MAONI: Mawazo yako mtaji wako katika chombo cha habari

Monday January 13 2020Ndimara Tegambwage ni  Mhariri Meza ya wa Jamii

Ndimara Tegambwage ni  Mhariri Meza ya wa Jamii 

Mwaka mpya–2020 unakuja vingine. Tayari Mhariri wa Jamii anapatikana kwa wepesi zaidi. Awali alikuwa anapatikana kwa simu na baruapepe. Sasa anapatikana pia kiganjani mwako kwa njia ya twitter. Heri ya Mwaka Mpya kwa wasomaji wote wa safu hii.

Ni fursa nyingine kukumbushana jukumu la Mhariri wa Jamii wa MCL – Mwananchi Communications Limited – wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na machapisho yake mengine katika mitandao ya kijamii.

Jukumu hilo ni kupokea maoni yako kwa njia ya barua, barua pepe, simu au twitter; kuzungumza nawe, kufanya utafiti juu ya maoni hasa yanapokuwa malalamiko au ushauri; na hatimaye kurejea kwako na majibu ili kukata kiu yako.

Sasa wasomaji wataweza kupata baadhi ya majibu kwa maswali au hoja zao kwa haraka zaidi; tuseme, hasa kwa wale watakaokuwa wameuliza kwa njia ya simu au twitter. Kwa kukumbushana, ni hoja na maswali juu ya utendaji wa kampuni, habari zilizochapishwa na chochote ulichoona – kosa, utamu, “wingi wa chumvi” au ukakasi na chochote unachotamani.

Kuna yale ambayo hukuyaona katika vyombo vya habari vya MCL; labda umeyasoma kwingine au umeyasikia mitaani. Kwa kuwa wewe unaamini hivi ndivyo vyombo ambavyo hukupa kilicho kweli na sahihi, sasa uliza: kwanini vimeyasusa, vimeyadharau, vimeyasahau, vimeyapuuza au havikuyaona. Weka maoni yako.

Meza ya Mhariri wa Jamii haihudumii mtu binafsi peke yake bali hata vikundi, asasi, kampuni, mashirika, vyama vya siasa na serikali. Kama kuna yeyote mwenye swali, malalamiko au anayetaka ufafanuzi, basi hapa ndipo pa kupata majibu.

Advertisement

Kuna fursa nyingine kutoka meza hii. Anayeona, kwa taarifa au habari iliyochapishwa, kwamba kuna hitilafu – iwe katika maadili, lugha, usahihi – au anaona hakutendewa haki kwa kutajwa hapa au pale; au kwa kutotajwa, aweza kuwasilisha mara moja maelezo mapana, siyo kwa mashtaka au malumbano bali kwa kuweka usahihi wa jambo lenyewe.

Utaratibu ulioelezwa hapo juu unalenga kufafanua dhana kwamba wasomaji, watazamaji na wasikilizaji wa taarifa na habari ni sehemu ya wamiliki wa vyombo vya habari. Umiliki huu ni kwa njia ya kutoa maoni yao na kwa kusikilizwa ili wanachotaka, wanachopenda – lakini kile kilichosahihi na kinachoendana na misingi ya uandishi wa habari – kinafuatiliwa; na inapobidi kinatekelezwa.

Kwahiyo, wanapotoa maoni, na maoni hayo kuchapishwa, wanakuwa wameshiriki kuandaa taarifa na habari. Wanakuwa sehemu ya wale waliomo katika mchakato wa kukusanya, kuchakata taarifa, kuandika na kuchapisha/kutangaza habari.

Pale ambapo wanashiriki kukosoa, kuibua mijadala au kuweka nyongeza kutokana na kile kilichochapishwa, basi wanakuwa pia wamechangia uwezekano wa kuongeza thamani ya taarifa na habari zitakazotoka baadaye. Aidha, wanakuwa wamejitambulisha kuwa ni vyanzo muhimu vya mawazo rutubishi.

Kuna wakati wasomaji, watazamaji na wasikilizaji wanaweza kuhoji: hili mbona hamliandiki, mbona hamlitilii mkazo au hamjawahi kuliandika. Maoni ya aina hiyo yanalenga kuonyesha kuwa wadau wanataja vitu ambavyo wanataka kusikia, kujua taarifa zake au hawataki kabisa. Mara nyingi wanataka ufumbuzi wa changamoto na siyo orodha ya zilizoshindikana.

Maoni ya wadau basi, katika kumiliki vyombo vya habari yana nafasi ya kuchangia msukumo wa kutafuta, kutafiti, kuchakata taarifa zinazorandana na matakwa, matarajio na nafuu kwao.

Hili ndilo linafanya wachapishaji wengi wakubwa duniani hivi sasa, kuruhusu mfumo wa maripota wao kujenga ukaribu na vikundi vya kijamii, shule na taasisi kwa shabaha ya kuchuma mwelekeo wa mawazo yao na hatimaye kuwapelekea taarifa na habari zinazoshabihiana na wanachokihitaji; na kuendelea kuwa na uhakika wa soko.

Kuna jambo moja ambalo Meza ya Mhariri wa Jamii ilikuwa haijafafanua. Vikundi, asasi, kampuni, mashirika, vyama vya siasa na hata serikali, wanaweza kumwalika Mhariri wa Jamii kwa ushauri, ufafanuzi wa kazi yake na majibu kwa maswali na hoja zao.

Shule, vyuo na taasisi zaweza kumwalika Mhariri wa Jamii, siyo tu kumwonyesha makosa, kumsomea malalamiko yatokanayo na kilichochapishwa na vyombo vyake vya habari; bali hata kuvuna kutoka kwake maarifa ya nyongeza juu ya kazi yake na mwenendo wa vyombo vya habari.

Kwa kuwa kazi nyingine muhimu ya Mhariri wa Jamii ni kufuatilia mwenendo wa kazi kitaaluma; na kwa kuwa taaluma ndiyo inaakisi ubora wa kazi yenyewe; vyuo hasa vya habari vinaweza kufuatilia mwenendo wa vyombo vyetu vya habari na hatimaye kumwalika Mhariri wa Jamii kushiriki mijadala na kujibu hoja zao.

Usikubali kuumia kwa msongo wa maswali na malalamiko. Uliza. Tunachojua tutakwambia. Tusichojua tutatafuta ili tukwambie. Tulichoshindwa kupata tutakwambia. Kilichotukwaza tutakwambia pia. Karibu kwenye Meza ya Mhariri wa Jamii.

Mhariri wa Jamii anapatikana kwa Simu: 0763670229/0713614872