Kanuni, taratibu za Ligi Kuu ziheshimiwe

Muktasari:

  • Msimu mpya wa ligi kwa namna moja au nyingine ni mwanzo wa baadhi ya watu kujipatia ajira, wakiwamo wachezaji, waamuzi na wengineo wanaojihusisha na uendeshaji wa michezo,  ikiwamo soka.

Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, VPL msimu wa 2016/17 imeanza na baadhi ya timu  tayari zimecheza mechi tatu.

Timu 16 zinashiriki ligi hiyo kama ilivyokuwa msimu uliopita huku kanuni na taratibu za uendeshaji,  zikiwamo za klabu kuwa na viwanja vya mazoezi na  vikosi vya vijana zikihimizwa.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limehimiza kwa muda mrefu kuhusu viwanja na timu za vijana na hili halihitaji kuzungumziwa tena.

Jingine ni klabu kuajiri makocha wenye ujuzi unaotambuliwa na mamlaka zinazosimamia mchezo huo katika bara la Afrika na duniani.

Msimu mpya wa ligi kwa namna moja au nyingine ni mwanzo wa baadhi ya watu kujipatia ajira, wakiwamo wachezaji, waamuzi na wengineo wanaojihusisha na uendeshaji wa michezo,  ikiwamo soka.

Kwa jumla, tunakubali kuwa soka ni ajira ambayo ikitumiwa vizuri inaleta tija, si kwa wachezaji pekee, bali jamii kwa jumla na ndiyo maana katika siku za karibuni tumeambiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba soka ni chanzo cha kodi.

Tunaamini, kodi zitakazotokana na uwekezaji katika soka, zitaisaidia nchi yetu kupiga hatua na wakati huo kuwezesha vijana wanaoajiriwa au kujiajiri katika sekta hiyo wajipatie maisha yenye staha.

Tunaposema maisha ya staha, tunamaanisha  vijana waanaojishughulisha na soka kuwa wanaweza kuishi vizuri kama  ilivyo kwa watumishi wa umma au binafsi, ikiwa watatumia vyema vipaji vyao.

Tunawashauri  wanasoka wetu,  wawe makini, wajitambue kuwa wanashiriki mchezo ambao kwingineko duniani una heshima, unalipa na kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana ama usajili au uhamisho wa wachezaji, tena kwa fedha nyingi.

Usajili huo wa kifahari wa fedha nyingi umeanza kufanyika pia katika Tanzania ambako tumeambiwa mara nyingi kuwa mchezaji mmoja amegharimu Sh100 milioni au zaidi ambazo tunajiuliza, ni jinsi gani wahusika wanavyonufaika.

Mbali ya mapato yanayotokana na soka, tumesema kuwa klabu zimeanza msimu zikitakiwa kuwa na viwanja vyao wenyewe, jambo ambalo tunaamini kuwa halijafanyika kwa klabu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo.

Unaweza kujiuliza, nini kinazikwamisha klabu zetu kubwa na ndogo kumiliki viwanja vyao zenyewe, kiasi cha kulazimika kukodi vya watu binafsi, mashirika au vyama, ikiwamo chama tawala, CCM kwa ajili ya kuchezea?

Tunazipongeza klabu kama Azam, Mtibwa na kidogo zile za mkoani Pwani, JKT Ruvu na Ruvu Shooting, ambazo zimekuwa zikitumia viwanja vyao.

Tunapenda kutumia nafasi hii kuzitaka klabu kubwa, Yanga na Simba zifikirie kuwa na viwanja vyao, ambavyo zitavitumia katika mechi zake mbalimbali na hata mazoezi. Kama haziwezi kila moja kumiliki uwanja wake, zinaweza kufikria kujenga mmoja na kuumiliki kwa ubia. AC Milan na Inter zinazocheza Ligi Kuu ya  Italia, Serie A. Timu zinatumia uwanja mmoja unaomilikiwa na Manispaa ya Milan.

Ni jambo jema kwa Azam kutaka mechi zake za nyumbani zifanyike Azam Complex, zikiwamo za Simba na Yanga.

Tunashauri Azam isiwekewe vikwazo katika nia yake hiyo njema ya kuutumia uwanja wake wa Chamazi kikamilifu kwani ndiyo huohuo ambao umekuwa ukitumika kwa mechi za kimataifa za timu hiyo na hata zile zilizohusisha timu za taifa hususan za vijana na wanawake.

Tunaamini kwamba kwa kutumia uwanja wake kwa mechi zote za nyumbani, itakuwa ni chachu kwa timu zitakazokuwa zikifika hapo hasa Simba na Yanga kwani zitakuwa na kitu cha kujifunza hasa ikizingatiwa kwamba pamoja na umri mkubwa zilionao, hazijapiga hatua kubwa kama hiyo.