Chama atoboa siri kipigo cha Al Ahly

Thursday February 14 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kiungo wa Simba Clatous Chama ametoboa siri ya ushindi walioupata dhidu ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Dar es Salaam juzi.

Bao pekee la Meddie Kagere kwenye Uwanja wa Taifa, zilifufua matumaini ya Simba kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Akizungumza jana, Chama alisema baada ya kufungwa mara mbili mabao 5-0 dhidi ya AS Vita na Al Ahly, waliweka mkakati wa kupata pointi tatu katika mchezo wa juzi.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Zambia, alisema baada ya kipigo cha jumla ya mabao 10, walitafakari namna ya kulipa kisasi kwa Al Ahly.

Chama alisema walikuwa wakiumizwa na matokeo hayo kwa kuwa yaliwaweka katika mazingira magumu katika kundi lao la D.

“Kufungwa kwetu kuliongeza morali, kila mmoja aliyepata nafasi alikuwa na shauku ya kutaka kuifanyia jambo Simba, mashabiki wengi waliumizwa na matokeo yetu mabaya,” alisema Chama.

“Navutiwa na uvumilivu wa mashabiki wa Simba ambao pamoja na kutofanya vizuri kwenye michezo hiyo, hawakusita kujitokeza kwa wingi uwanjani kutuunga mkono,” alisema Chama. Simba itarudiana na JS Saoura, Machi 9 kabla kuivaa AS Vita ya DR Congo Machi 16.

Advertisement