Hofu ya wasanii, uhuru na nguvu yao-3

Msanii wa filamu, Gabo Zigamba

Muktasari:

Pamoja na matatizo hayo kuwa yameanza toka zamani katika mwonekano tofauti kuanza kusikika kwa malalamiko ya wasanii katika siku za karibuni kumetokana na kundi kubwa la vijana kuishi kwa kutegemea tasnia ya sanaa.

Kwa muda mrefu sasa toka tasnia za muziki wa kizazi kipya na filamu zianze kushika kasi nchini, vyombo vya habari vimekuwa vikipambwa na malalamiko ya wasanii ambayo ni wazi yameshakuwa sugu.

Pamoja na matatizo hayo kuwa yameanza toka zamani katika mwonekano tofauti kuanza kusikika kwa malalamiko ya wasanii katika siku za karibuni kumetokana na kundi kubwa la vijana kuishi kwa kutegemea tasnia ya sanaa.

Kwa kuwa dhana hii imejengeka kwa muda mrefu basi mlolongo wa wasanii wote wanaochipukia wanaona njia na mlango pekee wa kutoka na kutimiza ndoto zao za sanaa ni kwa mfanyabiashara au mdau fulani bila hata kufungua fikra.

Tumekuwa tukisajili na kutoa vibali kwa wadau wengi wa sanaa na wenye kuwekeza katika sekta hii. Tunaamini kwamba fursa ya wawekezaji itatumiwa na wasanii katika kutanua uhuru wao wa biashara ya sanaa na kufuta dhana ya utegemezi wa mdau au mfanyabiashara mmoja mmoja.

Wakati tukiamini kuna wadau wengi sokoni wanaofanya kazi kubwa katika kuwekeza kwenye sekta ya sanaa, lazima wasanii kama tulivyoeleza katika makala zilizopita waone thamani yao, kazi wanazozalisha na kwa maana hiyo wakatae utumwa.

Utumwa wa wasanii hasa katika utegemezi unaleta picha moja tu kwamba kuna mushkeli katika kazi wanazozalisha. Pengine hazina ubora unaostahili hivyo kutegemea huruma ya wafanyabiashara katika kutangazwa na kulazimisha soko, hivyo kujikuta mateka.

Ni lazima wasanii kwanza watambue kwamba wao ndiyo wenye sanaa na kwamba bila wao mdau au mfanyabishara yeyote anayewekeza kwenye sekta ya sanaa hawezi kuwapo.

Nguvu hii ya wasanii ni ya muhimu na inahitaji kwenda sambamba na kufuta dhana potofu kichwani mwao kwamba lazima wategemee na kupiga magoti ndipo kazi zao ziweze kupata nafasi.

Pili; lazima wasanii wafikirie namna ya kutanua mianya mingine ya mapato. Hili tumelisisitiza sana katika makala zetu za nyuma.

Tumeeleza hapo juu kwamba, furaha ya mfanyabiashara ni kumfanya msanii awe tegemezi milele kupitia kuteka fikra zake, kumkatia mirija ya mapato na hivyo kuwa na nguvu ya kuamua hatima ya kipato cha msanii. Msanii akishafikishwa hapo anakuwa hana sauti tena.

Kwa hiyo, lazima msanii anapokuwa anashiriki matukio yoyote ya sanaa na kubuni kazi zake awe na fikra moja kichwani ya kutanua vyanzo vingine vya mapato. Afikirie muda wote kuwekeza fedha yake katika maeneo mengine ya uzalishaji ili kuwa na uimara wa kipato.

Uimara wa uchumi utasaidia msanii kuwa na sauti na kuepuka kukatika kwa pato lake ambao ni mtego muhimu sana unaotumiwa na mfanyabiashara yeyote katika kuhakikisha anaamua vyovyote atakavyo dhidi ya msanii yeyote.

Historia inaonyesha kwamba baadhi ya wasanii wamekua wakiingia kwenye mtego wa umaarufu na matumizi ya anasa na kuishi maisha yasiyoendana na vipato vyao halisi. Hali hii siyo tu inawapa faida wafanyabiashara, pia inapukutisha fedha zote anazochuma na hivyo kumrejesha katika umaskini wa kipato na utegemezi.

Aidha, ukiacha kupukutisha pato la msanii hali hii inaweza kuwa chanzo cha wasanii kushawishika na kuingia katika mtego wa kufanya biashara haramu na kujiingiza kwenye dawa za kulevya maana kazi halisi za sanaa zinakuwa hazikidhi vipato.

Kwa maneno mengine maisha ya starehe na anasa anayoishi msanii leo yanamuweka kwenye mduara wa ufukara. Yaani anapata fedha leo, anazunguka kwenye klabu za usiku kuzitafuna na wapambe wake halafu kesho asubuhi analia njaa na kuanza kumlilia mfanyabiashara aliyemlipa fedha kiduchu kwenye maonyesho au manunuzi ya kazi zake.

Tunaamini kabisa kuna wasanii leo kutokana na uimara wa vipato vyao uliotokana na kuwekeza katika maeneo mengine ya uzalishaji wanaweza kusimama dhidi ya mdau au mfanyabiashara yeyote na kusema hapana.

Wanaweza kukataa malipo fulani yasiyokidhi hadhi na viwango walivyoviweka kama thamani ya kazi zao. Aidha, wako huru kuamua vyovyote watakavyo juu ya hatima ya kazi zao na hivyo hawaishi kabisa chini ya nira za wafanyabiashara.

Kutokana na thamani waliyojiwekea na mbinu za kibiashara wanazotumia wanaweza kuruka viunzi vyovyote vile vinavyopandikizwa au kupangwa na mdau au mfanyabiashara.

Hawa ukiacha utanuzi wa mianya ya mapato, wametambua thamani yao. Wameelewa kwamba mfanyabiashara au mdau yeyote anayewekeza katika sekta ya sanaa hawezi kupiga hatua bila kumtegemea msanii.

 

Kwa mawasiliano, e-mail: [email protected]/[email protected], WhatsApp namba: 0756 700 496/0715 973 952. Twitter:@BasataTanzania & tovuti: www.basata.go.tz