Wenye uwezo kutopata mikopo vyuo vikuu

Rais John Magufuli 

Muktasari:

Rais pia amesema tayari Serikali imeshatoa Sh80 bilioni za mwanzo kwa ajili ya kukalibiana na changamoto ya mikopo, akiitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESLB) na bodi nyingine zinazohusika kuhakikisha wanafunzi wenye sifa tu ndiyo wanaopata mikopo.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali haitawakopesha wanafunzi wenye uwezo kwa sababu mikopo hiyo ni kwa ajili ya watoto maskini.

Rais pia amesema tayari Serikali imeshatoa Sh80 bilioni za mwanzo kwa ajili ya kukalibiana na changamoto ya mikopo, akiitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESLB) na bodi nyingine zinazohusika kuhakikisha wanafunzi wenye sifa tu ndiyo wanaopata mikopo.

Rais Magufuli amesema hayo wakati vyuo vya elimu ya juu vikianza masomo, huku baadhi ya wanafunzi, hasa wa mwaka wa kwanza, wakiwa hawajui wamepitishiwa asilimia ngapi ya mkopo, na wengine kutojua kama watapata au hawatapata fedha hizo.

Juzi, HESLB ilisema imefanya marekebisho katika mfumo wa utoaji mikopo kwa kurejesha wa zamani ambao utawafanya wanafunzi wote wapate fedha sawa za kujikimu na tofauti iwe kwenye ada ya masomo tu.