Wakuu wasitumie sheria ya saa 48 kuhukumu

Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia wakuu wa wilaya ‘wakishindana’ kutumia ‘sheria ya saa 48’ kutoa adhabu kwa kuwaweka baadhi ya watu mahabusu.

Mamlaka haya wamepewa kupitia Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 na hutakiwa kutumia amri ya kumweka ndani – kwa muda usiozidi saa 48 – mtu au kundi la watu ambao kubaki kwao nje kunaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii.

Tofauti ni kwamba tangu baada ya uchaguzi mkuu, baadhi ya wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia sheria hiyo kutoa adhabu au hukumu, badala ya malengo yaliyowekwa ya kulinda usalama kwa watu wengine. Wengi waliokumbwa na adhabu hizo ni viongozi wa vyama vya upinzani.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 (1) inasema: “Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa  na  maoni yoyote na kutoa nje  mawazo  yake,  na  kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana  zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”

Mbali ya Katiba ya mwaka 1977 inayotoa uhuru wa watu kutoa maoni yao, Sheria ya Vyama vya Siasa imefafanua haki za vyama vya siasa na wajibu wao huku ikiweka mkazo kuzingatia Sheria ya Jeshi la Polisi. Sheria ya Jeshi la Polisi ndiyo inatumiwa na wakuu wa wilaya, ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi za wilaya, kuzuia mikutano ya wapinzani ya hadhara na sasa hata baadhi ya mikutano ya ndani.

Vyama vya upinzani nchini vilirejeshwa tena mwaka 1992 kwa lengo la kukuza zaidi demokrasia na kuruhusu mawazo mbadala.

Kwahiyo upinzani uliruhusiwa kisheria na wajibu wa vyama vya upinzani ni kukosoa sera za chama tawala na kufafanua zao, lakini lengo kubwa ni kuifanya serikali isilale badala yake ichape kazi muda wote jambo ambalo ni zuri kwa maendeleo ya nchi.

Ili kuhakikisha Sheria ya Vyama vya siasa (Sura ya 258) inatumika ipasavyo Oktoba 12, 2007 kwa tangazo Na.215 Serikali ilitangaza kanuni zilizoainisha haki za kila chama cha siasa na wajibu wake maana hakuna haki bila wajibu.

Katika sehemu ya pili inayohusu Haki za Chama, kifungu cha 4 kinasema (1) (e) kila chama cha siasa kitakuwa na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa. Hali imekuwa tofauti kwani inaelekea baadhi ya wakuu wa wilaya ama hawajaelewa au wanafanya kusudi kuitumia sheria hiyo kuwaweka ndani baadhi ya viongozi wa upinzani wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kisiasa.

Kinachoshangaza zaidi ni kuwa maagizo ambayo huyatoa huwa si kuwataka watuhumiwa wahojiwe na kuacha mamlaka hayo kwa polisi kuendelea na taratibu zao za kisheria, badala yake viongozi hao wa serikali wamekuwa wakitoa hukumu na kuwaadhibu ‘watuhumiwa’ kwa kuwaweka ndani kwa saa 48. Sisi tunaamini kuwa kabla ya kutoa hukumu au adhabu huwa kuna utaratibu maalumu na haki ya msingi ni kwa mtuhumiwa kusikilizwa kwanza.

Kama tukiacha wakuu wa wilaya, mikoa au viongozi wengine kutoa adhabu hakutakuwa na haki na ndio maana tunashauri jukumu hilo liachwe chini ya mahakama pekee