Ulemavu na siri kubwa iliyojificha kwa Wamasai-1

Wanawake wa Kimasai wakiuza bidhaa kwa abiria wa basi la Loliondo Coach eneo la Engaruka
hivi karibuni. Picha na Florence Majani.

Muktasari:

  • Ni simulizi ya kusisimua inayokujia baada ya mwandishi kupiga kambi umasaini, inahusu mila na desturi, mtazamo kuhusu walemavu, uchumba na ndoa, uzazi hata kupeana watoto. Endelea…

Mwanamke yeyote akiwa mjamzito mawazo yake huwa ni siku ya kujifungua. Hiyo inatokana na sababu kwamba kujifungua ni mchakato mgumu unaohusisha uchungu na maumivu makali.

Siku ya kujifungua mwanamke hupigania uhai wake na wa mtoto. Hata hivyo, uchungu wote huo hupotea na kusahaulika pale anapompokea mtoto na kumpakata. Mtoto akizaliwa huongeza furaha, utulivu na upendo katika ndoa. Mtoto huleta faraja ya aina yake katika familia, ukoo na thamani ya mwanamke huongezeka.

Iko hivyo kwa makabila yote. Lakini kwa mwanamke wa jamii ya Kimasai, furaha ya kupakata mtoto, kumlea na kumwona akikua kuwa mtu mzima, inaweza isidumu iwapo mtoto aliyezaliwa ni mwenye ulemavu.

Hapo ndipo ilipo siri nzito iliyofungamana na mila za kabila hilo. Wazee wachache huweza kufunguka, wengi hubaki kutunza siri.

Jiulize; Je, umewahi kuwaona watu wenye ulemavu katika jamii ya wafugaji hasa Wamasai?

Kama jibu ni hapana; Unadhani katika jamii ya wafugaji hawazaliwi wenye ulemavu?

Au, unadhani wanatumia dawa gani ili wasizae watoto wenye ulemavu?

Baada ya kutafakari kwa kina, Mwandishi wa makala haya aliamua kufanya utafiti. Desemba 2015 alikwenda Arusha, huko alifunga safari ya saa 11 kutoka Arusha Mjini hadi Loliondo Wilaya ya Ngorongoro, kukutana na wazee wa mila katika vijiji wanakoishi wafugaji.

Alipiga kambi katika Tarafa ya Wasso, ambako alifanya mahojiano na watu mbalimbali vijiji vya Lorien, Lopolum, Samunge, Kata ya Engaruka na Wasso. Alitembelea wakunga wa jadi, wazee, viongozi wa kimila (Laiguanan) na waganga wa jadi (Laibon) wa kabila hilo.

Alikaa Wasso kwa siku nne akijifunza mila na desturi za Wamasai; Siku mbili katika nyumba ya mkunga wa jadi; Siku zilizosalia kwenye boma nyingine za Wamasai. Alitembelea Samunge na Engaruka. Alijiandaa vizuri. Alipata mkalimani mwenye maadili ya Kimasai na anayejua historia, siri, mila na desturi za kabila hilo.

Safari yake ilimfikisha kwa mwenyeji wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lopolum, Kata ya Lorien, Tarafa ya Loliondo, Silanga Kututu. Pia, alifanikiwa kukutana na wakazi wengine wa vijiji vya tarafa hiyo.

Baadhi ya maswali kwa kila aliyezungumza naye yalikuwa: Je, kijijini hapa kuna mlemavu? Kama yupo, ulemavu wake ni wa namna gani? Anaishije au anasaidiwaje? Kama hayupo, umewahi kumwona mlemavu katika jamii ya wafugaji? Naweza kupata fursa ya kumwona?

Wenyeji walikuwa waangalifu katika kujibu maswali hayo kwani yalikuwa yakigusa siri na mila. Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2002 na mwaka 2012, haionyeshi idadi ya walemavu nchini. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa, asilimia 10 ya watu katika kundi lolote la kijamii ni wenye ulemavu mbalimbali.

Ormaima na Orkirkoi

Kuhusu “Ormaima” yaani mtoto mwenye ulemavu, Kututu, mwenye wake watatu na watoto 18 anacheka kwanza, kisha anasema: “Kwa umri wangu huu wa miaka 48, nimewahi kuona walemavu wawili tu; Mmoja ni mzee mwenye ulemavu wa ngozi na mwingine ni mtoto, naye ana ulemavu wa ngozi.”

Kututu anasema kwa mila za Kimasai, mwanamke akijifungua Ormaima ni dalili ya mkosi au laana. “Lazima itaonekana kuwa kuna jambo baya huyo mwanamke alifanya, kwa hiyo analaaniwa na mizimu, labda ni laana au kuna mkosi kwenye ukoo huo,” anasema.

Wazee wa kimila wanaelezea sababu za kuwatelekeza porini walemavu, au kuwaua kwamba ilitokana na hadithi moja ya kabila hilo.

“Inaelezwa kuwa, hapo zamani ilikuwapo familia moja iliyokuwa na watoto watatu wa kiume; Wawili walikuwa wazima na mmoja alikuwa mlemavu. Wale watoto wawili wasiokuwa na ulemavu walifariki dunia, lakini yule mlemavu akanywa damu ya wenzake  hapo ndipo laana ilipoanza,” anasimulia.

Kututu anasema kuanzia wakati huo, yeyote aliyezaa mlemavu alihusishwa na laana hiyo na kuonekana alifanya jambo baya katika jamii. Hivyo, ili kuipoteza laana na kuondoa mkosi huo, mtoto akibainika kuwa mlemavu, alikuwa akiuawa kwa kunyongwa, au kutupwa porini ajifie au aliwe na wanyama.

Mwanamke akijifungua Ormaima familia hufanya mikakati kumkabidhi kwa “Orkirkoi” yaani mtu anayetumika kunyonga Ormaima au kuwatelekeza porini. Orkirkoi hufanya kazi hiyo kwa ujira wa ng’ombe. Analipwa na ndugu wa mtoto mlemavu anayenyongwa au kutelekezwa afie porini na hukubaliana kuitunza siri hiyo mpaka kufa.

“Sababu nyingine ya kuwaua Ormaima ni kutokana na mfumo wetu wa maisha wa kuhamahama. Ukiwa na mtu mlemavu ni shida, anaweza kuliwa na wanyama, hataweza kutembea wakati wa kuhama au wakati wa vita,” anasema Kututu.

Hata hivyo, Kututu anasema mila hizo zimeachwa hivi karibuni baada ya elimu kuingia katika jamii hizo.

Laibon (mganga wa kienyeji) wa Kijiji cha Lopolum, Mkenga Kitupey anasema Wamasai waliamua kuwaua Ormaima kwa sababu hapakuwa na namna ya kuwasaidia. “Wakiona mtoto anakua anafikia umri wa kutembea, hatembei na hana dalili ya kubadilika au hana dalili ya kupona, wanaona ni bora auawe au atelekezwe porini,” anasema.

Hata hivyo, Kitupey anasema hivi sasa Wamasai wameelimika, wanaona bora wawalee Ormaima hata kama kuwa nao ni mkosi, au atakuwa mzigo kwa familia. Hofu haikuwa kwa Ormaima tu, hata mwanamke aliyekuwa anazaa pacha kwa sababu ni matukio yaliyokuwa yakitokea kwa nadra na kiimani Wamasai walikuwa wanadhani si jambo la kawaida.

Mkazi wa Wasso, Joseph Kitupey anasema mila hizo zilikuwapo lakini anasisitiza kuwa hivi sasa ni wachache wanaoziendeleza na kama wanazifanya basi ni kwa siri kubwa.  “Siku hizi hawafanyi hizo mila, kama wanafanya basi viongozi tutakuwa hatujui,” anasema Kitupey.

Anasisitiza kwamba Wamasai wameelimika na wanajifunza mambo mengi, ikiwamo kuachana na mila potofu zisizo na manufaa.

Mwanamke wa Kimaasai, Napiskiory Olosini (32)  mwenye watoto saba, mkazi wa Engaruka anasema wakunga wa jadi wana siri kubwa kwani nao hushirikishwa katika kuwaua Ormaima.

“Kama mtoto ana ulemavu ambao unaonekana mapema, ile siku anayozaliwa, mkunga humkabidhi kwa Orkirkoi na mama mzazi huambiwa mtoto alifariki kwa bahati mbaya,” anasema.

Mkunga wa jadi, Noorkidemi Kitupey (60) anakataa. Anasema ajuavyo yeye huwa hawashirikishwi katika kutekeleza mila hizo, bali hujaribu kwa hali na mali kuwasaidia watoto wanaozaliwa wakiwa na ulemavu.

“Kama mwanamke amezaa mtoto amepinda miguu, sisi tulimnyoosha kwa kutumia mafuta ya ng’ombe na ilimsaidia sana mtoto,” anasema.

Noorkidemi anasema kumnyoosha mtoto viungo huanza tangu siku ya kwanza anapozaliwa, lakini kama ataonyesha dalili za wazi za viungo kujikunja kadri anavyokua, mkunga humnyoosha kwa kutumia mafuta.

Hata hivyo, Marea Akilel (80) anasema hajawahi kuona Ormaima kwenye jamii yake. “Ni nadra kuona Ormaima umasaini. Siri wanayo wazee wa kimila,” anasema.

Akilel anasema wanawake walifichwa kuhusu wanakopelekwa Ormaima, lakini walishangaa wanatoweka. “Hata watoto weupe (albino) walitoweka. Tulikuwa tunashangaa tu mtoto hayupo na tulikuwa tunaambiwa wanachukuliwa na mizimu,” anasema.

Kuingia kwa shule na dini kumewabadili. Wengi waliohojiwa katika maeneo ya Wasso, Loliondo na Engaruka wanasema ni dhambi kuwaua walemavu, ni bora kuwatelekeza porini au kuwanyima chakula.

“Sisi ni watu wa kuhamahama kutafuta malisho, kama hakuna punda wa kumbeba wakati wa kuhama basi tunamwacha ndani,” anasema Akilel. Kitendo cha kumuua Ormaima kilifanyika kwa siri kubwa baina ya wazee wa kimila, baba wa mtoto na Laibon.

Kama mtoto atabainika ni ormaima tangu akiwa mchanga, iliaminika kuwa ni laana lakini kama mtu atapata ulemavu ukubwani iliaminika karogwa. Dini zimechangia pia kuwapa watu elimu juu ya upendo na kuondoa mila potofu.

Utafiti wa Dk Sheryl

Maelezo kama hayo yamo katika ripoti ya utafiti uliofanywa mwaka 2009 na mtafiti wa masuala ya kijamii kutoka Chuo Kikuu cha Augustana, Marekani, Dk Sheryl Feinstein kuhusu maisha ya walemavu kwa Kabila la Wamasai. Utafiti huo ulioitwa “Utafiti Kuhusu Maisha ya Wenye Ulemavu Katika Kabila la Masai Tanzania,” ulilenga kuwaangalia watu wenye ulemavu wanavyoishi kata za Simanjiro, Makuyuni na Manyara, wilayani Monduli.

Dk Sheryl alitumia sampuli ya watu 68 wenye ulemavu na wasio na ulemavu. Katika utafiti huo, anasema walemavu walikuwa wakitengwa na hawakuwa wakishirikishwa kwenye shughuli za kimila, hawakwenda shule wala kupewa huduma za afya.

Baada ya kufanya mahojiano na walemavu, ndugu zao na viongozi wa kimila katika kata hizo, Dk Sheryl alibaini mambo matatu.

Kwanza ni imani kuwa ulemavu unasababishwa na matukio ya kimiujiza. Pili, hawakuwa na taarifa sahihi kuhusu chanzo cha ulemavu hali iliyochangia walemavu kunyanyapaliwa.

Tatu, sababu nyingine iliyohusishwa na ulemavu katika kabila hilo kuwa ni laana na uchawi.

Laana ilihusishwa na tabia mbaya iliyodaiwa kufanywa na mama au baba hapo zamani. Dk Sheryl alibaini kuwa walikuwa wakiamini, ulemavu uliojitokeza ukubwani ulisababishwa na uchawi. Alitoa mfano wa mtu mmoja aliyepooza akidai kuwa alirogwa.

Ripoti ya utafiti huo inaonyesha kwamba baadhi ya watu waliohojiwa walidai bado walikuwa wanaamini kwamba wenye ulemavu walikuwa wanaendelea kuuawa, lakini wengi walikana.

Hata hivyo, wote walikiri kuwa zamani lilikuwa jambo la kawaida na mwingine alisema: “Miaka 15 iliyopita imeleta mabadiliko makubwa.”

Mtu mmoja alisema kwamba anaamini wenye ulemavu wanaendelea kuuawa, lakini kwa siri sana. Wengine walisema kuua wenye ulemavu ni dhambi, ila waliona ilikuwa bora kuwatelekeza au kuwaacha bila kuwapa chakula. Mtoto mmoja katika Kituo cha Watoto Loliondo alitoa ushuhuda huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Dk Sheryl, mtoto mmoja wa kiume mwenye ulemavu wa macho alikutwa ametelekezwa  Bonde la Ngorongoro.  Aliachwa afe peke yake kwani alishindwa kuondoka kwa hofu ya wanyama wakali. Pia, binti mwingine mdogo alikutwa katika Kijiji cha Lopolum akiwa ametelekezwa, huku akiwa amewekewa kibuyu cha maji na chakula kidogo.

Maisha ya kuhamahama yametajwa katika utafiti huo kuwa, kikwazo kwa wenye ulemavu. Mama mmoja alisema: “Hawawezi kutembea nao, wanahitaji punda usafiri ambao mara nyingine si salama.” Mwanamke mwingine alisema: “Tulikuwa tunawaficha kwenye nyumba na kuwaacha tunapohama.”

Kadri ustaarabu unavyoingia na kuthamini haki za binadamu katika jamii ya Wamasai, suala la ‘kuua’ au ‘kutelekeza’ wenye ulemavu linaendelea kuzua mjadala; Baadhi wakikiri mila hiyo kuwapo na wengine wakikana.

Utafiti wa Mollel

Matokeo ya utafiti mwingine uliofanywa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) anayewakilisha wenye ulemavu, Amina Mollel yanaonyesha kuwa kihistoria maisha ya wenye ulemavu yalikuwa hatarini katika jamii ya wafugaji.

Mollel aliyewahi kuwa mtangazaji na mtayarishaji wa vipindi vya wanawake na watu wenye ulemavu katika Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), anasema alifanya utafiti huo kuhusu maisha ya wenye ulemavu kwa jamii ya Wamasai alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Tumaini.

“Niliifanya utafiti nilipokuwa nasoma mwaka wa tatu, Chuo Kikuu cha Tumaini mwaka 2008. Kama utafiti unavyojieleza ni kweli walikuwa wanawaua watoto wenye ulemavu na wakunga wa jadi walishiriki,” anaeleza kuhusu utafiti huo ulioitwa “Maisha ya Wenye Ulemavu Katika Jamii ya Wamasai”.

“Sasa hivi, hiyo jamii imeanza kubadilika, wanawapeleka shule na kesi za kuwaua zinapungua, kinachosababisha ni kuhamahama,” anasema.

Mollel anatoa ushauri kwa jamii kuwajali wenye ulemavu akisema ni watu sawa na watu wengine, hivyo hakuna sababu ya kuwanyanyapaa.

 “Kama mtu ana ulemavu wa mguu atashindwa kufanya kitu, lakini akijengewa uwezo anaweza kufanya kila kitu na hatakuwa tegemezi.

Walemavu wajengewe uwezo, wapelekwe shule. Wajiajiri, wapewe mitaji, wakitelekezwa wanakuwa tegemezi na hapo wanaonekana mzigo,” anasema mbunge huyo ambaye pia ni mlemavu wa mguu, lakini aliyejengewa uwezo na kuwa mwandishi wa habari mahiri na sasa mbunge.

Maoni ya viongozi

Mkuu wa Wilaya ya Loliondo, Hashim Mgandilwa anasema kihistoria anafahamu kwamba walemavu walikuwa wanauawa au kutelekezwa porini, lakini miaka ya hivi karibuni hajasikia habari zinazofanana na hiyo.

“Kadri siku zinavyokwenda tunaendelea kutoa elimu, taratibu wanapata ufahamu kuhusu mila ambazo hazina manufaa au mila katili. Ingawa sijawahi kuletewa kesi hapa kwangu ya mlemavu kuuawa au kutelekezwa, lakini ninasikia kuwa mila hizo zilikuwapo,” anasema. Anasema Serikali inachukuwa hatua muhimu kuwalinda watoto wenye ulemavu ikiwamo kuhakikisha wanakwenda shule na wanaohitaji matibabu au kulelewa kwenye vituo maalumu wanapelekwa.

Mgandilwa anaeleza zaidi kuwa, bado kuna mila za ukeketaji ambazo imekuwa vigumu kuzimaliza kwa kuwa zinafanyika kwa siri kubwa zikiwashirikisha wenyeviti wa vijiji na wazee wa kimila.

Mgandilwa anaeleza jinsi Wamasai wanavyotunza mila zao na kutoa mfano wa wakunga wa jadi kwamba, ndiyo wanaowarubuni wanawake wasiende hospitali ili waendelee kunufaika na ujira wa mbuzi au malipo ya Sh500 pindi wanampozalisha mjamzito.

“Juzi (Desemba wakati wa mahojiano) nilifanya mkutano na watu wa kata zangu tano. Nikawaambia kama wanataka, wajawazito wanaweza kwenda hospitali na wakunga wao wa jadi, lakini pia wanatakiwa kujifungua hospitali na wakawapa hao wakunga zawadi ya mbuzi. Suala hapa ni kujifungua salama,” anasema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, John Mgalula anasema kipindi cha mwaka mmoja alichokaa wilayani humo hajawahi kupata kesi ya mlemavu kuuawa, lakini zipo chache za kunyanyapaliwa.

Mgagula anasema anajua kuwa awali miaka mitano au sita walifanya hivyo. “Lakini walemavu tulionao sasa wanapelekwa shule na wanapewa huduma zote,” anasema.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Pentekoste, William Mwamalanga anasema alipotembelea umasaini aligundua kwamba mila za Wamasai zinamkataa mtoto yeyote mwenye ulemavu na hilo linafanywa siri kubwa.

 “Mila zao haziwaruhusu kutoa siri hiyo hasa mwanamke ni mwiko kufanya hivyo. Mimi nilikutana na wanawake 21 wa Kimasai maeneo tofauti, wakaniambia baba watoto wetu wanauawa,” anasema huku akidai waliommegea siri hiyo walimwapiza asiseme, kwani wanaweza kufukuzwa au kutengwa na jamii.

“Mbaya zaidi dhambi ya ulemavu anatupiwa mwanamke, anaonekana yeye ndiye mwenye mkosi. Viongozi wa kidini tunatakiwa kulikemea suala hili hasa la kuwakataa walemavu na kuwadunisha wanawake,” anaeleza.

Taarifa za mwaka 2010 kutoka Kituo cha Uangalizi Ngorongoro zinaonyesha kwamba, kuna walemavu 14  katika maeneo ya Kata ya Makuyuni, Manyara, Simanjiro na Tarafa ya Loliondo.

Tanzania haina takwimu za watu wenye ulemavu katika sensa za Makazi na Watu waka 2002 na 2012.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Felician Mkude anasema shirikisho hilo limewahi kupokea taarifa za mauaji maeneo ya vijijini Umasaini, lakini hawana takwimu kamili na eneo ambalo mauaji hayo hufanyika.

“Haya mambo yanafanyika, lakini hatuna takwimu kamili, hata hivyo huwa tunafanya kazi yetu kwa kuwaambia viongozi wa maeneo husika kuhusu mambo yanayofanyika,” anasema na kuongeza kuwa,  taarifa zinazowafikia ni kuwa watu wa kabila hilo kipindi cha nyuma walikuwa wakiwatelekeza walemavu kutokana na sababu mbalimbali,  ikiwamo kuwaona kama mzigo kwa sababu ya mazingira yao ya kuhamahama.

“Kama ilivyo kwa walemavu wa ngozi, hali kadhalika kwa walemavu wengine yanafanyika mambo kama hayo, lakini zinakosekana takwimu kwa sababu labda wanafichwa na inafanyika kwa siri, tofauti na mauaji ya albino,” anasema.  Mkude anasema hata mila na tamaduni hizo baadhi zinaamini kuwa mlemavu ni mkosi kwenye jamii au adhabu kutoka kwa Mungu.

“Ndiyo maana tunataka kuendelea kutoa elimu kwa kina kuhusu imani hizo, tuwaelimishe wale wanaodhani kuwa walemavu ni mizigo au laana,” anasema.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana na Walemavu, Dk Abdallah Posi anasema si jamii ya wafugaji tu, yapo makabila mengi yanayoua au kuwaficha na kuwatelekeza watu wenye ulemavu.

“Hilo linafahamika, makabila mengi yanafanya hivyo, chanzo kikubwa ni kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu walemavu,” anasema.

Dk Posi anasema mambo mengi yanayotokea vijijini hayaripotiwi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kutokuwa na elimu au kukosa sehemu ya kusemea huku wengine wakiona ni sahihi kwani hiyo ni sehemu ya mila.

“Kama haya matukio yanatokea mjini, basi lazima hata vijijini yapo, wapo watu wanawaficha watoto na kuwatelekeza. Kwa mfano, lile tukio la mtoto kufichwa kwenye boksi au wanaoua albino,” anasema.

Dk Posi anasema ili kukomesha unyanyasaji kwa watu wenye ulemavu, lazima kuwe na ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za watu wenye ulemavu. “Tunataka kufikia mahali, mtu aseme anaogopa kumficha mlemavu si kwa sababu atafungwa, bali aseme simfichi mlemavu kwa sababu siyo sahihi kufanya hivyo,” anasema.

 Alisema wizara yake itahakikisha inatoa elimu kwa wananchi kwa muda wote, badala ya kufanya hivyo kwa kipindi kifupi na kukusanya takwimu sahihi za watu wenye ulemavu ambazo zinajumuisha idadi na mahitaji yao.

Itaendelea kesho…