Sheria ya faini ya bima isitozwe kwa fedha za kigeni

Muktasari:

Baada ya Mtolea kukiri makosa yote, Hakimu wa Mahakama hiyo, Eriarusia Nassary alimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Pauni 100 za Uingereza kwa kosa la kuendesha gari ambalo bima yake imekwisha muda wa matumizi. Katika kosa la pili, alimhukumu kulipa faini ya Sh30,000.

Hukumu ya kesi ya kuendesha gari, iliyotolewa juzi dhidi ya Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea imeibua jambo jipya, kwamba faini inayotajwa na sheria husika, inatozwa kwa Pauni ya Uingereza.

Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke baada ya Mtolea kutiwa hatiani kwa kuendesha gari likiwa na bima iliyokwisha muda wa matumizi na kukataa kutii amri ya ofisa wa polisi.

Baada ya Mtolea kukiri makosa yote, Hakimu wa Mahakama hiyo, Eriarusia Nassary alimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Pauni 100 za Uingereza kwa kosa la kuendesha gari ambalo bima yake imekwisha muda wa matumizi. Katika kosa la pili, alimhukumu kulipa faini ya Sh30,000.

Kutokana na hukumu hiyo na kwa mujibu wa viwango vya kubadilisha fedha juzi, mtuhumiwa alilipa Sh291,000 sawa na Pauni 100 za Uingereza, lakini kiwango hicho kinaweza kubadilika siku hadi siku kulingana na viwango vya kubadilisha fedha wakati huo.

Hatukusudii kuzungumzia makosa au tuhuma zilizomfikisha mbunge huyo mahakamani wala mashtaka yake na jinsi yalivyoendeshwa, bali lengo letu ni sheria iliyotumika kumtia hatiani na kulipa faini, Sheria ya Bima za Magari ya mwaka 2002, Sura 169 kifungu cha 4(1), 4(2), inayotambua Pauni za Uingereza badala ya Shilingi ya Tanzania.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu akikutwa anaendesha gari ambalo bima yake imeisha muda wa matumizi, adhabu ni kifungo cha miezi sita jela au faini ya Pauni 100 za Uingereza.

Pamoja na kwamba sheria hiyo ni halali kama nyingine zilizotungwa na Bunge, hatuoni sababu kwa nini iendelee kutambua adhabu ya faini inayolipwa kwa fedha za nje badala ya fedha zetu.

Kwa muda mrefu kumekuwapo kilio cha wadau wa uchumi juu ya utozaji wa fedha za kigeni katika huduma mbalimbali zinazotolewa nchini, suala ambalo linadaiwa kuwa chanzo cha fedha zetu kushuka thamani yake.

Mathalan, kulikuwapo malalamiko kuhusu uuzaji wa muda wa maongezi ya simu za mkononi kwa dola ambayo baada ya malalamiko utaratibu ukabadilika na sasa muda huo unalipwa kwa shilingi.

Hata hivyo, huduma nyingine kama baadhi ya hoteli na maduka mbalimbali zimeendelea kutolewa kwa njia ya fedha za kigeni, huku wahusika wakieleza kuwa wateja wao wanatoka katika mataifa mbalimbali.

Pamoja na hayo, tunatambua kuwa Serikali imekuwa inapambana na watu mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa huduma kwa kutumia fedha za kigeni hapa nchini ili kulinda nguvu ya shilingi yetu, na tunashauri juhudi zaidi zifanyike ili kuiwezesha shilingi ya Tanzania kuwa imara zaidi.

Kwa mfano, hivi karibuni Benki Kuu Tanzania (BOT) ilifanya mapitio katika kanuni za uendeshaji wa maduka ya kubadilisha fedha kwa lengo la kuweka usimamizi wa biashara hiyo, jambo ambalo pamoja na kusimamia shilingi ya Tanzania pia linaweza kusaidia kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu.

Hivyo, pamoja na juhudi hizo zinazoendelea katika maeneo mengine, tunashauri hata upande wa sheria uangaliwe ili zile ambazo zinaendelea kutambua fedha za kigeni badala ya shilingi ya Tanzania zifanyiwe marekebisho haraka.

Ni matarajio yetu kuwa sheria hiyo itarekebishwa na kusisitiza zaidi matumizi ya shilingi yetu, badala ya fedha za kigeni kama pauni au dola. Tunayo fedha yetu tuithamini ili iwe na thamani zaidi.