Zitto aitwa polisi Morogoro

Muktasari:

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini yupo katika ziara ya mikoa mbalimbali kwa ajili ya kukagua na kuimarisha uhai wa chama hicho.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameitwa katika Kituo cha Polisi cha Mgeta wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya mahojiano.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini yupo katika ziara ya mikoa mbalimbali kwa ajili ya kukagua na kuimarisha uhai wa chama hicho.

Akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi Februari 22, 2017 Zitto amesema ametakiwa kuripoti katika kituo hicho baada ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), kuagiza aende.

“Hapa ninapozungumza na wewe naelekea kituoni gari yangu ipo mbele ya polisi nyuma. Bado sijajua sababu nini ,”amesema Zitto.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari yenye kichwa cha habari ‘Tuko Kikeo, polisi wametuvamia’, Zitto amesema, “Tumemaliza ziara yetu ya kutembelea Kata ya Kikeo, inayoongozwa na diwani wa chama cha ACT Wazalendo, hapa Halmashauri ya Mvomero, mkoa wa Morogoro.”

“Polisi wametuvamia jioni hii, hawajatueleza wanachokitaka. Tunakwenda nao Kituo cha Polisi Mgeta muda huu kuwasikiliza.”