Balinya, Kalengo wapigwa marufuku

Muktasari:

  • Mpaka sasa wachezaji wapya wa kigeni waliofika nchini na kujichimbia kambini sambamba na nyota wapya wazawa na wale waliokuwa kwenye kikosi kilichopita ni mabeki Lamine Moro, Mustapha Seleman; washambulaji Maybin Kalengo, Patrick Sibomana, Juma Balinya na Issa Bigirimana.

MPAKA sasa Yanga kambini kwao ina mastaa wanane wa kigeni, lakini benchi lao la ufundi limewapiga marufuku mastaa wake sita wapya ambao wameshafika kazini, lakini hapohapo wakapewa kazi moja kubwa kuthibitisha ubora wao.

Alichosema Kocha Noel Mwandila mbele ya Mwanaspoti ni kwamba, wachezaji wao sita wapya wa kigeni kwa sasa hawataruhusiwa kuongea chochote na vyombo vya habari.

Mwandila alisema mastaa hao kazi yao kubwa kwa sasa ni kujituma mazoezini ambapo kama wakifanya vizuri ndiyo watapewa nafasi hiyo. “Tumezuia hawa wachezaji wapya kuongea hovyo, tunataka kuona wanajikita katika kazi yao, wana kazi kubwa ya kufanya kwanza hamtawaona wanaongea hovyo,” alisema.

Mpaka sasa wachezaji wapya wa kigeni waliofika nchini na kujichimbia kambini sambamba na nyota wapya wazawa na wale waliokuwa kwenye kikosi kilichopita ni mabeki Lamine Moro, Mustapha Seleman; washambulaji Maybin Kalengo, Patrick Sibomana, Juma Balinya na Issa Bigirimana.

Kocha huyo Mzambia mwenye misimamo mikali alisema lengo la kuwazuia wachezaji hao ni kuwataka kujituma mazoezini na kutambulishwa kwanza na kazi yao. “Tunataka wathibitishe ubora wao kwanza uwanjani, sio kuwa maarufu kwa kuongea kwanza, wakifanya kazi vizuri tutawapa nafasi, tumewasajili kwa kuwa tuliridhika na viwango vyao lakini sasa kazi kwanza uwanjani.”

Alisema wachezaji hao wanatakiwa kuthibitisha kwamba Yanga haijakosea kuwasajili kwa kuonyesha uwezo uwanjani na sio kuwa maarufu kupitia vyombo vya habari.

Mwandila alisema zuio hilo pia linawagusa wachezaji wapya wazawa ambao wamesajiliwa msimu huu ambao nao wanatakiwa kuonyesha kwanza kazi uwanjani.