Wasomi wakosoa mjadala uchumi wa viwanda

Dodoma. Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa Razack Lokina amekosoa mijadala ya uchumi wa viwanda inayofanyika nchini bila kuwagusa wakulima ambao ni wateja wa bidhaa zitakazozalishwa.

Profesa Lokina akizungumza jana kwenye kongamano la wanataaluma wa Chuo cha IRDP, alisema nchi inapopanga kujenga viwanda inaangalia soko la ndani. “Tunaangalia kuna nini na tunazalisha nini, kwa hiyo wanataaluma tunatakiwa kuangalia ni maeneo gani yanaweza kuwa mwafaka kwa nchi,” alisema.

Alisema takriban asilimia 70 ya Watanzania wako vijijini na wanategemea kilimo, hivyo huko ndiko soko kubwa lilipo. Alisema kinachotakiwa kuangaliwa ni kipato chao ambacho kwa kiasi kikubwa kinategemea kilimo.

“Ndiyo maana ninasema tunazungumza viwanda, lakini kilimo kisije kikasahaulika. Ni vyema kukawa na mijadala mikubwa ya namna ya kuongeza uzalishaji kwa wakulima ili kipato chao kiongezeke. Ukisahau kilimo wakati mwingine viwanda vitakosa malighafi ambazo zinatakiwa kutoka kwa wakulima,” alisema.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi aliyeshiriki kongamano hilo alisema wengi wakiwamo wanasiasa wamekuwa wakitaka viwanda vijengwe maeneo ambayo malighafi zinazalishwa.

Hata hivyo, alisema kitaalamu uamuzi wa kiwanda kijengwe eneo gani unahusisha mambo mengi na siyo upatikanaji wa malighafi za uzalishaji kwenye kiwanda husika pekee.

“Unaweza kuwa na malighafi, lakini mambo mengine yanayohitajika kuwezesha uwapo wa viwanda yasiwepo. Kuna suala la umeme huko vijijini kwetu, wengi tunajua tatizo la nishati hiyo na masuala ya usafirishaji,” alisema.