TUONGEE UJANA: Kupanga ni kuchagua, huyawezi yote fanya ya muhimu

Muktasari:

Si kila ushauri unapaswa kuuchukua, chuja na iwapo utakufaa chukua.

Kwa mara nyingine, karibu katika jukwaa maalumu kwa ajili ya vijana kuelimishana, kukumbushana na kuhimizana kufanya yale yanayopaswa kwa rika muhimu kwa ujenzi wa taifa.

Kama ilivyo ada mambo ya kufanya katika kipindi cha ujana ni mengi, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa kupanga ni kuchagua.

Nimetumia msemo huo wa kupanga ni kuchagua kama ambavyo umekuwa ukitumiwa na wahenga nikimaanisha mambo ya kufanya ni mengi, lakini umakini unahitajika wakati wa kupanga na bila kusahau kuchagua ni muhimu, kuliko kulazimisha kuyafanya yote kwa wakati mmoja.

Jambo la msingi ni kuhakikisha unachambua bila shaka wala kusuasua na ukajipa sababu mujarabu kwa nini umepanga kufanya hayo unayotaka kuyafanya ni lipi lianze lipi lisubiri.

Wapo waliojaribu kufanya mambo yote kwa wakati mmoja matokeo yake hawakufanya vizuri katika yote, au yaliishia kati na kutotoa matokeo chanya. Na kama yalimalizika kwa kuchukua muda mrefu na kupitiliza sababu na malengo ya kufanywa.

Kwa mfano, umepanga na unataka kujenga nyumba kubwa ya kisasa, ili kuondokana na nyumba ya kupanga iliyokuchosha, lakini fedha uliyonayo haitoshi kumaliza nyumba kwa sababu unataka ununue na gari.

Hapo unapaswa upange na uchague, uendelee kuteseka kwenye nyumba ya kupanga?  Au ununue gari kuepuka adha ya usafiri.

Kama utachagua vizuri fedha hiyo hiyo unaweza kuitumia kununua gari na kuishi nyumbani kwako kwa kujenga banda la vyumba vichache na kuhamia huku ukijipanga kwa ajili ya kujenga taratibu nyumba ya ndoto yako.

 Lakini ukilazimisha utanunua gari na utajenga nyumba ya ndoto yako ambayo haitamalizika, hivyo utakuwa hujahamia kwako na hujamaliza nyumba.

Huo ni mfano tu wa kupanga na kuchagua kwa kujiridhisha, unaweza kufanya hivyo pia katika maeneo ya kazi, ama uwe mchapakazi hodari, uwe miongoni mwa wafanyakazi, uwe mfanyakazi wa vipindi maalumu, yaani kuna kipindi unafanya kazi kwa bidii na kuna kipindi unatega kwa visingizio hivi na vile.

Jikumbushe kila siku unataka nini maishani mwako huku ukiupa muda nafasi kwa sababu huwa haudanganyi.

Mafanikio uyawazayo hutokana na uchaguzi na mipango yako, kufanya jambo kwa kukurupuka kutakufanya uwe kama kipepeo unarukia kila tawi mwisho ujana unakupita ukiwa hujakamilisha jambo lolote. Yote unakuwa umeyagusa na kuyaachia hewani.

Pamoja na kupanga na kuchagua nidhamu, uvumilivu , kujali muda ndiyo nyenzo itakayobeba mafanikio ya ulichokipanga na kukichagua.

Kabla ya kuchagua nini ufanye katika uliyoyapanga jipe sababu muhimu  na za msingi  kwa nini unaanza kukifanya ulichokichagua, jipe muda wa kuanza utekelezaji ili usije kujuta katika hatua za awali au mwishoni, hiyo itakufanya uchukie hilo jambo.

Amua mustakabali wa maisha yako na usiangalie itamfurahisha au kumuumiza nani, usitake upewe majibu ya ulichokiamua na mtu mwingine, kama kina maswali, changamoto, majibu na utatuzi wake unao wewe mwenyewe.

Makala haya yameandikwa na Kalunde Jamal