Kagera Sugar yatangaza vita kwa Njombe Mji

Thursday January 11 2018

 

By Saddam Sadick

Kagera Sugar imesema haitaki mzaha tena na kuweka ahadi ni lazima waifunge Njombe Mji katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ili kujiweka nafasi nzuri katika msimamo.

Kagera Sugar ipo nafasi ya 12 ikiwa pointi 12 inatarajia kujitupa uwanjani Jumatatu ijayo kuwakabili Njombe Mji kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.

Kocha msaidizi wa Kagera Sugar, Ally Jangalu alisema  tayari timu imeshawasili mkoani humo kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa na kwamba lengo kubwa ni kuhitaji pointi tatu.

Alisema kuwa kwa sasa alama walizonazo na nafasi waliyopo haiwaridhishi na kwamba bado wana kazi ngumu kupambana kusaka ushindi,hivyo Njombe ijiandae tu kwa kipondo.

“Tumeshafika Njombe na tunaendelea na maandalizi, tumewahi kuzoea hali ya hewa kutokana na viwanja vya ugenini jinsi vilivyo, lakini kikubwa tunapiga hesabu namna ya kuchomoka na pointi tatu huku,” alisema Jangalu.

Kocha huyo aliongeza kuwa kinachowapa hamasa ni kutokana na wachezaji wote kuwa kwenye ari nzuri na morari ya juu na kwamba hakuna atayekosa mchezo huo.

“Wachezaji wote wapo fiti hakuna mwenye majeruhi yanayoweza kumkosesha mpambano,niwaombe wadau wajitokeze kwa wingi kushuhudia mpira”alisema kocha huyo.

Advertisement