Wizara zinazodaiwa na Uhuru matatani

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba na baadaye katika kampuni ya Uhuru inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo ambako aliagiza apelekewe orodha ya wizara zote zinazodaiwa na kampuni hiyo ili azikate yeye mwenyewe.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameahidi kuzikata fedha wizara zote zinazodaiwa fedha na kampuni ya magazeti ya Uhuru Publications Ltd ili aweze kulipa deni la Sh1.6 bilioni ambalo limelimbikizwa kwa muda mrefu.

Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba na baadaye katika kampuni ya Uhuru inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo ambako aliagiza apelekewe orodha ya wizara zote zinazodaiwa na kampuni hiyo ili azikate yeye mwenyewe.

Dk Magufuli ambaye alifanya ziara kama mwenyekiti wa CCM, alitoa ahadi hiyo baada ya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi kwamba hawajalipwa mishahara yao kwa kipindi cha miezi saba sasa tangu Februari mwaka huu sababu ikiwa ni deni la Sh1.6 bilioni zilizoko mikononi mwa wizara.

Wafanyakazi hao walimweleza Rais Magufuli kuwa wanaidai kampuni malimbikizo ya mishahara ya miezi saba ambayo imefikia kiasi cha Sh 607 milioni hali iliyowasababisha kufanya kazi katika mazingira magumu.

Kaimu Mhariri mtendaji wa kampuni hiyo, Ramadhani Mkoma alimweleza Rais Magufuli kuwa sababu ya kushindwa kuwalipa wafanyakazi hao mishahara yao inatokana na wizara kutolipa deni lililofikia kiasi cha Sh1.6 bilioni.

Ziara

Rais Magufuli alifanya ziara hiyo ya kushtukiza katika ofisi za chama hicho saa 3.30 asubuhi na akatia saini katika kitabu cha mahudhurio kisha alikwenda ofisini kwake ambako alikutana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka.

Hata hivyo haikuweza kufahamika kilichozungumzwa kati yake na viongozi wengine wa chama hicho. Alitoka ofisi kwake saa 6.28 mchana na akaenda kukutana na wafanyakazi na waandishi katika chumba cha habari cha magazeti ya Kampuni ya Uhuru.

Miongoni mwa wafanyakazi walioelezea kwa kina hali ya kampuni, kero za mishahara na kuuzwa kinyemela kwa mtambo ni Mkoma, mwandishi Selina Wilson na Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi tawi la Uhuru, Moses Makambi.

Mahojiano

Mkoma: Mheshimiwa Rais biashara ya magazeti imekuwa siyo nzuri kwa sababu hatujalipwa madeni ya Sh1.6 bilioni tunazozidai wizara zote.

Rais Magufuli: Sasa naomba uniorodheshe wizara zote zinazodaiwa leo hii (jana) nizipate na mimi nitawakata mwenyewe.

Wilson: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wafanyakazi wa kampuni ya Uhuru hatujalipwa mishahara yetu sasa ni mwezi wa saba.

Rais Magufuli: Kwa hiyo mnaishije kama hamlipwi mishahara?

Wilson: Tunaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

Makambi: Mheshimwa Mwenyekiti tunaishi katika mazingira magumu. Tunashindwa hata kusomesha watoto wetu katika shule nzuri kwa kukosa fedha, kwa kweli tuna hali ngumu. Tulikuwa na mtambo (Mordern Newspaper Printers Limited) wetu wa kuchapisha magazeti lakini umeuzwa kinyemela kama chuma chakavu na sasa tunaenda kuchapisha magazeti yetu katika kampuni ya Jamana kwa gharama ya Sh52 milioni kwa mwezi.

Rais Magufuli: Umeuzwa wapi? Na nani aliuza? Eti katibu mkuu unazo hizi taarifa?

Kinana: Mheshimiwa Rais, mtambo huu uliuzwa tangu mwaka 2011. Ulikuwa haufanyi kazi kwa kipindi cha miaka saba.

Rais Magufuli: Sasa huo mtambo ulikuwa hautengenezeki mpaka mkaamua kuuza kama chuma chakavu?

Mkoma: Mheshimiwa Rais mtambo huo ulikuwa hautengenezeki kwa sababu ulikuwa mbovu na ulikuwa unaiingizia hasara kampuni. Kutokana na hali hiyo bodi ilikaa na kupendekeza mtambo huo ulionunuliwa kwa Sh200 milioni kutoka Bulgaria uuzwe kama chuma chakavu kwa Sh 6milioni.

Rais Magufuli: Mwenyekiti wenu wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hii ni nani?

Mkoma: Mheshimiwa Adam Kimbisa

Rais Magufuli: Anafahamu hili na mwenyekiti huyu wa bodi anateuliwa na nani?

Kinana: Mheshimiwa Rais anateuliwa na Kamati Kuu na pia Kamati Kuu ndiyo inatengua wadhifa wake.

Rais Magufuli: Basi nikikaa na Kamati Kuu nitaweza kuteua mwenyekiti.

Pia, wafanyakazi hao waliichongea bodi hiyo kwa Rais Magufuli kuhusu wafanyakazi watano waliosimamishwa kazi kwa muda wa miezi mitatu lakini mpaka sasa wanaendelea kulipwa mishahara hivyo kuisababishia hasara kampuni kiasi cha Sh40 milioni kutokana na kuendelea kulipwa kwa mwaka sasa.

“Mwenyekiti kuna wafanyakazi watano walisimamishwa kazi na bodi kwa muda wa miezi mitatu, lakini mpaka sasa wamefikisha mwaka mmoja bado wanaendelea kulipwa mshahara na kuisababishia hasara kampuni ya Sh40 milioni,” alisema Rhoda Kangelo ambaye ni Ofisa Rasilimali Watu.

Wafanyakazi hao walimwambia Rais Magufuli kuwa wanataka wapatiwe mkurugenzi mpya ambaye ataendesha kampuni hiyo kwa faida tofauti na sasa ambapo kampuni hiyo inajiendesha kwa hasara.

Walidai kuwa mkurugenzi aliyekuwepo alisimamishwa kazi baada ya kumsimamisha mmoja wa wafanyakazi wa kitengo cha matangazo aliyebainika kuwa aliibia kampuni Sh 900,000.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaongea ukweli, lakini majina yetu tayari yameandikwa kwa ajili ya kufukuzwa kazi baada ya kuongea hali halisi ilivyo katika kampuni yetu,” alisema mmoja wa wafanyakazi huku wengine wakishangilia na kupiga makofi.

Walidai tatizo kubwa katika kampuni hiyo ni uongozi mbaya na hivyo walishauri mwenyekiti aunde menejimenti mpya ambayo itafanya kazi vizuri. Wafanyakazi hao walisema zaidi ya Sh800 milioni hazijapelekwa NSSF tangu mwaka 2011 hadi sasa.

Maagizo manne

Baada ya kusikiliza matatizo na changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa kampuni hiyo, Rais Magufuli alitoa maagizo ambayo ni kuhakikisha kuwa wafanyakazi hao wanalipwa malimbikizo yote yao ya mshahara wanaodai.

“Nataka malimbikizo ya mshahara wa hawa wafanyakazi yalipwe mwezi huu, watu hawawezi kufanya kazi, wanajitolea halafu wasipewe mshahara wao,” alisema Rais Magufuli.

Pili, aliagiza apelekewe orodha ya wizara zinazodaiwa na yeye atalifanyia kazi suala hilo ikiwemo kukata fedha zinazodaiwa wizara hizo ili zikatumike kuboresha kampuni hiyo. “Nataka orodha hii ije leo… niipate leo na iwe ya ukweli,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliwataka wafanyakazi hao wamwachie yeye suala la utawala kwani atakwenda kukutana na bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo na huko atatoa uamuzi.

“Mimi ndio JPM, niachieni haya matatizo nitayafanyia kazi na mimi haya yote matatizo nilikuwa nayajua hata kama msingeniambia najua,” alisema Rais Magufuli.

Agiza la nne aliahidi kuwanunulia gari kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa waandishi wa habari na wafanyakazi wote kwa ujumla.

Nje ya ofisi

Japokuwa Rais alikuwa katika eneo hilo shughuli mbalimbali ziliendelea kufanyika kama kawaida huku magari yakipita katika barabara ya Lumumba bila kuzuiwa kama ilivyozoeleka kiongozi wa nchi anapopita.

Wakati anaondoka saa 7.10 mchana, nje ya ofisi za CCM na Uhuru wananchi walikuwa wamejipanga kandokando ya barabara wakimsubiri.

Abdallah Swaleh na Ester Lazaro waliliambia gazeti hili kuwa walifurahishwa na hali iliyokuwepo kwani walidai kuwa hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa rais kufika kwenye ofisi hizo.