Monday, July 17, 2017

Wilaya za Rombo, Same zamliza Mghwira

 

By Janeth Joseph, Moshi mwananchipapers@mwananchi.tz

Moshi. Zikiwa zimepita takribani wiki tatu, tangu Rais John Magufuli aseme wasichana watakaopata mimba wakiwa shuleni hawataendelea na masomo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira, amezitaja wilaya za Rombo na Same kuwa zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wajawazito akisema hali hiyo inazorotesha sekta ya elimu. 

Mgwira alisema hayo jana katika kongamano la 10 la kimataifa la  taasisi ya New Life Foundation lililofanyika mkoani hapa ambalo lilijumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini na wafadhili kutoka nchi za Marekani, Korea ya Kusini na Uholanzi.

Alisema ni wajibu wa wazazi kuwapa elimu ya kutosha mabinti zao kuhusiana na athari za mimba za utotoni, pamoja na kutokujihusisha na mapenzi wawapo masomoni.

 “Sisi viongozi hatutachoka kusema hayo, ninyi wazazi ambao pia mnahusika katika kuwalea watoto, wapeni ushauri wazingatie masomo huku wakiachana kabisa na masuala  ya mapenzi ambayo ni ya watu wazima,” alisema.

 Alimpongeza Mkurugenzi wa New Life Foundation Askofu Glorious Shoo, kwa kuitikia wito wa Rais John Magufuli katika kuboresha sekta ya elimu.

“Nikupongeze Baba Askofu katika jitihada unazofanya katika kuboresha sekta ya elimu maana kazi hii Serikali haiwezi kuifanya peke yake,” alisema Mghwira na kuongeza Serikali inahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Mkurugenzi wa New Life Foundation, Askofu Shoo alisema dhumuni la kongamano hilo ni kuchochea watoto kuwa na uhusiano wa ndani zaidi na Mungu na kuipenda elimu.

Askofu Shoo  alisema taasisi  hiyo ipo kwa ajili ya kuziba mapengo yote ya watoto waliotupwa na kutelekezwa na wazazi wao.

Mkurugenzi wa Chuo cha Hebron Christian cha nchini Uholanzi, Geoff Mathews alisema kuwa wamekuwa wakitoa misaada kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wanaoanzia miaka mitano hadi 18.

“Tayari tumeshatoa misaada yenye thamani ya Dola za Marekani 374,000 kwa watoto 42 kati ya mwaka 2006 hadi 2017, kupitia wafadhili 46,” alisema.

-->