Wanawake 100 kupatiwa mkopo wa ng’ombe Mbarali

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dk Titus Kamani (kushoto) akitoa maelekezo kwa uongozi wa Kijiji cha Matebele wilayani Mbarali mkoani Mbeya alipokuwa akikagua ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho jana. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

Mpango wa unywaji wa maziwa shuleni unatarajiwa kuzinduliwa Wilaya ya Mbarali

Mbarali. Wanawake zaidi 100 wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebele wilayani hapa Mkoa wa Mbeya watanufaika na mkopo wa ng’ombe na elimu ya usindikaji wa maziwa kupitia mradi wa Uendelezaji wa Sekta ya Maziwa Afrika Mashariki (EADD).

Meneja wa mradi wa EADD Tanzania, Mark Tsoxo alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa Umoja wa Wafugaji Matebele (Uwarama) uliofanyika kijijini humo baada ya uzinduzi wa unywaji wa maziwa uliozinduliwa na Mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Ushirika Tanzania, Dk Titus Kamani.

Akizungumza katika mkutano huo, Tsoxo alisema lengo la kutoa elimu na mikopo ya ng’ombe kwa wanawake ni kuwawezesha kuongeza kasi ya uzalishaji sambasamba na usindikaji jambo litakalochangia kuwaongezea kipato na kuondokana na mfumo dume.

“Mkopo huo maarufu kama ‘Kopa ng’ombe lipa ng’ombe’ utakuwa chachu kwa wanawake walio katika umoja kwa lengo la kuchangia uzalishaji wa maziwa kuwa mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwatafutia soko la uhakika,” alisema Tsoxo.

Pia, alisema wanatarajia kuzindua mpango wa unywaji wa maziwa shuleni katika Wilaya ya Mbarali hasa kijiji cha Matebele na kwamba wanafunzi watakuwa wakinywa maziwa mara mbili kwa wiki jambo litakaloimarisha afya zao na kuwa wasikivu katika masomo.

Kwa upande wake, Dk Kamani alionya viongozi wa ushirika kuacha tamaa za mali za wanachama na kwamba Serikali haitowavumilia.

“Nimepewa kitengo hiki na mheshimiwa Rais John Magufuli, sitaki kusikia viongozi mnavunja umoja wenu kwa masilahi ya watu wachache kwa kweli hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kurejesha mali za wanachama ambazo zitabainika kupotea,”alisema.

Aliwataka viongozi wa Uwarama kuongeza nguvu kwa kushirikiana na wanachama ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika uzalishaji, masoko na biashara.

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Jeremia Temu alisema ili kufikia malengo waliyokusudia ya wafugaji kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, wameweka mikakati kwa kushirikiana na Uwarama kuanza kupandikiza ng’ombe kwa njia ya chupa ili kuzalisha mbegu chotara za ng’ombe wa maziwa.

“Upandikizaji huo utakuwa chachu ya kuongeza idadi ya mifugo katika kijiji hicho kwa kuwa wana maeneo makubwa ya malisho sambasamba na kupatiwa elimu ya kutunza malisho yatakayotumika katika kipindi cha kiangazi,” alisema Temu.

Makamu mwenyekiti wa Uwarama, Philip Oyeelayi alisema wametenga eneo lenye ukubwa wa eka 32,000 kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi hususan maeneo ya malisho na makazi.