Jafo ataka mwendokasi zilizoharibika kutengenezwa

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali  Suleiman Jafo amesema magari ambayo yameharibika kutokana na mvua wiki hii ni zaidi ya 30 hivyo yatengenezwe na  ifikapo Alhamisi  yaanze kutoa huduma na kuwaondolea adha abiria.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleimani Jafo ameagiza watoa huduma ya mabasi yaendayo Haraka (Udart) kuhakikisha wanatengeneza magari yaliyoharibiwa na maji ya mvua ili ifikapo Alhamisi , mabasi hayo yatoe huduma na kuwaondolea adha abiria.

 

Akizungumza leo Oktoba 29, Waziri  Jafo amewataka viongozi wa Mradi wa Uendelezaji Miji ya Mkakati Tanzania (TSCP) Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Wakala wa Barabara (Tanroads) na manispaa ya Kinondoni kukutana  ili kuja na ufumbuzi wa muda mfupi wa kudhibiti maji katika eneo la Jangwani.

 

Jafo amesema Udart wanatakiwa kuhakikisha ifikapo Jumanne   vipuri vilivyoagizwa vimewasili na matengenezo ya magari yaliyoathiriwa na mvua yatengenezwe ili kurejea barabarani.

 

Kwa nyakati tofauti, fundi mwandamizi wa Udart, Ally Ganzo amesema kuwa vipuri vilivyoagizwa vitawasili Jumanne na kwamba kuanzia Jumatano mabasi yaliyoharibika yatatengemaa.

 

 Mkuu wa maofisa usafirishaji wa Udart, Albert Masai akielezea   changamoto ya utengenezaji wa magari hayo amesema  miundombinu siyo rafiki na kuwa kazi hiyo ingekamilika baada ya wiki moja au mbili.

 

Kutokana na kupokea maelezo tofauti, Jafo amesema: “ Mbona mnatao taarifa tofauti tena ni wataalamu wa taasisi moja, sasa naagiza ikifika Jumanne vifaa vilivyoagizwa viwe vimefika,  nataka ikifika Alhamisi hali ya usafiri irejee katika hali ya kawaida na kupunguza usumbufu kwa wananchi.

 

Aidha, Jafo pia amewataka Udart kuondoa mabasi yaliyoko yadi ili kuepusha madhara zaidi jambo ambalo limefanya wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka(DART) kutoa eneo la Gerezani ambalo litatumika kuegesha magari hayo kwa muda.’

 

“Mvua bado hazijaisha, hivyo yaondoeni magari kwenye yadi. Mvua hizi magari zaidi ya 30 yameharibika, sasa mvua bado zinanyesha tusipochukua tahadhari mabasi zaidi yanaweza kuharibika hivyo mradi kushindwa kufanya kazi,” amesema.

 

Jafo pia ametaka DART na Udart kukutana na Jeshi la Polisi ili kuja na namna ya kusaidia mabasi yaendayo haraka yasitumie muda mrefu kwenye makutano hivyo kuweza kuhudumia wananchi kwa haraka na kuwaondolea adha.

 

Awali, Mtendaji Mkuu wa DART, Ronald Lwakatare amesema pamoja na kuwa na idadi ndogo ya mabasi barabarani, inaweza kupunguza adha kwa wananchi endapo mabasi hayo hayatakaa muda mrefu kwenye makutano, hivyo kupunguza muda unaotumiwa na gari na kuharakisha mzunguko.

 

Katika hatua nyingine, Jafo amesema pamoja na kutambua kuwapo kwa Mradi ya Uendelezaji wa Jiji (DMDP) ambao umelenga kuboresha eneo la Jangwani, alizitaka taasisi nne za TSCP, Dawasa, Tanroads na manispaa ya Kinondoni kuja na njia ya kukabiliana na mafuriko.

 

“Tatizo hapa eneo ambalo watu walikuwa wanaishi pametengeneza mlima wa mchanga ambao umezuia utiririkaji wa maji jambo ambalo linaathiri barabara si kwa mabasi yaendayo haraka pekee bali hata wananchi ambao wanatumia barabara hiyo ambao walilazimika kutumia njia ndefu,” amesema.