Watoto wa familia moja waliotoweka kwa siku mbili wakutwa wamekufa kwenye gari

Muktasari:

Watoto watatu wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia kwenye gari bovu aina ya Toyota Mark X baada ya kutoweka Oktoba 15, 2018 katika mtaa wa Njaro wilayani Temeke jijini Dar es Salaam


Dar es Salaam. Watoto watatu wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia kwenye gari bovu aina ya Toyota Mark X baada ya kutoweka Oktoba 15, 2018 katika mtaa wa Njaro wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Miili ya watoto hao, Jamila Mohamed (9), Amina Kunambi (7) na Yusuph Selemani (2) imepatikana leo saa 4 asubuhi Oktoba 17, 2018.

Akizungumza na MCL Digital leo babu wa watoto hao, Seif Mayumba amesema wajukuu zake walikwenda kumsalimia lakini baadaye wakaondoka na hawakuonekana tena.

Amesema alipatwa na mshangao alipowakuta wamefariki dunia kwenye gari kwa sababu baada ya kuondoka hawakuonekana.

"Leo asubuhi nilikuwa nasikia harufu kali nikadhani kuna panya au njiwa amekufa. Nikaanza kutafuta ili nitoe, ghafla nikaona nzi wengi chini ya gari, akili ikanituma nifungue mlango,” amesema Mayumba.

"Baada ya kufungua mlango ndipo nikakutana na mjukuu wangu mkubwa akiwa kichwa chini miguu juu. Basi nikapiga kelele, watu wakajaa, tukashauriana tuite polisi.”

Mayumba ambaye ni mlinzi katika nyumba lilipokuwa limeegeshwa gari hilo amesema polisi walifika eneo la tukio na kuchukua miili ya watoto hao huku yeye akichukuliwa kwa ajili ya kuhojiwa kituo cha polisi cha Chang'ombe.

Jirani na shuhuda wa tukio hilo, Hadija Athuman amesema siku walipopotea watoto hao, walishirikiana mtaa mzima kuwatafuta lakini hawakuonekana.

Amesema wameshangaa leo watoto hao wakipatikana wakiwa wamekufa.

"Sijui watoto wetu watakuwa wanachezea wapi, hivi vifo sio vya kawaida. Mimi naogopa sana, juzi tu walikuwa wanacheza na mwanangu hapa uwanjani, leo tumeokota maiti zao, " amesema mwanamke huyo huku akitokwa machozi.