Watumishi wa umma Tanzania wapigwa ‘stop’ kutumia mitandao

Muktasari:

  • Ni wale wanaotumia mitandao ya kijamii ofisini wakati wa kazi

Serikali ya Tanzania imezuia matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watumishi wa umma wakati wa kazi kwa madai yanaathiri kasi ya mtandao wa intaneti ya Serikali.

Pia, imedai watumishi wengi wanapoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuliko kutekeleza majukumu yao.

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk Laurean Ndumbaro kwa taasisi zote za umma, imeonya juu ya matumizi mabaya ya mitandao ya mawasiliano ya Serikali na kwamba, hatua hiyo imelenga kudhibiti matumizi ya mitandao.

“Kasi ya mtandao wa Serikali inapungua kutokana na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii hususan inayopakua video, mfano “YouTube” na hivyo kusababisha watumishi wengine wanaotumia mtandao wa intaneti wa Serikali katika kutekeleza majukumu yao kuathirika,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Aidha, taarifa hiyo inaeleza juu ya upakuaji wa nyaraka zenye hatimiliki bila idhini ya wamiliki kwa kutumia Intaneti ya Serikali kinyume na utaratibu.

“Mitandao ya kijamii haitapatikana kwenye intaneti ya Serikali wakati wa muda wa kazi kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri,” inaeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, Menejimenti ya Utumishi imezitaka taasisi zenye mahitaji maalumu ya matumizi ya mitandao ya kijamii wakati wa saa za kazi, kuwasilisha maombi yao kwa katibu mkuu wa utumishi yakiambatana na sababu za maombi hayo.

“Watumishi wa umma hawataweza kupakua nyaraka, picha na video zenye hatimiliki kwenye intaneti ya Serikali bila idhini ya wamiliki.”

Kwa mara kadhaa, Serikali imekuwa ikitoa miongozo ya matumizi ya Tehama kwa taasisi za Serikali ikiwamo kukataza matumizi ya mitandao kupitia intaneti ya Serikali saa za kazi.