TUONGEE UJANA: Kijana piga hatua, mafanikio yapo hatua chache kutoka ulipo

Muktasari:

  • Changamoto ulizonazo zitapita. Zitapitaje, zitakuacha katika hali gani? Mwamuzi ni wewe.

Katika maisha kuna nyakati mbili kuu. Nyakati za furaha na huzuni. Kila binadamu ana namna ya kupokea nyakati hizi.

 Wapo wanaokata tamaa wakati wa huzuni na kufanya mambo ambayo yatakayowafanya wawe na huzuni daima na pia wapo wanaotumia vibaya nyakati za furaha na hatimaye kuingia kwenye huzuni isiyokoma.

Vijana walio wengi huchanganywa na nyakati hizi na kushindwa kuamua wasonge mbele, warudi nyuma au wawe watumwa wa watu au vitu fulani.

Kuna mambo yanapaswa kufanywa ili kukabiliana na kipindi cha huzuni ambayo ni pamoja na kuamini kuwa hakuna magumu yanayokuja bila sababu maalumu.

Hii ni kwa sababu kila linalotokea lina dhumuni maalumu maishani mwa kila mtu, hivyo jambo la msingi ni kuhakikisha hicho hakiwi kikwazo cha kukatisha ndoto zako za kusonga mbele.

Mafanikio au kushindwa kupambana na hilo gumu ndiyo njia utakayokuwa umechagua kupita, kwa maana ya waliokubali kushindwa na kuwa watumwa wa kushindwa au kupambana na kushinda ili uwe sehemu ya wanaoshangilia mafanikio.

Cha kujifunza baada ya mapambano ya wakati wa huzuni na kupitia magumu, ni kutosahau nyakati hizo kwa sababu zitajirudia wakati wowote, kulingana na ulivyopokea ushindi au kushindwa.

Kuna msemo maarufu usemao “ Tumia changamoto kama mawe ya kujengea daraja litakalokuvusha upande wa pili”.

Kumbuka siku zote hakuna mafanikio rahisi, hivyo ukiona magumu, changamoto zinakuwa nyingi utambue mafanikio yapo karibu, tena inawezekana hatua chache kutoka ulipo. Inua mguu, piga hatua uyafikie.

Wahenga walisema “Giza la usiku linapokuwa nene sana ujue alfajiri imekaribia”.

Uvumilivu iwe silaha kuu, usisahau kuwa na mtizamo chanya kwa kila unalotaka kufanya. Usitangulize haiwezekani kwa sababu kila jambo linawezekana kwa bidii, maarifa, uvumilivu na kujituma, wakati unafanya hayo pokea ushauri wa maana achana na wanaokukatisha tamaa, angalia unataka kupata nini katika hilo jambo unalofanya.

Kama ambavyo giza halidumu milele na mitihani ya kimaisha pia  vivyo hivyo ongeza mapambano na magumu, huzuni,changamoto ulizonazo zitapita pia. Zitapitaje, zitakuacha katika hali gani? Mwamuzi ni wewe.

Vivyo hivyo unapopata mafanikio pambana kuhakikisha yanadumu na kukua zaidi, badala ya kuyaacha yalipo au kukubali yapotee.

Wakati wa mafanikio marafiki wa kweli na maadui marafiki huwa wengi, hapa ndipo busara, hekima au kukumbuka ulipotoka vinapohitajika.

Jifunze kwa waliofanikiwa, yafanyie kazi mawazo yao mazuri, huku ilichanganya na akili yako kuhakikisha unatimiza ndoto zako za mafanikio.

Wakati huu ujana huchukua nafasi kubwa, siku zote kumbuka usemi wa Wahenga usemao “Ujana Maji ya Moto” .

Itumie vizuri nafasi ya kuchanua kwenye mafanikio badala ya kuchanganya mambo, kama unasoma, unafanya kazi, unalima, unafuga fanya hayo yote huku ukiwa na hofu ya kushindwa, kwa sababu kushindwa siyo sehemu ya malengo yako.

Zingatia malalamiko, lawama hayana nafasi katika safari hiyo ya mafanikio uliyoianza, usikubali kumtaja mtu mwingine kuwa chanzo cha wewe kushindwa.

Kwa sababu umeshatoka na umeanza safari ya mafanikio ushindi ndiyo njia sahihi unayotakiwa kupita. Piga hatua njia hiyo ipo karibu na hapo ulipo. Sina uhakika lakini kwa mtizamo njia hiyo ipo hatua chache kutoka hapo ulipo.