Bocco, Kagere wambadili Kanda

Tuesday September 10 2019

 

By Olipa Assa na Thobias Sebastian [email protected]

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amelazimika kumuandaa winga Deo Kanda kwa kumfanyisha mazoezi maalumu ili aweze kucheza namba ya John Bocco ambaye ni majeruhi au Meddie Kagere katika mchezo wa Ijumaa wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.

Katika mazoezi ya jana ya timu hiyo kwenye uwanja wa Gymkhana, Kanda alijifua na wenzake mazoezi ya viungo na stamina kisha akahamia kwa kocha wa viungo, Aden Zran ambaye alimfanyisha mazoezi ya kukimbia huku wenzake wakiingia kucheza.

Akifafanua sababu ya Kanda kufanya mazoezi binafsi kocha Aussems alisema ni kwa kuwa Bocco hayuko fiti na pia hana uhakika na Kagere ambaye alikuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa kama atarejea akiwa fiti.

“Nahofia kumfanyisha mazoezi magumu Kanda, kabla ya kuwa na uhakika na Kagere ambaye yuko njiani akitokea Rwanda, lazima niwe mwangalifu, Bocco bado hajawa fiti na Kagere sijui yuko vipi, hivyo lazima nichukue tahadhari kwa Kanda ndiyo sababu sitaki afanye mazoezi magumu,” alisema.

Alisema mbali na wachezaji hao, wengine waliosalia wako fiti kwa ajili ya kuikabili Mtibwa ambayo imekuwa ikiwapa shida katika mechi zao.

Advertisement