MAONI YA MHARIRI: Tusiishie kusherehekea kumaliza mwaka, tutafakari

Sunday December 31 2017

Shamrashamra za manma hii za kufungua shampeni

Shamrashamra za manma hii za kufungua shampeni zitakuwa za maana kwetu endapo zitaambatana na tafakuri ya mwaka uliopita 2017 ili kuona wapi tulikosea na wapi tunatakiwa kusahihisha mwakani kuanzia kesho. Picha ya maktaba. 

By MWANANCHI

Leo ni siku ya mwisho ya mwaka 2017, kesho panapo majaliwa, tutauanza mwaka mwingine wa 2018.

Kwa kawaida, aghalabu siku hii huadhimishwa kwa sherehe mbalimbali, baadhi wakifanya ibada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuuona mwaka mpya lakini pia wapo wanaotumia siku ya kwanza ya mwaka huo kula, kunywa, kucheza na aina nyingine nyingi za shughuli alimradi kuonyesha furaha yao.

Kutokana na ukweli kwamba wapo wanaosherehekea kiasi cha kuvuka mipaka ya kiimani na pia kuvunja sheria za nchi, ndiyo sababu viongozi wa dini wamekuwa wakisisitiza, nasi tukiwaunga mkono kwamba siku hii inapaswa kutumiwa na binadamu kurejea kwa Mola Muumba wao kumshukuru kwa kuendelea kuwa hai na kumuomba awajaalie na kuwawezesha kutimiza malengo waliyojiwekea kwa mwaka unaofuata.

Kwa wale wanaovuka mipaka ya kusherehekea kiasi cha kuhatarisha usalama wao na wa wengine, Jeshi la Polisi limekuwa likitoa angalizo kwao. Nasi tunasisitiza kwamba furaha ya kuuona mwaka mpya ni yetu sote, usiitumie vibaya kiasi cha kuwakera wengine.

Pamoja na utangulizi huo, ni vyema tukumbushane njia bora zaidi ya kusherehekea kumaliza mwaka baada ya kupiga magoti na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake kwako.

Tukumbuke kwamba kadri siku zinavyosonga, ndivyo umri wetu unavyokuwa na kwa wengi wetu, ndivyo majukumu yanavyoongezeka, baada ya shukurani kwa Mola na kushereheka kidogo, kipindi hiki ni muhimu sana kuketi na kutafakari changamoto tulizokuwa nazo katika mwaka unaoisha na kuweka mikakati ya namna tutakavyokabiliana na changamoto mpya mwakani.

Tunatakiwa kufanya tathimini ya nyendo zetu kwa mwaka unaokwisha na kutazama nanona bora zaidi ya kuingia katika mwaka ujao tukiwa wenye manufaa zaidi kwetu sisi na kwa jamii kwa ujumla.

Ni kipindi cha kujitafakari, kujitathmini na kujiwekea alama kutokana na yale uliyoyafanya mwaka uliopita. Kama maksi zako zilikuwa juu, ni muda wa kuangalia njia bora zaidi ya kuzifanya ziendelee kuwa juu zaidi na kama ikiwa zilikuwa chini kazi kubwa ni kuhakikisha unakuwa na malengo sahihi ya kuzipandisha.

Tathmini hii isiishie kwa mtu mmojammoja au familia tu, tuangalie taasisi zetu tunazozisimamia, mashirika tunayoyaongoza au tulizomo, tumetimiza wajibu wetu kuhakikisha zinapata mafanikio?

Je, tumetoa mchango gani kwa maendeleo ya Taifa letu kwa mwaka huu? Kwa lugha nyingine umelifanyia nini Taifa lako kwa mwaka huu na una malengo gani kwa mwakani badala ya kutazama tu Taifa limekufanyia nini?

Tukiishi katika misingi hii, bila shaka tutakuwa katika njia sahihi ya kuendeleza taifa letu na ustawi wetu sisi wenyewe.

Tujiulize mwaka jana tulifanya nini cha maana na mwaka huu tumepanga kufanya nini? Kama tunaishia kusherehekea na kuendelea kuishi vilevile, mwaka mpya kwetu hautakuwa na maana zaidi ya kujumlisha namba moja kila baada ya miezi 12.

Mwisho, tunapenda kuwatakia heri na fanaka ya mwaka mpya wa 2018 tukimuomba Mungu atuwezeshe kuuvuka salama na kutimiza malengo yetu.