Kikapu Arusha yaingia nusu fainali

Muktasari:

Mjumbe wa Kamati ya Mashindano kutoka Chama cha Mpira wa Kikapu mkoani Arusha (ARBA), Barick Kilimba alisema mashindano hayo yaliendeshwa kwa mfumo wa ligi kwa miezi mitatu na timu nne za juu zimetinga nusu fainali.

Arusha. Ligi ya mpira wa kikapu Mkoa wa Arusha imeingia hatua ya nusu fainali ambapo timu nne zitachuana kusaka ubingwa na nafasi ya kwenda kwenye Ligi Kanda ya Kaskazini itakayofanyika mkoani Tanga.

Mjumbe wa Kamati ya Mashindano kutoka Chama cha Mpira wa Kikapu mkoani Arusha (ARBA), Barick Kilimba alisema mashindano hayo yaliendeshwa kwa mfumo wa ligi kwa miezi mitatu na timu nne za juu zimetinga nusu fainali.

Timu ya HOO iliyoongoza ligi hiyo, itavaana na Pallot iliyomaliza nafasi ya nne katika mchezo wa kwanza utakaochezwa Jumamosi huku Kings iliyomaliza nafasi ya pili ikicheza na Hooperz iliyomaliza nafasi ya tatu na zitarudiana Jumapili.

“Kila timu itacheza michezo miwili Jumamosi na Jumapili na timu itakayoshinda michezo yote miwili ndiyo itatinga fainali lakini kama kila mmoja atamfunga mwenzake kwenye hiyo michezo miwili basi tutaongeza mchezo wa tatu na mshindi wa mchezo wa tatu ndiye atacheza fainali,” alisema Kilimba.

Aliongeza kuwa mfumo huo umetokana na mabadiliko ya TBF ambayo wamedhamiria kufanya mabadiliko makubwa kwenye mchezo huo nchini kama wanavyofanya nchi nyingine zilizoendelea kwenye kikapu ulimwenguni.

Hata hivyo aliongeza kuwa bado kuna changamoto ya uwanja kwani uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliokuwa unatumika siku zote umekodishwa na sasa wapo kwenye mazungumzo na viongozi wa Pallot kuomba uwanja wao.

Ligi hiyo ilishirikisha timu 10 za: Scorpion, Kings, Hoopers, Spider, Polisi Morani, MS TDCDC, IAA, Pallot, Ilboru na Makumira.