Wafuasi wa Odinga waandamana Kenya
Muktasari:
- Waandamanaji wamebeba matawi ya miti, mabango mbalimbali
- Mabango hayo yana ujumbe unaotaka Mtendaji Mkuu aondoke
- Ni kuitikia wito uliotolewa jana na kiongozi wao mkuu Raila Odinga
Nairobi, Kenya. Wafuasi wa muungano wa upinzani wa Nasa leo wamefanya maandamano katika baadhi ya maeneo nchini ili kushinikiza kuondolewa kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) anayeshutumiwa kuvuruga uchaguzi wa rais wa Agosti 8.
Maandamano hayo yamefanyika kuitikia wito uliotolewa jana na kiongozi mkuu wa Nasa Raila Odinga kwamba wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kuandamana hadi kwenye makao makuu ya IEBC yaliyoko jengo la Anniversary Towers lengo likiwa kumtoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC Ezra Chiloba kwa madai ya kuhusika kuvuruga uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.
Maandamano hayo yanafanyika siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Katika mji wa Kisumu, ambao unatajwa kuwa moja ya ngome za Nasa baadhi ya wakazi waliandamana hadi ofisi za IEBC na baada ya kufika walitoa wito maofisa wa ngazi za juu akiwemo Ezra Chiloba wajiuzulu.
Walimshutumu Chiloba na kikundi chake kwa kufanya njama za kuingilia mchakato wa uchaguzi mkuu ambao matokeo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta yalifutwa na Mahakama ya Juu.
Waandamanao waliokuwa wamebeba matawi ya miti, mabango huku wakipiga yowe na honi za pikipiki walianzia barabara ya Obote wakaenda mtaa wa Oginga Odinga kabla ya kuchukua Barabara Kuu ya Kenyatta na baadaye Mtaa wa Ang’awa katikati ya jiji.