Hedhi nyingi kuliko kawaida

Tafiti mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa kila wanawake watano mmoja huwa na tatizo la kupata damu ya hedhi nyingi kupita kiwango cha kawaida.

Wanawake wanaokumbwa na tatizo hili huweza kubadili pedi kila baada ya saa moja ukilinganisha na mwenye hedhi ya kawaida huweza kubadili mara 3-4 kwa siku.

Damu ya hedhi inayotoka huwa ni mara 10-25 zaidi ya kile kiwango cha kawaida ambacho huwa ni sawa na vijiko vitano kwa mzunguko mmoja.

Tatizo la kupata hedhi nyingi kupita kiasi linaweza kuambatana na utokaji wa hedhi hiyo kwa muda mrefu na huku pia kukiwa na mzunguko wa hedhi unao badilika badilika.

Mwanamke mwenye tatizo hili hujikita kukabiliana na tatizo hilo badala ya kufanya shughuli za kumwingizia kipato, mfano hubaki nyumbani kwa kuhofia hali ya usafi wa mwili akiwa maeneo ya kazi.

Waathirika wa tatizo hili mara kwa mara ni wasichana waliovunja ungo na wanawake ambao wako mwishoni mwa umri wa miaka 40 na mwanzoni mwa umri wa miaka 50, yaani ambao wako karibu kufikia ukomo wa hedhi.

Zipo sababu mbalimbali za wanawake kupata tatizo hili ikiwamo kukosekana usawa wa vichochezi (hormones), hitilafu za kimaumbile katika nyumba ya uzazi ikiwamo kuwapo kwa uvimbe wa fibroid au polyps na matatizo ya kiafya ndani ya mwili.

Matatizo katika vichochezi ndiyo mara kwa mara yanayochangia kutokea kwa hali hii, inaweza kutokea mwili ukatengeneza kiwango kikubwa au kidogo cha vichochezi vya estrogen na progestrone (vichochezi vya uzazi wa kike).

Mfano ni kwa wanawake wengi wenye tatizo la kupata hedhi kwa wingi huwa pia na tatizo la kutopevusha kijiyai cha kike kutokana na hitilafu ya mzunguko wa hedhi unaochangiwa na vichochezi kutowiana.

Vile vile matatizo ya tezi ya shingo, hitilafu katika chembe za damu zinazogandisha na kuzui damu kutoka, upungufu wa chembe hai sahani, magonjwa ya figo na ini na saratani ya damu.

Yapo pia magonjwa ya wanawake yanayoweza kuchangia hali hiyo ikiwamo uvimbe wa fibroid, mimba kuharibika, mimba kutunga nje ya nyumba ya uzazi.