Maisha ya bibi mwenye miaka 113, bado ana nguvu

Muktasari:

 Wilayani Mpwapwa kuna mfano mzuri na ambao uko wazi, kwani yuko mwanadamu mwenye umri wa miaka 113 ambaye anaishi hadi sasa na anakula vyakula vyote wanavyokula wengine ikiwemo vitu vigumu kama nyama.

HADITHI nyingi katika vitabu vya kale husimulia namna binadamu wa zamani alivyoishi miaka mingi, tofauti na ilivyo sasa.

Hata hivyo kuna ukweli katika maisha ya sasa kuwa watu kutoka baadhi ya mataifa wakiwa wamekula chumvi nyingi zaidi na kuingia katika vitabu vya historia.

 Wilayani Mpwapwa kuna mfano mzuri na ambao uko wazi, kwani yuko mwanadamu mwenye umri wa miaka 113 ambaye anaishi hadi sasa na anakula vyakula vyote wanavyokula wengine ikiwemo vitu vigumu kama nyama.

 Ni katika Mtaa Igovu Kitongoji cha Ng’ambo si mbali kutoka katika makaburi ya wakoloni walioishi Mpwapwa zama hizo, katikati ya nyumba nyingi zilizojengwa kwa matofari ya udongo yupo Bibi ambaye ni maarufu kwa jina la Mdala Aksa liyezaliwa mwaka 1900.

 Aksa au Nyamiti (jina la utoto) ni mzaliwa pekee katika familia ya Marehemu Luwaha pamoja na mkewe aliyeitwa Mkaulugu wote wenyeji wa Mkoa wa Iringa, ingawa yeye anapinga kuwa si Iringa bali ni Uheheni.

 Simulizi zinaonyesha kuwa familia hiyo ilikuwa na ukaribu sana na familia ya shujaa na mtemi wa wahehe Mkwawa ambaye ni mtoto wa Muyugumba.

 Bado anaweza kuzungumza na kusikia bila ya shida yoyote lakini kinachomsumbua ni macho kupungua uwezo wa kuona, pamoja na miguu yake kukosa nguvu ingawa anaweza kutembea kwa msaada. Muda mwingi maisha ya mama huyo ni kulala tu.

Ndani ya nyumba

 Nilipoingia ndani ya nyumba nilipata kusikia mambo mengi, kwanza ni historia ya kikongwe huyo ambaye licha ya kupoteza baadhi ya kumbukumbu, anaonyesha mwenye uelewa mkubwa na masikio yake yanasikia kwa ufasaha na umakini wa hali ya juu.

 Simulizi yake

 “Zinji semigwe ninga……”(mengine nimesahau ila…….) anavuta pumzi na kuanza kusimulia kuwa alizaliwa mkoani Iringa baba yake akiwa ni mhehe na mama yake alikuwa ni mgogo mwenye mchanganyiko wa wahehe na alizaliwa akiwa pekee, kutoka kwa mama yake Mkaulugu.

 

“Nilipozaliwa waliniita jina la Nyamiti lenye maana kuwa (Wadawa) jina ambao linaakisi maisha yangu katika historia ya kuzaliwa kwangu kwani baba na mama yangu walilazimika kunywa madawa ndipo nikazaliwa,” anasimulia.

 

Anasema mara baada ya kuzaliwa alisongwa na mikosi kiasi ambacho wazazi wake walikata tamaa ya mtoto wao huyo kuishi kwani aliugua sana ugonjwa ambao haukufahamika.

Familia ilikimbia makazi yao

 

Kwa mujibu wa Aksa, baba yake na mama yake walilazimika kuhama kutoka Iringa hadi Singida kutokana na imani za uchawi wakitafuta dawa kwa ajili ya kumnusuru binti yao huyo ambaye mbali na kuwa na jila na Nyamiti ambalo lilizoeleka kwa watu wengi, wao walipenda kumuita cheupe kutoka na sura yake.

 

Akiwa Singida afya ya Aksa ilianza kuwa njema, baba yake alitaka kurudi Iringa na familia yake jambo ambalo halikumfurahisha mama yake mzazi na akagoma katakata kurudi Iringa akihofia maisha ya mwanae.Wakajikuta wanapeana talaka kwa sababu hiyo.

 

Mbali na kuachana kwa wazazi hao, hakuna aliyebahatika kupata mtoto mwingine licha ya Luwaha kuoa mwingine na Mkaulugu kuolewa.

 Aolewa na Lazaro Chanzi

 Inakadiriwa kuwa mwaka 1917 alipata mchumba ambaye ndiye alikuja kuwa baba wa watoto wake 6 na wakati huo wakiwa Mpwapwa eneo la Vinghawe namba 30 mahali lilipo chimbuko lao hadi leo na ambapo ni umbali wa zaidi ya kilomita 3 kutoka anapoishi kwa sasa.

Lazaro alikuwa ni Tarishi (mfanyakazi) Bomani katika kipindi cha utawala wa kikoloni na hivyo wakati fulani walilazimika kuhama kutoka Mpwapwa hadi eneo la Msanga kilomita nne kutoka Chamwino Ikulu ambako kulikuwa na boma pia.

Huyu ndiye Aksa ambaye mwaka 1918 alipata mtoto wa kwanza ambaye baadae alifariki. Miaka miwili baadae alipata mtoto mwingine ambaye ilikuwa sawa na yule wa kwanza naye hakuishi kabla ya mwaka 1922 kupata mtoto Andrew Lazaro Chanzi (Chalo karudi) aliyeweka rekodi na historia tukuka nchini Tanzania.

 Simulizi ya watoto wake

 Agnes Madelemu (72) ni mtoto wa mwisho wa Aksa kati ya familia ya watoto wake na ambaye anaishi naye kwa sasa, anasema kuwa katika kipindi cha ujana wa mama yao huyo, alipenda sana kusisitiza suala la amani lakini alikuwa ni mkorofi kama angechokozwa. 

Mtoto huyo wa Aksa anasimulia kuwa ukorofi wa mama yao ulitokana na kupinga uchafu na katu hakupenda mtu mwingine kuonewa mbele yake.

 Anachopenda kula

Licha ya umri huo, bibi huyo anapenda ugali wa mboga ya mlenda na nyama ya kupikwa.Anapenda pia kuoga mara kwa mara licha ya kuwa hana nguvu kwa sasa za kuoga hivyo huogeshwa na wajuu zake.

Asichopenda

Hapendezwi na dawa za kitabibu kwani anaamini kuwa si salama pamoja na kuwa ameishi Jijini Dar es Salaam kwa muda mrefu bado anaona kuwa dawa hizo ni sumu katika maisha ya mwanadamu.

Watoto na wajukuu

 Amezaa mara 8 lakini watoto aliobahatika kuishi nao ni sita ambao ni Andrew (Marehemu), Veronika, Amoni, Bertha na Agnes. Ana wajukuu 38, Vitukuu 102 na Vilembwe 38.

 Mchango kwa Taifa

Mchango wa kikongwe huyo kwa Taifa ni mkubwa, kwani mtoto wake Andrew Chanzi alikuwa ni mpiga picha mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii tangu wakati wa ukoloni na alitumwa maeneo yote ya Tanganyika akikusanya picha za matukio mbalimbali huku yeye akitumia nafasi hiyi kuwahamasisha Watanganyika kujiunga katika kudai Uhuru.

 Ni Chanzi aliyejulikana kwa jila la (Chalo Karudi) ambaye alicheza filamu ya Mhogo Mchungu iliyomuhusisha aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa rais Marehemu Rashid Kawawa.

 Mwingine katika uzao wake mjukuu wake Anderson Chanzi aliyezaliwa mwaka 1945 ambaye alikuwa ni miongoni mwa askari waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania ukombozi katika uvamizi wa majeshi ya Idd Amin wa Uganda.

 Wengi wa wajuu zake wana mchango mkubwa ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao baadhi yao sasa wanastaafu baada ya kuitumikia nchi kwa kipindi kirefu.

 Vitu viwili familia yake inajivunia kuwa haitamsahau, navyo ni upendo pamoja na usafi ambao hadi leo anaonyesha mfano wake.