampuni hiyo inaendelea kuwahudumia wateja wake kupitia Halo Pesa.

Julai mwaka jana, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lilikuwa la mwisho miongoni mwa washirika wa sekta hiyo baada ya kuzindua TTCL Pesa hivyo kufikisha watoa huduma sita sokoni.

Tangu mwaka 2008 kampuni za simu zilipoanza kutoa huduma za fedha kumekuwa na ongezeko kubwa la wateja wa huduma hizo kwa kutumia simu za mkononi pengine kutokana na urahisi, ufanisi na mazingira rafiki yanayochangiwa na mfumo wa kidijitali unaotumika kuzifanikisha.

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha hadi Machi kulikuwa na jumla ya watumiaji milioni 19.3 huduma hizo kati ya wateja milioni 40 wa simu za mkononi waliosajiliwa nchini.

Kampuni sita za mawasiliano zimekuwa na mchango mkubwa wa kufikisha huduma za fedha kwa wananchi zikizizidi benki za biashara na taasisi za fedha 58 zilizopo nchini.

Takwimu za Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) zinaonyesha mpaka mwaka jana, ni asilimia 16.9 pekee ya Watanzania walikuwa wanapata huduma za fedha kutoka benki wakati wale wanaotumia simu za mkononi wakiwa asilimia 58.

Gharama za huduma

Ingawa benki za biashara nazo zinazo huduma kupitia simu za mkononi, upo ushindani kati ya Vodacom, Tigo na Airtel. Mipango ya kuwa wateja wengi wanaofanya miamala mingi zaidi inaihusisha pia Halotel, Zantel na TTCL.

Mchuano uliopo kati ya watoa huduma hao sita, unaiweza Tanzania miongoni mwa mataifa yaliyo na huduma bora za fedha kupitia simu za mkononi duniani.

Mpaka sasa M-Pesa ndiyo inayotawala zaidi soko ikihudumia asilimia 43 ya wateja wote zaidi ya milioni 19.3 ikifuatiwa na Tigo Pesa yenye asilimia 36 kisha Airtel Money kwa asilima 17. Licha ya kuchelewa kuingia sokoni, Halo Pesa ina asilimia tatu ya wateja wote ikiishinda Ezy Pesa yenye asilimia moja na TTCL Pesa iliyoanza kwa asilimia 0.4.

Pamoja na hayo, wateja wa kampuni hizo za simu wanasema licha ya ufanisi wa huduma hizo, gharama za kufanikisha kila muamala ni kubwa na kwamba endapo zingepunguzwa huenda basi ushindani wa sekta ya fedha ungeongezeka.

Wengi waliamini kuwa kama ilivyo kawaida kuimarika kwa soko kungelipunguza gharama za uendeshaji hivyo huduma kupatikana kwa unafuu lakini katika biashara ya miamala ya simu hilo limekuwa tofauti kutokana na kampuni husika kuongeza gharama za huduma mara kwa mara.

Martin Joseph, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam anasema gharama zilizopo sasa ni kubwa tofauti na ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

“Wakati mwingine ni bora kutumia benki kwani zina makato madogo tofauti na mitandao ya simu. Ukitoa fedha kwenye ATM unatozwa chini ya Sh1,000 lakini fedha hiyo ukiichukua kutoka wakala wa kampuni ya simu utakatwa mpaka Sh6,500,” anasema Joseph akitoa mfano wa kukamilisha muamala wa Sh400,000.

Kwa kuwa simu za mkononi ni kimbilio la wengi, anasema kampuni zinazotoa huduma zinapaswa kuwa nafuu ili kila mtu afurahie mapinduzi ya Teknolojia ya Habari na Mwasiliano (Tehama).

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini mteja anayetaka kutoa Sh100,000 katika mitandao wowote kati ya sita iliyopo atatakiwa kulipa Sh2,300 ambacho ndicho kiasi kidogo zaidi huku kampuni nyingine zikitoza hadi Sh3,600.

Kufanikisha muamala kwa simu, kuna wateja wa aina tatu. Wapo waliosajiliwa, wasiosajiliwa na ama kutuma ndani ya mtandao au nje.

M-Pesa

Vodacom yenye wateja milioni 12.87 ina watumiaji milioni 8.2 wa M-Pesa waliosajiliwa ambao hutozwa kuanzia Sh300 wanapotoa kati ya Sh1,000 hadi Sh2,999 kwa wakala wa huduma hizo kiasi ambacho hufika Sh8,000 fedha hizo zinapozidi Sh800,000.

Gharama ya kutuma fedha kwa wateja waliosajiliwa ndani ya mtandao na washirika wao wa biashara huanzia Sh10 kuanzia Sh1,000 na Sh5,000 kinachozidi Sh1 milioni.

Hata hivyo gharama za kutuma fedha kwa namba ambazo hazijasajiliwa ni ghali zaidi kwani kufanya hivyo kati ya Sh1,000 hadi Sh2,000 mteja hutozwa Sh375 na Sh11,300 anapotuma kati ya Sh800,000 hadi Sh1 milioni.

Tigo Pesa

Kati ya wateja milioni 11.32 wa Tigo, zaidi ya nusu, milioni 6.95 wamejisajili kutumia Tigo Pesa ambao hutozwa kuanzia Sh350 wapotoa kuanzia Sh1,000 hadi Sh2,999 na Sh8,000 kwa zaidi ya Sh800,000.

Wanapotaka kutumiana ndani ya mtandao na washirika, wateja hao hutozwa kuanzia Sh10 kwa muamala wa Sh100 hadi Sh999 na Sh5,000 kwa muamala unaoanzia Sh1 milioni hadi Sh3 milioni.

Airtel Money

Mpaka Machi, takwimu za TCRA zinaonyesha Airtel ilikuwa na zaidi ya wateja milioni 10.99 huku zaidi ya milioni 3.23 wakisajiliwa kutumia Airtel Money hivyo kutozwa kuanzia Sh300 wanapotoa kati ya Sh1,000 hadi Sh2,999. Wanapotaka kutoa zaidi ya Sh800,000 kutoka kwa wakala wa huduma hiyo hulazimika kulipa zaidi ya Sh8,000 kulingana na ukubwa wa muamala.

Wateja wa Airtel Money hutozwa kuanzia Sh5 wanapotuma kiasi kisichozidi Sh1,000 huku wakilipa Sh1,000 kwa muamala unaoanzia Sh200,000. Hata hivyo, kutuma kuanzia Sh200,000 ndani ya Airtel Money ni bure.

Aidha, wateja wanaotuma fedha kwa namba ambayo haijasajiliwa au nje ya washirika wa biashara gharama mpokeaji hakatwi fedha yoyote wakati wa kutoa kiasi alichopokea.

Halo Pesa

Halotel ilianza kutoa huduma zake nchini mwaka 2015 na mpaka Machi, TCRA inaonyesha ilikuwa na zaidi ya wateja milioni 3.55 huku 609,770 wakisajiliwa kutumia Halo Pesa.

Takwimu zinaonyesha gharama ya kutoa fedha katika mtandao huo mchanga nchini ni Sh275 mteja anapohitaji kati ya Sh1,000 hadi Sh1,999 na hufika Sh6,800 kwa muamala unaozidi Sh1 milioni.

Kutuma kati ya Sh100 hadi Sh999 kwa mteja mwingine aliyesajiliwa ndani ya mtandao gharama huwa Sh8 na kiasi kinapozidi Sh1 milioni gharama hizo huzidi Sh3,500.

Kumtumia Sh1,000 hadi Sh1,999 mteja wa Halo Pesa asiyesajiliwa gharama huwa Sh350 na kati ya Sh900,000 hadi Sh1 milioni ni Sh8,300.

TTCL Pesa

Kati ya wateja 471,103 wa TTCL, wacha kati yao wanatumia TTCL Pesa. Takwimu zinaonyesha wanaotumia huduma hiyo ya fedha ni 7,980 tu.

Wateja hao, wanapotaka kutoa kati Sh1,000 hadi Sh2,999 hulazimika kulipia Sh350 na Sh7,000 wanapotoa kati ya Sh1milioni hadi Sh3 milioni kutoka kwa wakala yeyote nchini.

Mteja wa mtandao huu akitaka kutuma Sh100 hadi Sh999 kwa mwenzake hulipia Sh5 gharama zinazoongezeka mpaka Sh2,800 anapotuma kati ya Sh1 milioni hadi Sh3 milioni.

Wanapotuma kati ya Sh1,000 hadi Sh1,999 kwa wateja wasiosajiliwa hulipia Sh350 au Sh9,000 wanapotuma kati ya Sh900,000 hadi Sh1 milioni.