Ageuka baba na mama wa wadogo zake sita

Mnanka Gofrey Chacha (17) akiwa na wadogo zake .Picha na Anthony Mayunga

Muktasari:

  • Ni kauli ya kinyonge ya Mnanka Godfrey Marwa (17) mkazi wa mtaa wa Chamoto mamlaka ya mji mdogo wa Mugumu wilayani Serengeti ambaye amelazimika kubeba majukumu ya kuwalea wadogo zake baada ya kifo cha mama yao wakati anajifungua.
  • Huku akilengwa lengwa na machozi anasema pamoja na kupenda kusoma lakini anashindwa kutokana na majukumu aliyonayo’ “Tumezaliwa watoto kumi, wa kiume wanane na wa kike wawili, hatumjui baba, tuliishi na mama yetu ambaye Oktoba 2016 alifariki wakati alipokuwa akijifungua mtoto wake wa kumi na akaacha kichanga hicho. Ndipo nikalazimika kubeba majukumu yote,” anasema.

Serengeti. “Nimefaulu kujiunga kidato cha kwanza Kambarage Sekondari, nawaza nikienda shule wadogo zangu sita wanaonitegemea watakula nini? Mimi ndiyo baba na mama yao, nalazimika kufanya vibarua ili wapate chakula.”

Ni kauli ya kinyonge ya Mnanka Godfrey Marwa (17) mkazi wa mtaa wa Chamoto mamlaka ya mji mdogo wa Mugumu wilayani Serengeti ambaye amelazimika kubeba majukumu ya kuwalea wadogo zake baada ya kifo cha mama yao wakati anajifungua.

Huku akilengwa lengwa na machozi anasema pamoja na kupenda kusoma lakini anashindwa kutokana na majukumu aliyonayo’ “Tumezaliwa watoto kumi, wa kiume wanane na wa kike wawili, hatumjui baba, tuliishi na mama yetu ambaye Oktoba 2016 alifariki wakati alipokuwa akijifungua mtoto wake wa kumi na akaacha kichanga hicho. Ndipo nikalazimika kubeba majukumu yote,” anasema.

Huku akisita kutokana na kububujikwa na machozi Mnanka anasema pamoja na kwa mama yao alipokuwa hai maisha yao yalikuwa magumu, lakini uwepo wake ulimwezesha yeye kwenda shule, lakini baada ya kufariki majukumu ya kutafuta mahitaji yote yako mikononi mwake, hakuna ndugu wanajitokeza kusaidia zaidi ya majirani.

Kifo cha mama yake

Anasema siku hiyo usiku mama yao Mariam Marwa maarufu kwa jina la Chacha alishikwa na uchungu uliomsumbua sana, “nyumba tunayoishi ni chumba kimoja na sebule, alihangaika mpaka akajifungua lakini akaendelea kupiga kelele kutokana na maumivu, kondo la nyuma halikutoka, tukaita majirani kuja wakakuta mtoto yuko chini, mama naye hajiwezi alikuwa anatokwa na damu nyingi,” anasimulia Mnanka huku akifuta machozi.

Majirani walijitahidi kumsaidia, lakini wakakosa usafiri wa kumpeleka hospitali kwa kuwa hawakuwa na fedha. Mnanka anasema walifanikiwa kupata msaada saa 9 usiku na kumpeleka hospitali Teule ya Nyerere Wilaya ya Serengeti, kabla ya kupata matibabu mama yao alikata roho.

Nyangi Daniel (36) jirani yao anasema kwa kuwa kondo la nyuma halikutoka ndiyo sababu yule mama akawa anatokwa na damu nyingi, na hiyo ndiyo sababu ya kifo chake. Chacha alijifungua nyumbani kwake bila msaada wa mtu mzima anayejua masuala ya uzazi. Baada ya watoto kuona hali imekuwa mbaya walipiga kelele, kwa kweli tulimfikisha hospitali akiwa hoi na haikuchukua muda akaaga dunia,” anasema.

Anasema kichanga kilichukuliwa na binti mkubwa wa marehemu ambaye ameolewa katika kijiji cha Mbirikiri kwa ajili ya matunzo, kwa kuwa hapo nyumbani watoto hawakuwa na namna yoyote, ingawa ndugu waliambiwa kusaidia hilo wote wakakataa.

Wakataa kuwa wachunga mifugo

Mnanka anasema ndugu wa mama yake walifika kwenye msiba akiwemo mjomba wao anayeishi Mwanza: “Walijitokeza wengine na kutaka kuchukua mwili wa mama wakazike kijijini, kwa kweli nililazimika kukataa maana hakuna aliyewahi kujitokeza na kutusaidia au kusema yeye ndiye baba, lakini wakadai watuchukue sisi lengo lao likiwa ni kutugeuza wachunga mifugo yao,” anabainisha.

Maisha yao

Mnanka anasema kuna wakati wanashinda na kulala bila kula kwa kuwa inategemea kama amepata fedha za kununua mahitaji: “Nimeanza kazi ya vibarua toka nasoma na mama yu hai ili kumsaidia maana naye alikuwa ni mlezi kupindukia, naendelea na kazi hiyo ili tupate mahitaji ya kila siku,” anasema.

Anasema kazi kubwa anayofanya ni kuingiza nyimbo kwenye simu kupitia komputa ya mtu ambaye hutakiwa kumlipa Sh4,000 kwa siku, hata hivyo anasema kuna wakati anapata Sh5,000 hadi Sh6,000 na kuna wakati hafikishi kiwango na kulimbikiza deni kwa ajili ya tajiri yake.

“Ukipata zaidi unapunguza deni, ukikosa mnashinda njaa maana hakuna jinsi, tunapokosa kabisa huwa tunachemsha uji kwa ajili ya watoto wadogo zaidi, mdogo wangu Godfrey Mnanka (14) aliacha shule akiwa darasa la kwanza kwa saa ndiye anabaki nyumbani kwa ajili ya kuwapikia chakula watoto,” anasema.

Alivyosoma

Anasema kutokana na ugumu wa maisha katika familia yao aliamua kuanza darasa la nne akiwa na umri wa miaka 13 akiwa hajui kusoma wala kuandika. Katika mtihani wa kwanza alishika nafasi ya 98 lakini kuanzia darasa la tano alikuwa kwenye kumi bora.

“Kwa mwezi nilikuwa nasoma wiki tatu, moja ni kwa ajili ya kufanya vibarua vya kusaidia familia, maana maisha yetu yalikuwa magumu toka awali, nimesoma hivyo hadi darasa saba nilipoomba kuishi kwa mwalimu ili niweze kujisomea na nilifaulu vizuri mitihani ya darasa la saba,” anasema.

Mnanka anasema ndoto yake ilikuwa ni kusoma ilia je awe mwanasheria kwa kuwa anapenda kazi ya kusaidia wengine lakini ndoto hiyo inazidi kufifia kutokana na majukumu mazito aliyoachiwa ya kulea wadogo zake kwa kuwatafutia chakula na mahitaji mengine.

Mnanka anasema wadogo zake wawili wanasoma darasa la kwanza Kambarage Shule ya Msingi na Mapinduzi B, watatu wenye umri wa kwenda shule hawajaanza na mmoja aliachia darasa la kwanza huku mdogo anayefuatiwa na kichanga kilichoachwa na mama yake ana umri wa miaka mitatu.

Anasema kaka yao mkubwa alikimbia familia kabla mama yao hajafa na dada yao ameolewa naye hana uwezo wa kuwasaidia wao.

Ombi lake

Anasema ombi lake kwa watakaoguswa ni kupata msaada wa kusoma yeye na wadogo zake, mahitaji ya chakula na makazi kwa kuwa hayo ndiyo mahitaji yao makubwa yanayowasumbua.

Wanatakiwa kupisha nyumba

Wakati hawajapata ufumbuzi wa matatizo ya maisha na elimu, wanatakiwa kupisha nyumba wanayoishi ili mwenye nyumba aweze kuibomoa kwa lengo la kujenga nyumba nzuri.

“Tumeishaambia kufikia mwezi wa tatu tunatakiwa tuwe tumeondoka hapa nyumbani, sasa sijui tutaenda wapi, tumeishi humu kwa msaada wa wasamaria wema maana awali tulikuwa tukilala kwenye majumba yaliyobomoka …,” anasema Mnanka.

Mwalimu mstaafu Paulo Mniko anasema yeye baada ya kuikuta familia hiyo ndani ya nyumba hiyo iliyokuwa katika hatua ya kubomoka aliamua kuikarabati: “Nilishikwa na huruma baada ya kumkuta huyo mama na wanawe wakiwa wanaishi kwenye jumba lililokuwa wazi na liko katika hatua ya kuanguka, niliamua kuikarabati bila kumfahamu mmiliki wake,”anasema.

Anasema baada ya ukarabati huo ndipo akamsaka mwenye nyumba na ambaye tayari ameagiza wahame ili aibomoe na kujenga nyumba nzuri. “Mama yao alikuwa anakunywa pombe sana, nilimshawishi mpaka akaanza kuingia kanisani, hata hivyo alikataa ghafla baada ya kundi lake kumbana,”anabainisha.

Mwalimu anasema Kanisa la Sayuni walikuwa tayari kumsaidia Mnanka aanze masomo, hata hivyo wameshindwa baada ya kuwauliza wadogo zake watasaidiwaje kwa masuala ya chakula wakati Mnanka akienda shule?

“Wakati wa msiba ndugu walikuja, nilikaa nao na kuwaomba wagawane hawa watoto hakuna aliyekubali, babu yao mzaa mama yao alikuwa amefungwa miaka 30 katoka hivi karibuni, sasa hivi anafanya vibarua kwenye miji ya watu kuchunga mifugo, hana msaada kwa wajukuu zake,” anasema.

Mwenyekiti wa kitongoji

Mwenyekiti wa kitongoji cha Chamoto Joseph Magoiga anakiri mama ya watoto hao hakuwa kwenye mpango wa kaya maskini zinazosaidiwa na Tasaf kwa kuwa makazi yake yalikuwa hayajulikani na kuwa wameweka utaratibu kupitia kamati ya maafa ya kitongoji ili kuwasaidia.

Mtoa huduma ya afya

Anthony Julius mhudumu wa afya ya msingi Chamoto ambaye amekuwa mstari wa mbele kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya watoto hao anaomba halmashauri ya wilaya kuwa na mipango ya kusaidia makundi kama hayo.

“Kunatakiwa kuwa na bajeti ya kusaidia makundi kama haya ili kujenga ustawi wa jamii, kama Benki ya Dunia kupitia Tasaf imetoa ufadhili kwa kaya maskini, lazima na wilaya ziwe na mafungu maalumu ili kuepuka mfumo wa kuwapitishia barua za kugeuka ombaomba, tuwe na mfumo maalumu,” anasema.

Wajibu wa serikali za mitaa

Kwa mjibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 inabainisha wazi kuwa serikali ya mtaa inapaswa kuhakikisha watoto walio katika uhitaji au yatima wanapata mahali pa kuishi na kuendelea na shughuli zao, kuhakikisha kuwa ustawi wao unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwatafutia shule.

Hata hivyo Afisa Ustawi wa Jamii wilaya Faustine Matesi anasema kutokana na ufinyu wa bajeti wanashindwa namna ya kusaidia, hivyo wanashirikisha jamii ili iweze kuwasaidia kwa huduma mbalimbali ikiwemo masuala ya elimu.

Mama yao aliolewa Nyumba Ntobu

Kwa mjibu wa watu mbalimbali wanaomfahamu marehemu mama yake Mnanka wanadai kuwa alipokuwa mdogo aliolewa na mwanamke (Nyumba Ntobu). “Aliolewa na mwanamke ambaye hakuzaa ili watoto wanaozaliwa wawe wa familia yake, ndiyo maana watoto wote wanajiitia jina la Chacha “anasema jirani yao.

Anasema pamoja na kuwa alikuwa akizaa na wanaume tofauti lakini watoto wote wanajiitia jina la Chacha, ndiyo maana wakati mama yao alipofariki walijitokeza watu wakadai kuwa hao watoto ni wa ukoo wao, hali iliyowastua watoto kwa kuwa hawakuwahi kuwaona wala kuwafahamu.

Kwa watakaoguswa na matatizo ya watoto hawa wawasiliane kwa kutmia no. 0787239480, 0767891849 au 0713290944.