Griezmann: Asanteni Atletico Madrid

Madrid, Hispania. Antoine Griezmann ameaga mashabiki wa Atletico Madrid baada ya kuitumikia kwa miaka mitano.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alijiunga na klabu hiyo katika usajili wa msimu 2014 na amefunga mabao 94 katika mechi 174 alizocheza Atletico.

Mshambuliaji huyo anatarajiwa kujiunga na Barcelona kwa ada ya Pauni 104 milioni katika usajili wa majira ya kiangazi.

Barcelona imetaka huduma ya Griezmann kwenda kuimarisha safu yake ya ushambuliaji baada ya kutolewa kwa aibu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Nimezungumza na Cholo (Diego Simeone), pia Miguel Angel na sasa ni zamu ya mashabiki ambao siku zote walikuwa upande wangu, nimefikia uamuzi wa kuondoka kwenda kupata changamoto mpya, asanteni sana,” aliandika Griezmann katika ujumbe wake.

Griezmann alisema anaondoka Atletico akiwa na rekodi ya kuipa mataji kadhaa katika kipindi chote alichokuwa katika klabu hiyo.

Barcelona iliwahi kumtupia ndoano mchezaji huyo majira ya kiangazi msimu uliopita, lakini iligonga mwamba. Griezmann anatarajiwa kucheza mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Levante, Jumamosi wiki hii.

Rais wa Barcelona Josep Bartomeu alisema klabu hiyo inaweza kusajili mchezaji mwenye umri mkubwa wa miaka 27 au 28. Griezmann ana miaka 28.