Dk Tulia anahitaji kujua umuhimu wa diplomasia

Wabunge wa upinzani wakiandamana kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma, mwezi uliopita kupinga namna Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alivyokuwa akiendesha vikao. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Nilifurahia uwezo wa kujieleza wa Dk Tulia ambaye kitaaluma ni mwanasheria kama nilivyofurahia aina ya maswali yaliyoulizwa na Mhando. Kwa kweli kwa kiasi fulani ilikuwa burudani ya aina yake.

Wiki iliyopita nilipata bahati ya kuangalia kipindi kiitwacho ‘Funguka’ kupitia runinga ya Azam na nikamshuhudia Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akihojiwa na mwanahabari Tido Mhando.

Nilifurahia uwezo wa kujieleza wa Dk Tulia ambaye kitaaluma ni mwanasheria kama nilivyofurahia aina ya maswali yaliyoulizwa na Mhando. Kwa kweli kwa kiasi fulani ilikuwa burudani ya aina yake.

Hata hivyo, katika kipindi hicho nilitegemea Dk Tulia angezungumzia zaidi kuhusu ni nini anachokiona ni tatizo kati yake na wabunge wa upinzani kilichosababisha wasusie vikao vya Bunge alivyoviongoza.

Kikubwa zaidi nilitarajia Naibu Spika ambaye kwa nafasi hiyo ni kiongozi wa wabunge wenzake kwa kuwa ni mbunge mteuliwa wa Rais, atupe mwanga nini kifanyike kuondoa taswira mbaya inayoonyesha Bunge la vyama vingi limegeuka la chama kimoja. Nilichokisikia kutoka katika kinywa cha kiongozi huyo wa mhimili muhimu kati ya mitatu ya nchi kilifanya nichoke kabisa na kukata tamaa. Nikajiuliza, hivi ukiitwa mwanasheria maana yake diplomasia haina nafasi kwako?

Nikafikia hitimisho kwamba kiongozi huyo angestahili kubakia katika nafasi yake ya kwanza ya Mwanasheria wa Serikali kuliko kuwa Naibu Spika wa Bunge kama hili tulilonalo.

Alipoulizwa swali na Mhando anaionaje kazi yake ya sasa akilinganisha na ile aliyokuwa nayo awali, alijibu “Mimi ni mwanasheri, kazi yangu ni kutafsiri sheria hivyo ninaifurahia kazi hii niliyonayo kama nilivyoifurahia kazi yangu ya kwanza”.

Dk Tulia akisema anaifurahia kazi yake hakuna atakayembishia kwa sababu kwake kazi aliyobobea nayo ni hiyo ya kutafsiri sheria na kweli anaitendea haki fani yake.

Miongoni mwa tabia za wanasheria ni kutoa majibu rahisi kwa maswali magumu ilimradi sheria imezingatiwa.

Hata hivyo, alipaswa kujua kuwa mbali na kutafsiri sheria, katika nafasi ya sasa tulitarajia ajue kuwa bungeni siyo mahakamani, bali ni mahali pa Serikali kushauriwa na wawakilishi wa wananchi, hivyo sambamba na kutafisri sheria diplomasia ingechukua nafasi yake.

 

Bunge halimfai Dk Tulia?

Bunge hili la vyama vingi limesheheni vijana ambao kitabia ni wadadisi, wabishi na hata wakorofi. Kama Dk Tulia angekuwa anaongoza Bunge la chama kimoja, kuegemea katika fani yake ya kutafsiri sheria ingekuwa mahali pake.

Hata katika Bunge la vyama vingi ili kuliendesha kwa ufanisi Spika na Naibu wake hawapaswi kushikilia kutafsiri sheria, bali kujua jinsi ya ‘kupiga makasia’ kutafuta mwafaka inapotokea mivutano.

Hili ndilo somo ambalo Naibu Spika Dk Tulia anapaswa kulisoma kutoka kwa ma-spika wa mabunge mengine yenye wabunge wa vyama vingi barani Afrika. Namshauri afanye ziara ya kikazi nje ya nchi.

Kwa bahati nzuri Dk Tulia ana mfano mzuri wa kuiga kutoka kwapika wa Bunge la Afrika Kusini, Baleka Mbete.

Kufuatia Mahakama ya Katiba nchini humo kutoa hukumu kwamba Rais Jacob Zuma alivunja Katiba ya nchi kwenye lile sakata la ukarabati wa nyumba, mwanamama huyo alifanya haraka kukutana na wabunge wa vyama vyote ili kuona Bunge lifanye nini.

Kikao kati ya Spika Mbete kutoka chama cha ANC kilihudhuriwa na mbunge na kiongozi wa Chama cha Democratic Alliance (DA), Mmusi Maimane ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Zuma.

Wengine waliohudhuria ni kiongozi wa wabunge wa ANC bungeni humo, Jackson Mthembu, Kenneth Meshoe wa chama cha African Christian Democratic Party (ACDP), Johnn Steenhussein wa DA, Floyd Shivambu wa Economic Freedom Fighters (EFF) na Nhlanhla Khubisa wa National Freedom Party (NFP).

Baada ya mkutano huo, Spika Mbete aliwaambia wanahabari kwamba maoni mbalimbali yaliyotolewa na wabunge wa vyama vya upinzani yatafikiriwa na kuzingatiwa.

Kilichonisikitisha kutokana na mahojiano yale ya Dk Tulia na Mhando ni kuona kwamba Naibu Spika anaona mtafaruku uliopo sasa katika Bunge kati yake na wabunge wa upinzani kwake siyo tatizo kubwa.

Hivi akifanya kama Spika Mbete wa Afrika ya Kusini, kukutana na viongozi wa wabunge wa vyama vya upinzani au hata na kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuzungumzia sakata lililopo atapunguza nini?

Hivi kati ya mawili haya kuendelea na hali iliyopo sasa huku wabunge wa upinzani wanasusia vikao vya Bunge na kukaa nao kupata ufumbuzi ili Bunge lirejee kuwa kitu kimoja ni lipi jambo la busara na hekima?

Natamani Mwenyezi Mungu ammiminie busara na hekima Dk Tulia na wabunge wa upinzani ili waangalie masilahi mapana ya wananchi na Taifa kupitia Bunge letu.

Inapendeza namna gani kusikia Naibu Spika akisema kama Spika Mbete mara baada ya kumaliza kikao chake na wabunge wa vyama vyote aliponukuliwa na vyombo vya habari akisema “…all parties had agreed that the image of the National Assembly had been eroded and that institutional reform was needed to restore it”.

Akimaanisha vyama vyote vimekubaliana kuwa taswira au heshima ya Bunge la Taifa imemomonyoka na kwamba mageuzi ya kikatiba yanahitajika ili kuirejesha.

 

Mageuzi ya kikatiba yanahitajika?

Kwa kinachotokea katika Bunge letu pengine kinahitajika hicho walichoshauri wabunge wa Afrika Kusini yaani kufanyika kwa mageuzi ya kikatiba ili kurejesha heshima.

Dk Tulia anaweza kulaumiwa kwa anakichofanya, lakini naye ni mwathirika wa mfumo wetu wa Bunge ulivyo, mfumo ambao bado ni kivuli cha siasa za chama kimoja.

Hilo linapaswa kufahamika vyema na hata wabunge wa upinzani wapime faida na hasara za kumsusia Dk Tulia katika mazingira ya Bunge yaliyopo. Kwa maoni yangu hasara ya kumsusia ni kubwa kuliko faida.Dawa ya hali inayoendelea bungeni kwa wabunge wa upinzani kutoonyesha uwezo wao wote ni matokeo ya Katiba ya nchi ilivyo, hivyo haitegemewi kuondoka hadi mabadiliko yafanyike.

Mchakato wa Katiba uliokwama inaelekea uko mbioni kufufuliwa ili uendelee na Katiba Pendekezwa ambayo wapinzani waliisusia.

 

Nasaha kwa Dk Tulia

Nasaha zangu kwa Dk Tulia ni hizi zifuatazo; unaweza kushikilia msimamo ulionao wa kutafsiri sheria ukawadhibiti wapinzani. Bila shaka utajizolea sifa kemkem kutoka kwa chama chako. Hata hivyo, ukumbuke kila mmoja wetu anaandika historia kupitia anachokifanya.

Nionavyo ungechukua msimamo kama ule wa Spika Mbete wa Afrika Kusini ungeandika historia iliyotukuka. Kaa na viongozi wa wabunge wa vyama vya upinzani kwa nafasi yako ya uongozi wa Bunge ulionao, ongea nao, wasikilize, wafanye wakuelewe na wewe uwaelewe ili kurejesha umoja wa wabunge wa Bunge lako.

Vinginevyo historia itakuandika tofauti na matarajio ya watu wengi kwa upinzani bungeni, yaani ‘terminator’ (mmalizaji) badala ya ‘pacifier’ yaani mrekebishaji wa mambo yanapoharibika. Fani ya sheria unayo, lakini pia tafuta na fani ya diplomasia.

Katika mahojiano kupitia kipindi kile cha Funguka pale Azam TV hukuonyesha kusononeshwa hata kidogo na kinachojiri katika Bunge letu. Hii siyo sifa ya mlezi.

Kwa wabunge, wewe uko mahali pa mzazi au mlezi. Ulipaswa uonyeshe huzuni ya mzazi kwani mzazi huonyesha kusononeshwa na ukorofi wa watoto wake pamoja na kutokukubaliana na ukorofi huo.

 

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana kwa baruapepe: [email protected]