Doreen Noni; Aukimbia msongo wa mawazo, ashinda mamilioni

Wakati mwingine unaweza kujiuliza kwanini baadhi ya watu hufanya mambo yanayohatarisha afya zao hasa unywaji wa pombe kupindukia na kujitenga mbali na jamii inayowazunguka.

Pia, unaweza kukutana na mtu barabarani anazungumza peke yake au amekaa sehemu kajiinamia huku akionekana mwenye mawazo mengi.

Wengi wao hukosa watu wa kuwashauri kwa kuogopa kuchekwa au kusemwa vibaya na jamii bila kujua kama wanahatarisha afya zao na kukaribisha magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, vijana wenye miaka 15 hadi 30 ndiyo wanaathirika zaidi na msongo wa mawazo na wengine hufikia hatua ya kujiua.

Doreen Noni ni miongoni mwa vijana waliokumbwa na msongo wa mawazo, lakini aliweza kuukabili baada kuzungumza matatizo yake kwa wengine, hivyo kuwa tiba kwake.

Baada ya hali yake kurejea kawaida, alifikiria namna nzuri anayoweza kuwasaidia vijana kuondokana na hali hiyo kwa njia rahisi na kuwafanya warudi katika hali zao za kawaida.

Noni anasema, “nilipitia changamoto hii (msongo wa mawazo), lakini nilipokutana na wenzangu na kuzungumza nao nikaona ni jambo la kawaida

“Kilichonisaidia ni kuzungumza na vijana walionipa uzoefu wa namna walivyokabiliana na changamoto za maisha. Nilichokigundua vijana wengi wanapenda kusikia hadithi za wenzao ili wavutiwe zaidi.”

Noni amepitia katika kipindi cha msongo wa mawazo hasa baada ya baba yake kupelekwa mahabusu kwa mwaka mmoja na miezi minne sasa.

Baba yake, Peter Noni ambaye ni mfanyabiashara na mkurugenzi wa Kampuni ya Six Telecoms na wanzake wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya utakatishaji fedha, matukio wanayodaiwa kuyafanya kati ya mwaka 2014 na 2016.

“Baada ya baba yangu kuwekwa mahabusu Gereza la Keko, nilipitia kipindi kigumu sana mimi na familia yangu, hasa mama yangu.

“Lakini baada ya kuzungumza na vijana wenzangu na kubadilishana nao mawazo, nikaanza kuondokana na hali hii na ilifika kipindi nikienda kufanya maombi kanisani,” anasema Noni ambaye kupitia kipindi cha Peter’s Daughter anachotarajia kukianzisha na kurusha matangazo yake katika runinga, ameahidi kusaidia vijana wenye matatizo hayo.

Noni anaamini itakuwa ni namna bora ya kuwafikia vijana waliokata tamaa kama ilivyokuwa kwake.

Kipindi hicho kitakuwa na maudhui ya kukutanisha vijana kujadiliana namna ya kuwasaidia wenzao walioka tamaa za maisha na wanaokabiliwa na msongo wa mawazo.

Anasema msongo wa mawazo umekuwa ni tatizo kubwa siyo tu kwa vijana wa Kitanzania bali watu wengi duniani.

“Ninachojua mimi kadri unavyozidi kuongea na watu na kubadilisha nao mawazo na kuona watu wanavyopata tiba na hatimaye kupona, ndivyo utakavyowasaidia wengine wenye msongo wa mawazo kupata ahueni. Pia, utasaidia kujua dalili za msongo wa mawazo ambao ni ugonjwa kama ilivyo malaria na unatibika.

“Nataka nizungumze na vijana wenzangu ili kuweka uwelewa kwa jamii kuhusu msongo wa mawazo. Kwa Afrika mtu akisema ana msongo wa mawazo, unachekwa au unaambiwa ni ugonjwa wa Kizungu, hali inayosababisha baadhi yao kuanza kunywa pombe ili kupunguza mawazo au wengine kujiua,” anasema Noni.

Pia, anasema kipindi hicho pia kitakuwa msaada kwa vijana watakaojadiliana kuhusu hali wanazopitia na namna ya kupambana nazo ili kuepuka msongo wa mawazo.

Noni anasema atakaa pamoja na Serikali kuangalia namna ya kuwezesha na kuhamasisha masuala ya huduma ya ushauri ili mtu akitokea anataka kupata tiba asichekwe.

“Haya matatizo (msongo wa mawazo) yapo kila mahali sehemu za kazini, vyuoni na shuleni hadi katika familia. Afrika na Tanzania, kuna baadhi ya vijana wamekata tamaa wanaona mazingira wanayoishi kama wamezaliwa kwenye hali ya umaskini, hawezi kuendelea jambo ambalo si la kweli.

Anasema kuna baadhi ya vijana wanaamini kuwa hawezi kuendelea kimaisha kutokana na changamoto zinazowakabili katika mazingira wanayoishi.

“Nataka wajue hawapo peke yao, wanaokumbana na changamoto hizi. Ni lazima vijana tuambizane ukweli ili tusaidiane katika kuiletea maendeleo nchi, ndiyo maana nimeanzisha kipindi hiki,”anasema Noni aliyezawadiwa hundi ya Sh30 milioni baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika shindano la linalowalenga vijana wenye mawazo mbadala ya biashara na miradi inayoweza kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii linaloitwa “Startupper of the Year Challenge.”

Shindano hilo liliandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Total na kushirikisha washirikia 800.

Mkurugenzi Mtendaji wa Total, Tarik Moufaddal anasema shindano la kwanza lilifanyika mwaka 2015 na mchakato huo unazingatia wazo la ubunifu na umuhimu wa mradi huo kwa jamii.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde ndiye aliyemkadhi Noni hundi ya Sh30 milioni baada ya kuibuka mshindi.

Mbali na kitita hicho, Noni atapelekwa Ufaransa kati ya Aprili 15 hadi 19 kwa ajili ya kujifunza masuala ya ujasiriamali.