Yahya Jammeh akubali kuachia madaraka

Kiongozi wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh

Muktasari:

Taarifa za kuondoka kwa kiongozi huyo aliyetawala Gambia kwa miaka 22 zimetolewa na rais anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow kupitia mtandao wake wa Twitter.

Banjul. Gambia. Kiongozi wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh amekubali kuachia madaraka na amesema anaondoka nchini humo kwenda kuishi uhamishoni.

Taarifa za kuondoka kwa kiongozi huyo aliyetawala Gambia kwa miaka 22 zimetolewa na rais anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow kupitia mtandao wake wa Twitter.

Barrow ametangaza hayo baada ya mazungumzo ya saa kadha yaliyonuiwa kumshawishi Jammeh kukubali matokeo ya uchaguzi.

Mataifa ya Afrika Magharibi yamewatuma wanajeshi Gambia na kutishia kumuondoa Jammeh madarakani kwa nguvu iwapo angekaidi amri ya kuachia madaraka kwa hiari.

Barrow amekuwa nchini Senegal kwa takriban wiki moja. Aliapishwa kuwa rais mpya wa Gambia katika ubalozi wa Gambia mjini Dakar Alhamisi iliyopita. Ametambuliwa na jamii ya kimataifa kama kiongozi mpya wa Gambia.