Wataalamu huru kufanya uchunguzi eneo la mradi wa bomba la mafuta

Muktasari:

Lengo la kutuma wataalamu hao wasiofungamana na upande wowote ni kujiridhisha kabla ya kuanza kazi ya ujenzi wa bomba hilo ili mradi huo ujulikanao kwa jina la Eacop usiitie doa kampuni hiyo na mshirika wake Tullow katika sura ya kimataifa.

Kampuni ya mafuta ya Total yenye makao makuu Ufaransa ambayo ni miongoni mwa wajenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga imetuma timu ya wataalamu huru kuchunguza kama kuna malalamiko kuhusu fidia na tathmini ya athari za mazingira na kijamii.

Lengo la kutuma wataalamu hao wasiofungamana na upande wowote ni kujiridhisha kabla ya kuanza kazi ya ujenzi wa bomba hilo ili mradi huo ujulikanao kwa jina la Eacop usiitie doa kampuni hiyo na mshirika wake Tullow katika sura ya kimataifa.

Habari zilizothibitishwa na kiongozi wa timu hiyo, Luc Zandviliet kutoka kampuni ya Triple R Alliance yenye makao yake nchini Uholanzi, itakutana na makundi yote yanayohusiana na mradi huo.

Makundi hayo ni wakazi wa vijiji ambavyo bomba la mafuta litapita, maofisa wa idara za Serikali, wawakilishi wa asasi za kiraia zinazohusiana na mazingira, wanawake, haki za binadamu na viongozi wa maeneo husika.

“Sisi ni kampuni huru, tumeombwa kuja kujua hofu, shaka, wasiwasi na matarajio ya wanajamii walio kwenye maeneo linakopita bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga, halafu tutayafikisha kama yalivyo,” alisema Zandviliet.

Mtaalamu huyo alisema itakapokusanya taarifa hizo, kampuni ya Total itakaa na serikali za Uganda na Tanzania kujadili ili kuepusha malalamiko ambayo yanaweza kuutia doa mradi mzima wa bomba la mafuta.

Timu ya wataalamu hao ilishatembelea maeneo kadhaa ikiwamo kata ya Chongoleani ambako ilikutana na wananchi waliofidiwa kupisha mradi, viongozi wa Serikali za vijiji; Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa na wawakilishi wa baadhi ya asasi za kiraia.

“Kuna sheria na sera za ardhi za nchi husika na zina viwango vyao vya fidia, Total inaweza kuzishauri nini kifanyike ili maisha ya waliopisha ardhi yawe bora zaidi,” alisema Zandviliet.

Mwakilishi wa mradi wa Eacop nchini Tanzania, Theophil Selestine alisema ufuatiliaji huo unaweza kuwasaidia kujua malalamiko ya jamii iliyopisha ujenzi wa bomba la mafuta.

“Katika mradi mkubwa kama huu ni wazi kwamba hayakosekani malalamiko. Yanapokuja, kampuni isiyo na upande wowote hutathmini mapokeo ya wananchi juu ya mradi . Hii inatusaidia kutambua nini kifanyike ili usiingie dosari kimataifa,” alisema Selestine.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusiana na mradi huo walisema kuna mambo mengi yameanza kujitokeza ikiwamo kwa kampuni za kitapeli ambazo zinakusanya fedha kwa vijana kwa ahadi ya kuwapa ajira wakati mradi huo itakapoanza.