Mashabiki wanakuza malumbano wanawashusha wasanii

Hakuna cha kustaajabisha kwenye malumbano ya Alikiba na Diamond au Vanessa Mdee na Shilole kwa sababu yote ni marudio ya yaliyofanywa na Sikinde na Msondo Ngoma enzi hizo; isipokuwa tu malumbano ya Ommy Dimpoz na Diamond au ya Billnass na TID.

Malumbano ya kisanaa baina ya msanii na msanii au bendi na bendi ni jambo lilikuwepo tangu miaka ya nyuma duniani kote; tena kwa kipindi kile yalikuwa yanakwenda mbali zaidi na kufikia hatua mbaya kabisa ya hadi wasanii kuuana; rejea kifo cha rapa 2pac Shakur wa Marekani kuthibitisha hilo.

Wataalamu wa mambo wanadai kuwa malumbano au kwa lugha ya mtaani ‘bifu’ huwa na matokeo makuu ya aina mbili.

Matokeo chanya ambayo hupatikana endapo tu wasanii wanaovutana wanaungwa mkono na mashabiki wa ukweli, (mashabiki ambao msanii wao atakapofanya onyesho watajaa kumuunga mkono na bado watanunua kazi zake). Mfano ni mashabiki wa Sikinde na Msondo, mashabiki wa pande zote mbili walikuwa wakiupa nguvu upande wanaouunga mkono kwa kujazana kwenye maonyesho ya kila wiki yaliyokuwa yakifanyika hasa jijini Dar es Salaam.

Aina ya pili ni matokeo hasi ambayo hutokea endapo wasanii wenye mgogoro wanaungwa mkono na mashabiki uchwara.

Hawa ni mashabiki ambao wenyewe wamehitimu katika suala zima la kummwagia matusi mpinzani wao katika mitandao ya kijamii—kwa jina la mtaani wanaitwa ‘mashabiki maandazi’. Wao hawana muda wa kuhudhuria shoo za msanii wao, hawana muda wa kununua kazi zake lakini kwenye simu wanazo, kikubwa wanachokijua ni kuanzisha ‘hashtag’ zenye kumpa ‘bichwa’ msanii wao huku zikimuongezea umaskini na upofu wa kushindwa kutazama njia za jinsi anavyoweza kupata mafanikio kiuchumi kupitia sanaa anayoifanya.

Kwa juhudi wanazofanya wasanii wetu hasa wa Bongo Fleva tulitakiwa tuwe mbali zaidi ya hapa tulipo leo; lakini tunaridishwa nyuma na mashabiki uchwara.

Kwa mfano; utakuta msanii wa Tanzania yumo katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo fulani za kimataifa na ili kushinda ni lazima awe na kura nyingi za mashabiki zaidi ya wasanii wote.

Lakini kwa sababu tu msanii huyu anakuwa na ‘bifu’ na msanii mwingine wa nyumbani basi mashabiki uchwara huwa radhi kutompigia kura msanii wa Tanzania, badala yake kuhamasishana na kumpigia kura mwingine kutoka nje ilimradi tu tuzo isiende kwa mpinzani wao—haya siyo malumbano ya ushabiki wa sanaa.

Bifu linastahili kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa wasanii; yaani wenye msuguano wakiandaa tamasha la pamoja mashabiki wafurike kwa kiasi kikubwa; au labda zile ‘hashtag’ wanazozianzisha kwenye mitandao ya kijamii zihamie kwenye fulana ambazo msanii ataziuza kwa kuzifanya kupata pesa ya kujikimu.

Mashabiki uchwara wanaokuza bifu walistahili kuwa chachu ya wasanii kutoa albamu kwa sababu kwa sasa wasanii hawafanyi hivyo na moja ya sababu ni kwamba hakuna wanunuzi.

Kimsingi hatuwezi kuzuia misuguano katika sanaa, kwani ni kitu cha lazima ambacho hata katika maisha nje ya usanii tunakumbana nacho. Tuna maadui katika maeneo tunapoishi, makazini na kwingineko—hatuwezi kuishi bila kuwepo kwa migororo.

Cha msingi tunachohitaji ni bifu zinazoungwa mkono na mashabiki wa damu, mashabiki ambao badala ya kuwadidimiza wasanii watawainua kiuchumi na hapa ndipo wanamuziki wetu wataona faida ya misuguano kwenye sanaa.

0713 48 28 16