Aussems aifungia kazi TP Mazembe

Friday March 22 2019

 

By THOBIAS SEBASTIAN

ACHANA na mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi Uganda ‘The Cranes’ ambayo itachezwa Jumapili ya Machi 24, wawakilishi wa Tanzania Simba watakuwa na mechi ngumu ya robo fainali dhidi ya TP Mazembe, Aprili 6, katika Uwanja wa Taifa.

Simba ilifuzu hatua hiyo kutokana na pointi tisa ilizozipata katika Kundi D lililoongozwa na Al Ahly iliyofikisha pointi 10.

Wachezaji wa Simba wasiokuwa kwenye majukumu Stars wamepewa mapumziko ya siku tano baada ya kupata ushindi katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting na Jumatatu asubuhi wataanza mazoezi na maandalizi dhidi ya TP Mazembe.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema itakuwa mechi ngumu kuliko zile za awali kulingana na ubora wa TP Mazembe.

Aussems alisema Mazembe ina wachezaji wazoefu kwenye mashindano haya kwani wamecheza mara kwa mara na hata msimu uliopita waliishia hatua hii.

Alisema: “Tunafahamu ubora wa Mazembe na tufanya maandalizi kulingana na wapinzani walivyo katika ubora na udhaifu wao.

Advertisement

“Mechi ya kwanza tutacheza nyumbani na tunafahamu nguvu na hamasa tunayoipata kutoka kwa mashabiki wetu tangu tumeanza mashindano haya, tunaomba mashabiki waendelea kujitokeza kwa wingi kutupa nguvu ili kutimiza malengo ya kupata ushindi,” alisema Aussems

Kiungo mkabaji wa Simba, James Kotei alisema hatua waliyofikia ilikuwa ni lazima wakutane na timu kubwa katika mashindano hayo kama Mazembe.

“Ili kuwa bingwa lazima uwafunge mabingwa kama Mazembe, itakuwa mechi ngumu ambayo kwetu tutaifanyia maandalizi ya kutosha kuona tunapata matokeo mazuri dhidi yao hapa nyumbani,” alisema Kotei.

MSIKIE MGOSI

Simba mara ya mwisho ilicheza na Mazembe katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa mwaka 2011, hatua ya pili ambayo ilikuwa inatoa matokeo ya timu itakayokwenda kucheza hatua ya makundi.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam, Simba ilikubali kichapo cha mabao 3-2, kabla ya kwenda Lubumbashi Uwanja wa Stade de la Kenya ambako walipigwa mabao 3-1.

Nahodha aliyekuwa katika kikosi hicho wakati huo Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema Mazembe ambayo ilikuwa wakati wanacheza nayo ni tofauti kabisa na ya wakati huu.

“Simba kwanza watambue wanacheza na timu kubwa yenye kufahamu faida ya mashindano haya lakini hofu yangu kubwa ni wanapocheza ugenini wanapoteza kwa kufungwa mabao mengi ingawaje wao wana uwezo wa kushinda hapa nyumbani.

“Bahati nzuri wataanzia nyumbani jambo ambalo wanatakiwa kushinda kwa mabao mengi ili watakapokwenda ugenini wacheze kwa tahadhari ya kuzuia ili wasifungwe idadi kubwa ya mabao lakini ikiwa tofauti na hapo, huo utakuwa ndio mwisho wa Simba kushiriki michuano ya kimataifa kwa mwaka huu,” alisema nyota huyo wa zamani wa Stars.

Advertisement