Waziri wa Fedha aliamsha bandarini

Muktasari:

Dk Mpango ameagiza TRA kufanya mabadiliko makubwa ya watumishi idara ya upimaji na ukaguzi wa mizigo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufanya mabadiliko makubwa ya watumishi wa idara ya upimaji na ukaguzi wa mizigo katika Kituo cha Forodha cha Bandari ya Dar es Salaam.

Ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika kituo hicho na kubainika kuwa baadhi yao wanajihusisha kwa namna moja au nyingine na upotevu wa mapato ya Serikali.

Taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango imesema waziri ametoa muda wa siku saba kwa TRA kumpa taarifa kamili ya utekelezaji wa agizo hilo, ikiwemo kuwahamisha watumishi wote waliokaa muda mrefu kwenye eneo la upimaji na ukaguzi wa mizigo ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya Serikali katika bandari hiyo.

 

Dk Mpango ameeleza kushangazwa na mapato katika Bandari ya Dar es Salaam kutoongezeka licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali za kuboresha bandari hiyo kutokana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kodi ya Serikali.

“Pamoja na kuwepo kwa mitambo ya kukagua mizigo (scanners), baadhi ya bidhaa zinakadiriwa kodi ndogo ikilinganishwa na thamani ya mizigo, huku mizigo mingine ikiwa si ile iliyotajwa kuwemo kwenye makontena na hupitishwa na watumishi wasio waaminifu,” amesema.

Waziri ameagiza TRA kuhakikisha wanaongeza mapato katika bandari ya majahazi kutoka wastani wa mapato ya Sh3.5 bilioni kwa mwezi hadi Sh5 bilioni kulingana na malengo yaliyowekwa baada ya kubainika kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa mapato ya Serikali katika eneo hilo.

Dk Mpango ameagiza TRA kuhakikisha bandari ya majahazi inatumia mfumo wa kukusanya mapato wa Tansis ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.

Pia, ameviagiza vyombo vya dola kuwachunguza watumishi wote wakiwemo wa ngazi za juu katika idara ya forodha bandarini na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoikosesha Serikali mapato.