Mbu wote wanaambukiza matende, mabusha

Watu ambao wanaugua ugonjwa wa matende wakiwa katika moja ya hospitali nchini.Picha na Maktaba.

Muktasari:

  • Kulingana na mabadiliko ya kimazingira, hata Anopheles naye huambukiza magonjwa  ya matende na mabusha., hali inayoweka wasiwasi zaidi.

Ni wadudu wachache duniani wenye kujiamini kiasi cha kupenya katika makazi ya mwanadamu na kutawala kiasi ambacho mbu hutawala.

Mdudu huyu, anaweza kupenya popote, sebuleni, jikoni, bafuni au hata uvunguni mwa kitanda na akafanya atakacho, akamuuma binadamu mahali popote mwilini.

Ana uwezo wa kuingia chumbani na kelele za mabawa yake zikamwamsha mwanadamu aliyepumzika baada ya kazi za kutwa nzima. Licha ya kero za muwasho wake anapokung’ata na kelele, lakini mdudu huyu anaambukiza magonjwa  kadhaa  yanayosababisha kifo, kubwa likiwa ni malaria.

Hapo zamani, ilidhaniwa kuwa mbu aina ya culex pekee ndiye anaambukiza ugonjwa wa matende.

Hata hivyo tafiti zilizofanyika hivi karibuni zimebaini kuwa, hata mbu jike aina ya anopheles, anayefahamika kwa kuambukiza ugonjwa wa malaria, sasa anaweza kuambukiza ugonjwa wa matende kutokana na mazingira hatarishi ambayo wengi tumeendelea kuishi.

Matende na mabusha ni magonjwa yasiyopewa kipaumbele ingawa  yana athari kubwa kwa maisha ya watanzania ambapo asilimia moja hadi 69 ya watu  wamo hatarini kupata ugonjwa huo.

Mratibu wa Mradi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele, (NTDPC) (matende na mabusha) kutoka Taasisi ya Utafiti wa Tiba Nchini, (NIMR) Dk Upendo Mwingira, anasema mbu aina ya Anopheles ambaye zamani aliambukiza zaidi Malaria, sasa anaambukiza pia ugonjwa wa matende ambao zamani uliambukizwa zaidi na mbu aina ya culex.

Dk Mwingira anasema mbu anayeambukiza malaria anaweza kuambukiza matende kwa sababu maradhi hayo yanaambukizwa kwa minyoo midogo midogo iliyoko kwenye mfumo wa majimaji na damu.

Anasema zipo dhana mbalimbali kuhusu ugonjwa wa matende   na mabusha ambapo baadhi ya watu wanadai unasababishwa na unywaji wa maji ya madafu.

“Dhana hizi si za kweli, matende  na mabusha hayasababishwi na maji ya madafu bali mbu aina ya culex na sasa hali ni ya hatari zaidi kwani anopheles naye anausambaza,” anasema Dk Mwingira.  Baadhi wanadai kuwa matende huwapata watu waishio ukanda wa pwani tu lakini kwa hali iliyopo hata wale wa bara nao wapo hatarini kupata maradhi hayo wasipowadhibiti mbu.

“Watu bilioni moja wapo hatarini kupata ugonjwa wa matende iwapo hatua hazitachukuliwa,” anasema Dk Mwingira

Maradhi yasababishwayo na mbu husababisha vifo vya mamilioni ya watu ulimwenguni kila mwaka na kuwaathiri zaidi watoto na watu wazima katika nchi zilizoendelea.

Zipo aina zaidi ya 3,000 za mbu, lakini wanachama watatu wanasifika kwa kusababisha maradhi kwa binadamu.

Yupo mbu aina ya Anopheles, ambaye anabeba vimelea vya ugonjwa malaria, na hivi sasa anaambukiza pia matende.

Culex, yeye anaambukiza zaidi ugonjwa wa matende, mabusha na virusi vya West Nile. Lakini pia yupo mbu aina ya Aedes, ambaye anapatikana zaidi katika bara la Asia, huyu, huambukiza ugonjwa wa Homa ya Manjano na Dengue pamoja na Ensephenecalitis.

 Matende

Ugonjwa wa matende hujitokeza kwa uvimbe katika maeneo ya miguuni au kichwani. Uvimbe huu husababishwa na kujikusanya kwa maji kusiko kawaida katika tishu.

Ngozi kwa kawaida huwa nyepesi na baadaye hubadilika kuwa nyeusi. Mgonjwa huwa na homa, kuhisi baridi na maumivu makali.

Mabusha

Mabusha huweza kuathiri sehemu za siri za kike au za kiume. Kwa wanaume, korodani huweza kuvimba na kujaa maji.

Kwa wanawake, sehemu za kike (vulva), kwa nje huvimba na kuunda mitoki katika viungio vya miguu

Tatizo la mabusha  limekuwa likichukuliwa na baadhi ya watu kuwa ni hali ya kudhalilisha ingawa kwa wengine huonekana ni hali ya kuwa ‘mzee wa heshima’ au ‘umwinyi’.

Hata hivyo ni tatizo lenye madhara kiafya endapo halitachukuliwa hatua za haraka.

Mtandao wa madaktari Tanzania (TanzMed) unaeleza kuwa mabusha hayana dalili zozote.

Hata hivyo, baada ya muda fulani,  korodani hujaa na uvimbe huweza kuonekana hata kwa nje. Kwa kadiri uvimbe unavyozidi kuongezeka, dalili zifuatazo zaweza kujitokeza pia;

Muhusika kujihisi hali ya uzito na kuvuta sehemu za siri kutokana na kujaa na kuongezeka kwa uzito wa  korodani.

Mgonjwa huweza kujihisi hali ya usumbufu na kutokujisikia vizuri maeneo ya kinena mpaka mgongoni.

Kwa kawaida mabusha hayana maumivu yeyote. Hata hivyo, iwapo mgonjwa ataanza kujihisi maumivu, hiyo ni dalili ya kuwepo kwa uambukizi katika mshipa wa epididymisi.

Uvimbe huwa na tabia ya kupungua iwapo mgonjwa atakaa kitako na huongezeka pindi anaposimama.

Iwapo mgonjwa atajisikia homa, kichefuchefu na kutapika, hizo ni dalili za kuwepo kwa uambukizi katika mabusha.

Kwa kawaida mabusha hayana muingiliano na uwezo na ufanisi wa utendaji wa ngono.

Hata hivyo kuna taarifa tofauti za kitafiti kutoka Bara Asia na Afrika Magharibi kuwa mabusha yanaweza kuathiri ufanisi wa tendo la ngono na kwa kiasi fulani kusababisha mhemko au msongo wa mawazo kwa mwathirika.

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti, NIMR, Dk Julius Massaga anasema si kwamba mbu aina ya Anopheles hakuwa akiambukiza matende bali hivi sasa ana hatari ya kuambukiza zaidi kwa kuzoa vimelea kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

 “Culex, ndiye mwenye kuambukiza zaidi matende, anopheles pia alikuwa anaambukiza lakini kwa kiasi kidogo kuliko hivi sasa,” anasema Dk Massaga,

 Kwa maana nyingine, watu wengi zaidi wapo hatarini kuambukizwa ugonjwa matende kuliko zamani endapo hawatapata dawa za kuzuia matende na mabusha.

Juni, 22 mwaka huu, Kitengo cha Magonjwa yasiyopewa kipaumbele cha NIMR, kitafanya kampeni ya kugawa dawa za kuzuia matende na mabusha bure kwa wakazi wa Dar es Salaam na Mwanza.