NANI NI NANI URAIS: Freeman Mbowe: Mwenyekiti wa Chadema

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwasili kwenye Uwanja wa Extended mjini Urambo mkoani Tabora katika moja ya mikutano yake ya kisiasa. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Mbowe ni mmoja wa waasisi muhimu wa Chadema tangu mwaka 1992 na ndiye alikuwa muasisi kijana zaidi kuliko wote walioanzisha chama hicho. Baada ya kuasisiwa, alipewa jukumu la kuongoza kurugenzi ya vijana kwa miaka kadhaa lakini pia akiwa mtu muhimu katika utekelezaji wa masuala ya michakato ya ujenzi wa chama na ushauri wa usimamizi wa fedha.

Historia

Freeman Mbowe ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Jina lake la kwanza “Freeman” waliwahi kupewa vijana wengi tu waliozaliwa mwaka ambao Tanganyika ilipata uhuru. Mbowe alizaliwa Septemba 14, 1961 hapahapa Tanzania. (atafikisha miaka 54 Septemba). Baba yake, Mzee Aikael Mbowe, ni miongoni mwa wapigania uhuru wa Tanganyika walioshirikiana vyema na Mwalimu Julius Nyerere kabla na baada ya uhuru.

Wasomaji wataniwia radhi kwa sababu taarifa za elimu ya kiongozi huyu na mambo mengine muhimu yanayohusu wasifu wake na mtiririko wake haviko katika tovuti ya Bunge. Lakini pia ofisi yake haikutoa ushirikiano ili kupata taarifa hizo na hata viongozi wa juu na waandamizi wa chama hicho (ambao wengine ni marafiki zangu) waliahidi kukamilisha wasifu huo na kunipa lakini baadaye wakanieleza kuwa hawawezi kuutoa kwa sababu Mbowe siyo mgombea urais, pamoja na kuwa nilishawajulisha kuwa anachambuliwa kwa sababu anatajwa na wananchi kuwa ana sifa na vigezo.

Watu wa karibu na kiongozi huyu wamenijulisha kuwa amewahi kuwa mfanyakazi wa muda mrefu katika sekta ya fedha hapa nchini na nchi jirani na nimeambiwa kwamba amewahi kuwa mfanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kipindi kirefu.

Mbowe ni mmoja wa waasisi muhimu wa Chadema tangu mwaka 1992 na ndiye alikuwa muasisi kijana zaidi kuliko wote walioanzisha chama hicho. Baada ya kuasisiwa, alipewa jukumu la kuongoza kurugenzi ya vijana kwa miaka kadhaa lakini pia akiwa mtu muhimu katika utekelezaji wa masuala ya michakato ya ujenzi wa chama na ushauri wa usimamizi wa fedha.

Baada ya kukitumikia chama chake kati ya mwaka 1992 – 2003, Mbowe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa mwaka 2004, akichukua nafasi ya Bob Makani (sasa marehemu) na ameendelea kuongoza chama hicho kwa miaka zaidi ya 10 hadi sasa.

Pamoja na kuongoza chama, Mbowe ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), aliianza nafasi hiyo mwaka 2010 akichukua nafasi ya Hamad Rashid wa CUF, amemuoa Dk Lilian Mtei na wana watoto.

Mbio za ubunge

Mbowe, “Kamanda wa anga” alianza harakati za ubunge mwaka 1995 katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi katika Jimbo la Hai Mkoa wa Kilimanjaro. Hata hivyo, katika uchaguzi huo mgumu, mshindi alikuwa ni Mwinyihamisi Mushi wa NCCR – Mageuzi ambaye alipata kura 29,046 (52.0%), Mbowe alipata kura 15,995 (28.6%) na kushika nafasi ya pili. 

Juhudi zake alizozianza mwaka 1995, zilizaa matunda katika uchaguzi wa mwaka 2000. Safari hii akiwa amejizatiti ipasavyo, aliwashinda wagombea wa vyama vingine akiwamo wa CCM wakati NCCR ilionekana kudhoofu kutokana na migogoro. Alipata asilimia 64.5 ya kura zote.

Baada ya kukaa nje ya siasa za ushindani za moja kwa moja kwa miaka mitano, Mbowe alirejea tena mwaka 2010. Aliingia katika kinyang’anyiro kupambana na CCM iliyokuwa imemsimamisha Godwin Kimbita aliyeibwaga  Chadema mwaka 2005. Mbowe alilirejesha jimbo hilo kwa kura 28,545 (51.63%) dhidi ya 23,349 (42.17%) za Kimbita.

Mbio za urais

Mbowe siyo mgeni katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya nchi. Walau ana uzoefu wa kuisaka nafasi hiyo mara moja, na hii ilikuwa mwaka 2005. Katika uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika Oktoba 39, 2005, Chadema ilimpa fursa ya kutafuta kura za urais ili kuunda Serikali.

Lakini kabla ya siku ya uchaguzi, mgombea mwenza wa Chadema, Jumbe Rajab Jumbe (kutoka Zanzibar) alifariki dunia na hivyo uchaguzi ukaahirishwa hadi 14 Desemba mwaka huo ili kukipa chama hicho muda wa kupata mgombea mwingine. Aliyejaza nafasi hiyo alikuwa Maulidah Komu.

Baada ya matokeo kutangazwa, Mbowe aliibuka katika nafasi ya tatu akitanguliwa na Jakaya Kikwete wa CCM aliyekuwa na ushindi wa asilimia 80.28, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF aliyepata asilimia 11.68. Mbowe aliwapita wagombea wengine kama vile Augustine Mrema wa TLP na Dk Sengondo Mvungi (marehemu) wa NCCR.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mbowe hajatangaza kugombea urais na wasaidizi wake wa karibu wameniambia huenda hana kabisa mipango hiyo, lakini anaingia kwenye orodha ya wanasiasa wanaochambuliwa katika safu hii kwa sababu jamii inamtazama kama “presidential material” na kwamba anafikia sifa, uwezo, vigezo na kila mambo muhimu yanayoweza kumfanya mwanasiasa yeyote afae kuvaa viatu vya urais.

Nguvu yake

Nguvu na sifa ya kwanza ya Mbowe kwa siasa za sasa ni kuwa “Kiongozi wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni”. Katika mabunge yote duniani, huu ni wadhifa mkubwa na mara nyingi watu wanaopitia wadhifa husika huwa wanatazamwa kama “marais wanaosubiri kuingia ikulu.” Ameifanya kazi hii ya kuongoza upinzani kwa mafanikio makubwa na yanaonekana ndani na nje ya Bunge. Sifa hii ni nguvu muhimu kwake kama anataka kwenda Ikulu.

Sifa na nguvu ya pili ya Mbowe iko kwenye ujasiri. Yeye ni mmoja wa viongozi wenye ujasiri mkubwa katika masuala wanayoyafanya na anajua ni muda gani aongoze mapambano dhidi ya Serikali kwa ukali na muda gani atumie lugha nyepesi. Aina ya siasa za Mbowe ndiyo pia ilimsaidia kuwavuta vijana wengi katika chama hicho, ambao wanaendelea kufanya vizuri kwenye ulingo huo nchini. Sifa hii nadhani inamsaidia pale itakapotokea anaongoza nchi.

Tatu, Mbowe ni mtu mwenye msimamo na anayetaka mambo yafanyike na kuonekana kwa haraka, naweza kusema kuwa ni mmoja wa viongozi wanaohitaji matokeo ndani ya muda mfupi na staili yake ya uongozi imemsaidia katika maeneo kadhaa, mathalan; amekuwa Mbunge wa Hai kati ya mwaka 2000 – 2005 na katika wakati wake alihimiza kazi kubwa ya ujenzi wa sekondari za kata. Serikali ilipokuja na mkakati wa kujenga shule za kata nchi nzima, Wilaya ya Hai haikuwa na kazi hii tena. Huu ni mfano wa uongozi wenye matokeo.

Mwisho, tabia ya Mbowe inamtofautisha na viongozi wengi Tanzania. Yeye ni mtu wa kawaida naweza kusema. Akiongea na makundi ya kijamii hutumia lugha ambazo makundi hayo yangependa kuzitumia na hii ni sifa muhimu kwa viongozi waliofanikiwa duniani. Ndiyo maana mwandishi mkongwe hapa nchini, Samson Mwigamba, aliwahi kumuelelezea Mbowe kwenye gazeti moja la kila wiki, kama “…mtu wa watu “social”, anayeweza kuongea hata na walinzi na wahudumu wa chini kabisa na kutaniana nao, lakini asiyetaka mchezo kwenye kutekeleza wajibu wake. Huweza kujishusha sana kiasi kwamba wakati mwingine utamkuta akitoa “photocopy” za nyaraka za chama na hata kubana karatasi pamoja (stepling)”. Tabia za Mbowe zinamfanya awe na uhuru wa kujichanganya mahali popote na kufanya jambo lolote na sifa hii ni kubwa na muhimu.

Mwisho ni ubunifu na uwezo wa kufanya siasa za kisasa. Kati ya Watanzania waliotoa mchango mkubwa katika kubadilisha mazingira ya kisiasa kutoka zile za kizamani na kuanza kufanya za kisasa ni pamoja na Mbowe. Ndani ya chama chake mathalan, amefanikiwa kusimamia uanzishwaji wa mambo kadhaa ambayo baadaye yalikuwa maarufu kwa Watanzania, moja ya masuala hayo ni “kubuni vazi la kombati kwa chama chake” lakini pili ni kuanza utaratibu wa kutumia helikopta ili kuwafikia wapigakura haraka na kwa ufanisi. Jambo hili sasa linafanywa na vyama karibu vyote vyenye uwezo, kila vinapoona inafaa. Sifa hii ya ubunifu na uwezo wa kufanya siasa za kisasa ni mambo muhimu pia kwa mtu anayetaka kuongoza dola.

Udhaifu wake

Nayatizama mambo matatu kama udhaifu wa Mbowe:

Jambo la kwanza ni tabia ya kutangaza uamuzi mgumu na wakati mwingine asiweze kuutekeleza na au bila kuwa amekubaliana na wenzake. Mara kadhaa amewahi kusikia akitangaza maandamano makubwa au akitoa masharti makubwa kwa Serikali na kuna wakati haikuyatekeleza na hakuchukua hatua zaidi. Wepesi huu wa kutangaza maazimio kadhaa bila kufanya mashauriano ya kina, mapana na ya kimkakati na wadau wote wa ndani na nje ya chama chake – vinampunguzia uwezo wa kiutendaji ambao amekuwa akizoeleka nao.

Udhaifu wa pili ni katika kufanya uamuzi. Watu waliofanya kazi na Mbowe ndani ya Chadema kwa muda mrefu, wameniambia kuwa ana tabia ya kufanya uamuzi kwa haraka mno na ana tabia ya kuamini taarifa za watu anaowaamini, hataki hakuzichuja vizuri. Staili hii ya uamuzi na tafakuri ya mambo ni upungufu ambao unaweza kumwangusha kiongozi yeyote. Mara kadhaa nimesisitiza kuwa kiongozi mzuri hupaswa kufanya uamuzi, lakini hupaswa kuyafanya kwa utaratibu na akijipa muda wa kutosha wa kupima athari zake ziwe za muda mfupi na muda mrefu.

Tatu, Mbowe kwa kipindi kirefu amekuwa akihimili siasa za kiuhamasishaji na harakati na kuna wakati amewahi kusikika kwenye chombo kimoja cha habari akisisitiza kuwa chama chake kinaachana na siasa za harakati. Kwa umri wa vyama kama Chadema, si sahihi kufanya harakati hadi hivi sasa. Kimeshakomaa na kinahitaji kujipanga kushirikiana na vyama vingine vilivyokomaa kupewa ridhaa ya uongozi nchi. Siasa za kiuhamasishaji za Mbowe pamoja na ufanyaji harakati pana vinaweza kuwa udhaifu mwingine ambao bado ameendelea kuushikilia, pamoja na kuwa chama chake kinakwenda mbele zaidi, kikianza kuhimili kasi ya siasa za kitaifa, za kupigania nchi na siyo harakati za kawaida au masuala madogo.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?

Mambo mawili makubwa yanaweza kabisa kumvusha Mbowe na akawa mgombea urais wa Chadema na labda baadaye Ukawa:

Moja, yeye ni mhimili muhimu wa ukuaji wa Chadema. Chini ya uongozi wake, ndipo kwa mara ya kwanza Chadema kilipata wabunge wenye ujasiri mkubwa, kina Zitto Kabwe, Halima Mdee na wengineo na kwa wakati huo chama hicho kilikuwa na wabunge wengi kuliko vingine vya upinzani Tanzania Bara. Lakini pia, chini ya uongozi wake ndipo kiliruka kutoka kuwa na wabunge 11 kwa ujumla katika Bunge la Muungano mwaka 2005 hadi kuwa na wabunge zaidi ya 40 mwaka 2010. Mafanikio haya yametokea chini ya usimamizi wake na huenda yakawa moja ya sababu za kumpitisha kugombea urais ili aweze kusimamia mabadiliko makubwa ya nchi.

Lakini jambo la pili ni uzoefu wa muda mrefu ndani ya siasa za upinzani. Tofauti na wanasiasa kadhaa wakubwa ambao tangu mwaka 1992 hadi leo wamekuwa kwenye vyama vitatu au vinne, Mbowe amekaa Chadema muda wote huo na amekijua vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa mbunge na hata mgombea urais kwenye kipindi kimoja. Uzoefu huu unaweza kuifanya Chadema pia imuone kama mtu muhimu katika nafasi ya urais.

Nini kinaweza kumwangusha?

Mambo mawili makubwa yanaweza kumwangusha katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya Chadema:

Jambo la kwanza ni umaarufu na ukuu ambao Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa, ameujenga kwa Watanzania. Pamoja na kwamba Mbowe alikabidhiwa uenyekiti wa Chadema na Dk Slaa akiwa Katibu Mkuu wake miaka 10 iliyopita, lakini kwenye Bunge la mwaka 2005 – 2010 ambalo Mbowe hakuwemo, Dk Slaa, Zitto na Mdee walikuwa miongoni mwa watu waliofanya kazi kubwa ya kujenga taswira ya Chadema. Baada ya hapo Dk Slaa aligombea urais mwaka 2010 na kupata kura nyingi kiasi cha kuitikisa CCM. Ikiwa Dk Slaa atahitaji kugombea nafasi hiyo tena mwaka huu, huenda chama hicho kikampa nafasi kubwa zaidi na hivyo Mbowe akasubiri wakati mwingine.

Jambo la pili ambalo ni la moja kwa moja, ni ikiwa Chadema haitatoa mgombea Rais. Sielewi viongozi wa Ukawa wanapanga kutumia utaratibu gani kumpata mgombea urais, lakini ikitokea nafasi hiyo inakabidhiwa kwa chama kimoja na chama hicho kisiwe Chadema, moja kwa moja Mbowe atapaswa kujipanga kwa majukumu mengine zaidi.

Asipochaguliwa (Mpango B)

Mbowe anaweza kuwa na mipango mitatu ikiwa hatapitishwa kugombea urais:

Moja ni kugombea ubunge katika Jimbo la Hai – Kilimanjaro. Tukumbuke kuwa yeye ni mbunge wa jimbo hilo hadi sasa na sijaambiwa ikiwa hatagombea na mara nyingi ameonekana akizidi kujiimarisha mno kisiasa katika jimbo hilo. Nadhani atakuwa na fursa ya kugombea kipindi kingine, ikiwa hatagombea urais.

Pili, nadhani Mbowe atakuwa na kazi ya kuendelea kuijenga Chadema. Ni mwenyekiti wa chama kwa sasa na nadhani bado anaweza kugombea tena uenyekiti kwa sababu kwa siasa za Afrika kugombea uongozi mara nyingi ni utamaduni wa kawaida na unatokana na sababu ya watu madhubuti kuendelea kuhitajika katika taasisi ili ziwe imara zaidi kabla ya kuwaachia wengine.

Mwisho ni kuendelea na biashara. Mbowe ni mfanyabiashara na anamiliki miradi na kampuni kadhaa. Ikiwa hatagombea urais na labda kuipata nafasi hiyo, naona akiwa na muda mzuri wa kuendelea na usimamizi wa biashara zake.

Hitimisho

Mbowe ni mmoja wa viongozi watakaokumbukwa kama vinara wa mageuzi na demokrasia ya vyama vingi katika nchi. Kiongozi huyu amesimamia mbadiliko mengi ya kidemokrasia ndani ya nchi na ameshiriki kwa vitendo. Naamini bado anapaswa kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa kama letu ambalo ndiyo kwanza linajikongoja kuelekea kwenye maendeleo. Sehemu kubwa ya masuala anayoyasimamia yana tija kubwa na huwezi kuyabeza kirahisi. Namtakia kila la heri katika harakati za kuitafuta Tanzania ambayo inasubiriwa na wengi.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.