TUONGEE UJANA: Usikubali kuwa sponji kufyonza kila unachoona

Kijana anapaswa kuwa na ndoto nyingi zenye manufaa kwake binafsi na kwa jamii kwa ujumla. Pia anabakiwa na sifa ya asili ambayo ni kijana wa kiume kuwa baba bora na wa kike kuwa mama bora.

Ninachotaka kueleza hapa ni kuhusiana na umuhimu wa vijana katika masuala mbalimbali ambayo anapaswa kuyatekeleza akiwa na mtazamo wa kizalendo.

Kijana pia anategemewa kuwa na ari ya kushiriki shughuli za kijamii, mwenye busara, soni, huruma kwa wengine  na mstaarabu.

Kwa nchi changa kama Tanzania inahitaji zaidi busara za vijana katika kuibua msisimko wa mijadala ya masuala mbalimbali ikiwamo ya kiuchumi, kielimu, kiafya,  kisiasa na kijamii.

Wakati wa kutekeleza au kuamsha mijadala hiyo inahitajika uzoefu wa kujenga hoja, kuzitetea na kuweka mbele uzalendo.

Licha ya kuweka uzalendo, bado kijana hapaswi kukurupuka kutetea au kuaminishwa kuwa lililopo, lililosemwa ni sawa  anachotakiwa kufanya ni kutumia busara, hekima kuliwasilisha au kulipinga.

Kijana hapaswi kuamini kila anachokisikia kwa sababu atakuwa hana tofauti na sponji inayofyonza kila kimiminika hata kama kitaliharibu lenyewe.

Katika hili kijana shupavu, anayejiamini na mzalendo huchunguza, hufuatilia, hujiridhisha na huja na hoja nzito kupinga au kukubali kinachoendelea katika taifa lake katika nyanja nilizozitaja hapo juu.

Simaanishi afanye vurugu anapoona kuna jambo halipo sawa. Ninachomaanisha asikubali kila analoambiwa, wanaloambiwa wengine, analoaminishwa bila kujiridhisha kama lina manufaa kwake na  kwa jamii inayomzunguka.

Kijana hapaswi kupiga makofi kwa jambo asilolijua kwa kisingizio cha suala hilo limesemwa na mkubwa ambaye yupo upande wake.

Kuwa mwanachama wa chama fulani, mwanafunzi wa chuo fulani, mkwe wa familia fulani, hakukufanyi wewe kuwa mtumwa wa fikra za tajiri wa mawazo mgando kuamini kinachosemwa na wakuu wa upande uliopo ni sahihi.

Kijana anapaswa kuhakikisha anashiriki katika harakati mbalimbali za kukomboa nchi iwe katika nyanja ya siasa, uchumi, elimu na hata jamii ilimradi havunji sheria na hasemi au habishani asichokifahamu.

Kumekuwa na tabia ya vijana kujitokeza katika baadhi ya mambo yenye maslahi nao ya moja kwa moja na kusahau kujitoa kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi utakaodumu milele.

Ufumbuzi huo ni katika mambo mbalimbali ikiwamo yanayokwamisha mustakabali wa Taifa ambayo pengine vijana wangejitokeza na kuinua mijadala mikubwa ambayo itakuwa na hoja mchanganyiko za kupinga na kukubali zinazoweza kutoa majibu.

Narudia tena kijana usikubali kuwa sponji kufyonza vimiminika kwa kisingizio cha nidhamu. Kukaa kimya kwa mambo yanayohitaji hekima zenu ni uoga.

Uoga, uzembe, kujifungia ndani ya boksi ni sumu kali kuliko ya nyoka kwa mustakabali wa kijana na Taifa alilopo, jitokezeni mlete malumbano ya hoja ili kupata muafaka wa yasiyokuwa sawa hapa nchini.

Kijana jitokeze dai haki yako hakuna atakayesimama kwa ajili ya nchi yako zaidi ya wewe.

Duniani kote inaaminika kijana ni taifa la kesho, lakini kutokana na dunia kukimbia kwa kasi msemo huo umebadilika na kuwa kijana ni Taifa la leo, kwa sababu unatakiwa uiandae kesho yako leo.

Sauti yako ukiipaza itaungana na za wengine na hatimaye kupata jibu la masuala mtambuka katika jamii inayokuzunguka.

Narudia tena kijana siyo sehemu ya waoga, wanakubali kila wanalolisikia bali hutenga muda wa kulitafakari.

Makala haya yameandikwa na Kalunde Jamal