Prof Ndalichako, wenzio tuepushieni mtego huu wa panya!

Muktasari:

Nchi yake, Tanzania ameonyesha kuipenda na kuitumikia kwa moyo wake, pengine akiwa peke yake, akiachwa nyuma na mifumo, inatetereka kwa kiasi cha kuanza kutia hofu na wasiwasi, kwani sekta ya elimu, ikiwamo ile ya juu inafanyiwa mzaha.

Mwaka mmoja tangu Rais John Magufuli aingie madarakani unapokaribia, yaani Novemba 5 ambayo haipo mbali, kwa ufupi, kiongozi huyo mkuu wa nchi amekuwa akijiainisha kuwa mkusanya kodi, mtu wa watu wakiwamo wanyonge, ingawa kwa sasa safari ndani ya meli yake ya matumaini inakwenda mrama!

Nchi yake, Tanzania ameonyesha kuipenda na kuitumikia kwa moyo wake, pengine akiwa peke yake, akiachwa nyuma na mifumo, inatetereka kwa kiasi cha kuanza kutia hofu na wasiwasi, kwani sekta ya elimu, ikiwamo ile ya juu inafanyiwa mzaha.

Tumeona mengi yakitendeka, tunamkumbuka jinsi Magufuli alivyoahidi elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne ametenda na mambo yameanza vizuri, ingawa kuna chembe za shaka kuhusu fedha zinazotengwa na Serikali yake na kuwekezwa kwenye sekta hiyo kama zinatumika vizuri au zinaliwa.

Ninaona shaka, ninaifikiria migomo ikiwamo ya wanafunzi wa elimu ya juu, wahadhiri kwani tumeambiwa kuwa wengi wa wanafunzi, zaidi ya 60,000 nchini hawana mikopo ya kuwawezesha kusoma kwenye vyuo vikuu, vikiwamo vya umma na binafsi licha ya kuwa wamechaguliwa kuanza masomo muhula huu, baadhi yao wameripoti vyuoni, lakini bila fedha za ada, pango na hata zile za kujikimu, jambo ambalo ni hatari.

Kwa bahati nzuri, tulishaanza kusahau migomo, lakini kwa hali ilivyo sasa inaelekea kuwa bila umakini wa kimkakati ulio thabiti, siku si nyingi tutaiona tena ikitokea na kuwaathiri wazazi, walezi, wakiwamo wanaojinyima ili kuwasomesha watoto wao walioanza elimu ya juu, lakini bila mikopo licha ya kuwa na sifa zote zilizoainishwa na Serikali ya Rais Magufuli.

Ni kwa masikitiko, nachelea kusema jambo hili linaweza kuepukwa kama kauli yake (Rais Magufuli) kwamba atahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapatiwa mikopo na kwamba Serikali yake haitakubali kuelekeza mikopo hiyo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa, kama ingetimizwa.

Wakati akiwahutubia wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Juni mwaka huu, Rais Magufuli alisema Serikali yake itatoa elimu bora kwa Watanzania na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto zinazovikabili vyuo.

Nimkumbushe Magufuli au Mtoto wa Jeba kwamba alieleza kusikitishwa na kuwapo kwa wanafunzi waliodahiliwa na baadhi ya vyuo bila kuwa na sifa zinazowawezesha kujiunga na taasisi hizo za elimu ya juu.

Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya kisasa ya UDSM, inayojengwa Kampasi ya Mlimani kwa msaada wa Korea Kusini,Rais Magufuli alieleza kuwa wapo wanafunzi waliokopeshwa kusoma elimu ya juu, lakini hawana sifa.

Alimueleza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuwa hatua alizochukua msomi huyo ili kusafisha wizara zilikuwa za kutia moyo, jambo ambalo nampongeza pia leo Ndalichako na bosi wake kwa yale wanayoyasimamia, yakiwamo ukaguzi wa vyeti vya taaluma kwa walimu na watumishi wengine, mishahara iliyokuwa ikilipwa kwa watu wasiostahili na kadhalika.

Kwa bahati mbaya, maneno kwamba atahakikisha wanafunzi wenye sifa wanasoma ni kama yameanza kumrudi Dk Magufuli, kwani vijana walijisomea, kufaulu mitihani yao ya kidato cha sita na mingineyo, wenye sifa za kudahiliwa kwenye vyuo vikuu, wamekosa mikopo. Kwanini?

Hao, siyo vilaza kama alivyowaita Magufuli, walifaulu vizuri na kupata daraja la kwanza au la pili, sifa ambayo Prof Ndalichako aliahidi kuwa ingewawezesha kudahiliwa na hata kupewa mikopo.

Kwa bahati mbaya, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imeanza vibaya kwa kushindwa kuwatangazia wanafunzi wanaostahili mikopo, hata katika chuo kimoja, UDSM, achilia mbali vingine, Sokoine (Sua), Chuo Kikuu Dodoma na vinginevyo, vikiwamo vya binafsi ambako baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wamerudishwa kwa wazazi na walezi wao ili kusaka ada, fedha za usajili, za kujikimu na nyinginezo.

Niseme wazi, mimi ni mmoja wa wazazi, lakini ninaumizwa na hilo linaloendelea kutokea kwa watoto wetu ambao walijituma, wakasoma kwa bidii, kufaulu, sasa Serikali ya Dk Magufuli haina uwezo wa kuwapa wote mikopo. Naamini Magufuli anakosa usingizi, kwani alieleza kuumizwa na tabia hiyo, hasa kwa mikopo ambayo watarejesha baada ya kuhitimu masomo yao, kama wanavyofanya baadhi yao kwa sasa, ingawa wapo wanaolalamikia fedha ambazo wanakatwa kwamba hazilingani na zile walizokopeshwa.

Ni wazi kuwa Prof Ndalichako, ambaye sina shaka ni zao la elimu ya bure ya zama za Mwalimu Julius Nyerere na awamu yake ya kwanza ndiye anayebeba dhamana kubwa ya kumshauri bosi wake namna nzuri ya kuondokana na tatizo hili kubwa, zito linaloiumbua nchi yetu.

Haiwezekani, Tanzania ambayo hata kama ndoto zake ni kuwa nchi ya viwanda, ikawa ya kibaguzi, kwa kutoa mwongozo huu wa kuwasomesha kwa mkopo wanafunzi wanaosoma sayansi, ualimu na kuwaacha wengine kwa sababu hizo ambazo juzi Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella Manyanya alizitetea hadharani na kuonekana kwenye vyombo vya habari.

Sitaki kuamini kuwa wanafunzi wa fani mbalimbali za sayansi au wa ualimu ndio wanaostahili mikopo au ndiyo waliozaliwa kwenye familia ambazo hazina sababu ya kukopeshwa.

Ukiondoa wanafunzi wachache wenye kile kinachojulikana kama uhitaji kama vile kutokea kwenye familia masikini, wenye ulemavu na wengineo, ambao tumeambiwa na Waziri Manyanya kuwa ndiyo wanaostahili mikopo, wengine wanabaguliwa.

Siielewi Serikali yetu ilitaka nini ilipotaka vijana waombe mikopo wote, je, ilitaka wadhalilike kwa kujiona kwenye mitandao kwamba wamekosa mikopo, lakini bila kuelezwa sababu za msingi?

Je, Serikali yetu ilitaka wazazi au walezi waseme uongo kwamba ‘wamekufa’, hata kama bado wako hai, wadai eti hawana uwezo ili watoto wao waweze kupewa mikopo? Je, Serikali inaamini wanafunzi wa sayansi wote hawana uwezo, ikilinganishwa na wenzao wa sanaa? Je, kusema ukweli kwa wazazi au walezi wengi ndiyo sababu ya watoto wao kutopewa hata senti ya sehemu ya mikopo hiyo wanapojiunga na vyuo vikuu ambavyo kama nilivyoeleza awali, vijiandae kwa migomo mipya kwani wale ambao waliahidiwa mikopo hiyo, ikacheleweshwa mno wakianza kugoma, watafuatiwa na walimu au wahadhiri wao, sekta nzima itaathirika.

Huu ni mtego wa panya ambao waswahili husema, hunasa waliomo na wasiokuwamo! Naamini, Tanzania inaweza kuuepuka mtego huo kwa busara za kuangalia upya vigezo hivyo ambavyo Waziri Manyanya anavipigia debe na kuangalia uwezekano wa kuiepusha sekta hiyo kwenye mizozo.