Azory, Ben maswali mengi lakini majibu bado hakuna

Muktasari:

Watanzania walio wengi wanajiuliza, kwa nini miaka ya karibuni watu wenye majukumu fulani kwenye jamii wamekuwa wakitoweka katika mazingira ya kutatanisha? Watekaji ni kina nani, kwa nini wanateka, wanafanya kazi kwa kutumwa na nani? Wana ajenda gani? Kesho watamteka nani? Hawa watekaji wana nguvu kuliko vyombo vya ulinzi na usalama? Maswali ni mengi mno!

Inafahamika vizuri kuwa, mwandishi wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda alichukuliwa Novemba 21, 2017 na Ben Saanane, kada wa Chadema na msaidizi wa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, aliyepotea Novemba 18, 2016 hadi sasa hajulikani alipo.

Watanzania walio wengi wanajiuliza, kwa nini miaka ya karibuni watu wenye majukumu fulani kwenye jamii wamekuwa wakitoweka katika mazingira ya kutatanisha? Watekaji ni kina nani, kwa nini wanateka, wanafanya kazi kwa kutumwa na nani? Wana ajenda gani? Kesho watamteka nani? Hawa watekaji wana nguvu kuliko vyombo vya ulinzi na usalama? Maswali ni mengi mno!

Mkiru

Nimetumia neno Mkiru kufupisha maneno (Mkuranga, Kibiti na Rufiji). Mwaka 2017, kulizuka mauaji ya kutisha kwenye ukanda wa wilaya hizo mkoani Pwani. Takribani viongozi 17 wa CCM waliuawa kikatili, polisi kadhaa walivamiwa na baadhi kuuawa. Hali ile ilikuwa mbaya mno.

Katikati ya mauaji yale, wadau wa siasa, taasisi za kidini na za kiraia na wananchi wa kawaida walipaza sauti wakitaka suala hilo lifuatiliwe kwa ukaribu. Baadhi ya wabunge wa CCM na upinzani walitaka Bunge liletewe ripoti ya mauaji hayo. Hadi leo, Bunge halijapewa ripoti na raia wote nchi nzima hawaambiwi nini kilitokea.

Mara kadhaa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wamesimama hadharani na kutangaza kuwa wamedhibiti hali ya usalama kwenye maeneo hayo, lakini maswali ya msingi ya wananchi yanabakia palepale, nani walikuwa ni wauaji? Walikuwa na ajenda gani? Walitumwa na nani? Wauaji wale walikamatwa? Walifikishwa kwenye mahakama zipi?

Hadi sasa kuna kesi ngapi zinazoendelea? Maswali yote haya hayana majibu. Tumekuwa taifa ambalo linakalia mambo makubwa mno. Dola yetu inaamini kuwa ina hatimiliki ya taarifa, hata zinazohusu masuala yaliyotokea hadharani – maana, watu wakishauawa hakuna siri tena, kinachofuata ni wauaji kutafutwa na taifa kujulishwa waliua kwa nini? Je, ni magaidi? Je, wameua kwa sababu za kisiasa, kidini, kikabila, kisasi?

Sandarusi

Sandarusi limekuwa neno maarufu hivi karibuni, likihusishwa na hali ya watu kuuawa na miili yao kutupwa baharini ikiwa ndani ya mifuko ya plastiki au mifuko mingine ambayo hujulikana kama “sandarusi.” Vyombo vyetu vya dola vilitoa maelezo kuwa wale ambao miili yao inakutwa baharini au kwenye fukwe za bahari ni wahamiaji haramu. Jibu hili halitoi mwanga wowote kwa jamii ya Watanzania ambao wameingiwa na hofu kubwa kutokana na mwonekano wa miili hiyo.

Kwa kawaida miili hiyo ama hukutwa kwenye mifuko ya sandarusi, au imefungwa kamba, au ina majeraha makubwa au imefungwa mawe. Wananchi walipodai uchunguzi wa wazi zaidi ukihusisha madaktari bingwa na watu huru, Serikali ikakataa. Bunge lilipotaka kujadili masuala hayo kwa kina, nafasi haikuwepo! Wananchi wamebaki na maswali mengi kuliko majibu.

Mauaji

Februari 1, 2016, Diwani wa kata ya Kimwani iliyoko Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Silvester Miga (CUF) aliuawa kikatili kwa mapanga. Mtuhumiwa wa mauaji hayo hadi sasa hajafikishwa kwenye vyombo vya dola.

Septemba 28, 2017, Kaimu Mwenyekiti wa CUF Jimbo la Mto Pepo, Zanzibar, Ali Juma Suleiman aliuawa kikatili na kikosi maarufu cha wahuni kijulikanacho kama ‘Mazombi’, kikosi hicho kila mara huwalenga wanachama wa chama kimoja cha siasa Zanzibar. Hadi leo, wahusika hawakuwahi kuchukuliwa hatua.

Novemba 14, 2015, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo aliuawa kikatili kwa kukatwakatwa na silaha zenye ncha kali. Ushahidi unaonesha kuwa waliomshambulia ni vijana wanaofahamika kwa majina na sura lakini hawajawahi kukamatwa wala kuchukuliwa hatua.

Februari 12, 2018, Kada na kiongozi wa Chadema Kata ya Hananasifu Jimbo la Kinondoni, Daniel John, alitekwa, kesho yake mwili wake uliokotwa katika ufukwe wa Coco ulioko jijini Dar es Salaam ukiwa na majeraha makubwa. Hadi sasa polisi wanaendelea na uchunguzi kama ilivyo kule Ifakara alikouawa diwani wa kata ya Namawala (Chadema), Godfrey Luena Februari 22, 2018 kwa kukatwa mapanga mwili mzima.

Pia Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Akwilina Akwilin, aliuawa kwa kudunguliwa na risasi Februari 16, 2018 wakati akiwa kwenye daladala akienda kwenye majukumu yake wakati polisi wakitawanya maandamano ya Chadema.

Kuuawa kwa Akwilina, ni mfano tu wa mauaji mabaya ambayo yamewahi kufanywa na polisi, ikiwa ni mwendelezo wa udhaifu wao wa kutumia nguvu kupita kiasi hata katika masuala ambayo kulihitajika busara au nguvu za kadri.

Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum, Lazaro Mambosasa, alieleza askari wote waliofyatua risasi zile wamekamatwa. Mpaka sasa polisi wanaendelea kumsaka muuaji wa Akwilina.

Jaribio la kumuua Lissu

Septemba 7 mwaka jana, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi takribani 38 na zaidi ya risasi 10 zikampata na kumdhuru vibaya. Hadi tuzungumzavyo, waliojaribu kumuua Lissu kikatili, hawajakamatwa na polisi mara kadhaa imeeleza kuwa wanamsubiria dereva wa Lissu na Lissu mwenyewe ili iwahoji na kupata mwanga wa tukio zima lilivyokuwa.

Jambo la kushangaza ni kuwa, hata wananchi walipojumuika kwenye hospitali mbalimbali kutoa damu kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wa hospitali hizo ikiwa ni ishara ya kumwagika kwa damu ya Lissu, zoezi hilo lilipigwa marufuku.

Bunge lilipotaka kujadili jambo hilo, likakatazwa. Unaweza kujiuliza kirahisi sana, kwa nini mambo yote haya yanatokea? Kwa nini jaribio la kumuua Lissu halitolewi majibu? Kwa nini waliojaribu kumuua Lissu hawakamatwi? Kwa nini habari za jaribio la kumuua Lissu hazijadiliwi kwa uwazi kwenye vyombo vinavyowawakilisha wananchi kama Bunge? Maswali juu ya maswali na hakuna majibu.

Jukumu la wote

Ni wazi kwamba hali ya usalama katika nchi yetu imo kwenye shaka kubwa, hatumo vitani wala kwenye hali ya hatari, lakini ni wazi kuwa hatuko salama. Moja ya majukumu makubwa ya kila Mtanzania ni kulinda usalama wa nchi yake ikiwa ni pamoja na kuvikumbusha vyombo vya usalama kila vitakapofanya vibaya katika kazi zao za kulinda usalama wa raia.

Kama watu wanauawa namna hii na hakuna majibu sahihi, watu wanapotea namna hii na hakuna majibu, Watanzania wote wanayo haki ya kuungana na kupiga kelele kwa njia ya amani na njia za kikatiba. Kupotea kwa Azory hakuna maana ya kuwaachia gazeti la Mwananchi kazi ya kumpigania, kupotea kwa Ben hakuna maana ni jukumu la Chadema kumpigania – hili ni jukumu la kila mmoja wetu.

Katika hali za namna hii lazima kelele za maaskofu, mashehe, wachungaji, wanaharakati, taasisi za ndani na nje ya nchi, wawakilishi, wabunge, na mabalozi waendelee kukemea hali hii na kupiga kelele, kelele zipigwe mchana, usiku na asubuhi.

Lazima kuwe na mjadala mkubwa sana wa kitaifa juu ya haki ya kuishi kwenye nchi yetu ili kuvibana vyombo vya ulinzi na usalama vichukue hatua kali kuwasaka na kuwakamata watekaji na wauaji wote bila kujali wanatumwa na nani, yuko wapi, ana uwezo gani, ana fedha ngapi na anatumwa na nani. Maana, haki ya kuishi inapochezewa, haki zingine zote zinakuwa zimepotezwa.

Wajibu wa wananchi

Watanzania wote wana jukumu la kulinda usalama wa taifa hili. Na Watanzania wote wanawajibika kupiga kelele ambazo zitasikika masikioni mwa Serikali na vyombo vyake, kwamba mauaji na utekaji vimetuchosha, vinatunyong’esha na vinatuumiza.

Wananchi wasije kujidanganya kuwa wanaopaswa kuhoji mauaji na utekaji ni wanasiasa – kwa sababu, wauaji na watekaji hao wakiachwa waendelee, hali ya utekaji na mauaji itahamia kwa raia wa kawaida na mara nyingi tumewahi kuona hilo.

Huko nyuma, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere amewahi kusema na kusisitiza kuwa kama kuna mtu anakunywa damu ya watu mahali, mtu huyo ataendelea kunywa tu. Njia ya kipekee ya kumzuia asiendelee kunywa ni kumbaini na kumchukulia hatua kali.

Wananchi watambue kuwa jukumu lao kubwa kuliko yote ni kulinda haki zao za msingi na kuhakikisha maslahi yao hayachezewi. Watanzania wote waendelee kupiga kelele, usiku na mchana hadi siku tutaona hakuna mtu mmoja tena anatekwa, hakuna mtu anauawa, hakuna raia anauawa kwa sababu ya nguvu za polisi za kupitiliza.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])