Kaze aanza kwa ushindi, Simba yafa kwa Prisons

Muktasari:

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, mabingwa watetezi Simba walishindwa kutamba mbele ya Tanzania Prisons baada ya kutandikwa bao 1-0 kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Nelsin Mandela mjini Sumbawanga.

Dar es Salaam. Bao pekee lililofungwa na kiungo raia wa Congo dakika 70 limetosha kuipa Yanga ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru, dar es Salaam, jana..

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, mabingwa watetezi Simba walishindwa kutamba mbele ya Tanzania Prisons baada ya kutandikwa bao 1-0 kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Nelsin Mandela mjini Sumbawanga.

Bao la kichwa la Samson Mbangula dakika ya 49 lilitosha kuinyamazisha Simba, ambayo ilikuwa na mabadiliko kikosi, ikiwakosa wafungaji wao, Chris Mugalu, John Bocco na Meddie Kagere.

Yanga ililazimika kusubiri dakika 70 kupata bao hilo mfungaji akifunga kwa shuti la kubabatiza lililobadilishwa uelekeo na beki wa Polisi na kumshinda kipa Manyika Peter.

Kocha Cedric Kaze akiiongoza kwa mara ya kwanza miamba hiyo, alikuwa na wakati wa kuangalia mpangilio wa kikosi chake alichokifanyia mabadiliko kutoka mechi ya zilizopita.

Awali chini ya kocha Zlatko Krmpotic, mshambuliaji wa Ghana, Michael Sarpong alikuwa akianza pamoja na kiungo Zawadi Mauya, ambaye jana aliansihwa Farid Musa na Yacouba Sogne, ambaye alikuwa akitokea benchi.

Kaze pia alikuwa na imani na kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, ambaye alikuwa pia na wakati mgumu chini ya kocha Zlatko, lakini naye alikuwa na nafasi katika timu iliyopangwa jana.

Kipindi cha kwanza, Yanga ilionekana kutawala mchezo lakini kocha wao anatakiwa kufanya kazi ya ziada katika kuwaongezea mbinu washambuliaji wake kuwa makini katika kutumia nafasi wanazotengeneza.

Dakika ya 20 Yanga ilifanya shambulizi kali baada ya kushutukia ugumu wa kuipenya ngome ya Polisi, shuti kali la kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ lilipanguliwa na Manyika na mabeki kuuondoa mpira katika hatari.

Mabadiliko ya Kaze ya kumpumzisha Niyonzima na kumwingiza Ditram Nchimbi yaliongeza nguvu katika kikosi cha Yanga, ambacho pia kilimtumia Sarpong badaye kwenye mchezo huo.

Mkoani Rukwa, hali haikuwa nzuri kwa mabingwa watetezi kutokana na kupoteza pointi tatu za kwanza katika msimu huu.

Kocha Sven Vandebroeck sasa atakuwa amepata jibu la kwanini anatakiwa kuwa na wachezaji wake hatari katika ushambuliaji, Clatous Chama, Kagere, Mugalu na Bocco kutokana na jana kutokuwa na hatari kubwa na kuisumbua safu ya ulinzi ya Prisons.

Simba, ambayo iliwatumia Jonas Mkude na Hassan Dilunga katika eneo la kiungo na Charles Ilanfia na Luis Miquissone, wakati Bernand Morrison na larry Bwalya wakiwa kama viungo wa pembeni.

Lakini ni kama walishindwa kuwa na maelewano vizuri kutokana na kushindwa kutengeneza nafasi za kutosha na mipira mirefu ilishindwa kuwasaidia washambuliaji hao.

Ni wazi kuwa Simba haitakuwa na mpango mwingine zaidi ya kulazimisha kuwa na wachezaji wote hatari katika eneo la ushambuliaji, huku mabadiliko ya lazima ya mapema baada ya kuumia Shomari Kapombe na kuingia kwa Kennedy Juma kuliifanya miamba hiyo kumtumia Erasto Nyoni kwenye upande wa kulia ikiwa inamkosa Pascal Wawa.