Wema Sepetu amleta Bongo Van Vicker, asimulia walivyokutana

Muktasari:

  • Van Vicker ni mwigizaji wa Ghana aliyeshirikishwa katika filamu  mpya ya D.A.D ya Wema Sepetu ametua Tanzania jana kwa ajili ya uzinduzi wa filamu hiyo.
  • Filamu hiyo ilikuwa izinduliwe miaka mitatu iliyopita, sasa inazinduliwa Septemba 28, 2018 siku ambayo Wema atakuwa akitimiza umri wa miaka 30.


Supastaa wa Bongo Movie, Wema Sepetu alfajiri ya leo amempokea mwigizaji wa Ghana, Van Vicker tayari kwa aajili ya uzinduzi wa filamu yao ya pamoja utakaofanyika keshokutwa,  Septemba 28, katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi wa filamu hiyo iliyobatizwa jina la D.A.D unakuja miaka mitatu tangu walipoigiza huku Wema akisema Mghana huyo ndio chanzo cha kuichelewesha kuingia sokoni kwa kuwa amekuwa na mambo mengi kiasi cha kuwafanya wakwaruzane mara kwa mara.

Mbali na uzinduzi wa filamu, Wema atakuwa anasherehekea kutimiza umri wa miaka 30.

“Van Vicker ni rafiki yangu lakini hapo katikati tumekuwa tukikwaruzana mara kwa mara kwa sababu kila nikimwambia filamu inabidi iingie sokoni mara ataniambia hivi mara vile, lakini  siku zote alikuwa ananiambia anataka tufanye kitu kizuri,” anasema.

Awali filamu hiyo ilikuwa izinduliwe Juni 30 mwaka huu lakini aliahirisha baada ya Van Vicker kusema hatahudhuria kutokana na kubanwa na shughuli nyingine.

Akizungumzia namna walivyokutana anasema alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi katika mtandao wa Instagram akimuomba wafanye kazi pamoja na baada ya muda mfupi alimjibu hata yeye angefurahi kufanya kazi naye.

“Baada ya kumtumia ujumbe mfupi alinipa namba yake ya simu, tulizungumza namna tutakavyofanya kazi, kwa sababu nilitaka kufanya kazi kimataifa nilimwambia lazima niende Ghana akakubali. Nakumbuka nilikaa wiki mbili kule wakati wa kutengeneza filamu hii.”