Kiungo Mbrazil awagawa mastaa Simba

TAARIFA za kiungo Gerson Fraga kuwa miongoni mwa wachezaji walio katika uwezekano wa kupigwa panga dirisha kubwa la usajili la Simba zimepokelewa kwa mtazamo wa tofauti na nyota wa zamani waliowahi kuicheza klabu hiyo.

Mastaa hao wa zamani wa Simba, wamegawanyika katika makundi mawili na wapo wanaounga mkono taarifa za nyota huyo kuachwa na wapo walioshauri aendelee kubakia katika kikosi cha Simba.

Winga wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa ni Kocha Mlage Kabange alisema kiungo huyo ana sifa zote za kuichezea timu hiyo na hadhani ni sahihi kutemwa wakati wa dirisha kubwa la usajili.

“Kwa mtazamo wangu nilikuwa na mashaka sana na ujio wake wakati aliposajiliwa.

“Lakini baada ya yeye mwenyewe kufika akafanya mazoezi na kisha kucheza nadhani hastahili kuachwa kwa sababu ana vitu vingi ambavyo anavitoa ndani ya uwanja ingawa bahati mbaya tu hapati nafasi kikosini.

Nafasi anayocheza ndio ambayo amekuwa akipangwa Jonas Mkude. Lakini ukiwalinganisha hao wawili, Mkude si aina ya mchezaji wa ukabaji kulinganisha na yeye. Pia Fraga anafunga, anakaba na anachezesha timu.

Kuhusu kupata nafasi inategemea na mifumo na mipango ya kocha. Lakini kama mnavyoona kila anavyopata nafasi amekuwa akifanya vizuri,” alisema Kabange.

Mtazamo wa Kabange umepingana na ule wa kocha wa AFC ya Arusha ambaye naye alicheza Simba kwa mafanikio katika nafasi ya winga na ushambuliaji, Ulimboka Mwakingwe ambaye ameshauri kiungo huyo asiendelee kubakia klabuni.

“Fraga ni mchezaji mzuri lakini inategemea na matakwa ya mwalimu. Kwa nafasi anayocheza, kocha ameona kuna mchezaji mwingine ambaye anaweza kufanya vizuri zaidi yake lakini hata huyo asipokuwepo, bado amekuwa hapati nafasi.

Sasa suala la nafasi inategemea na mchezaji mwenyewe kwani mwalimu anachokiangalia ni nini kinaleta matokeo.

Sasa ni jukumu la mchezaji mwenyewe kujitazama bado ninapewa nafasi na mwalimu au la kisha aamue mwenyewe ili kulinda kipaji chake na kama anaona mazingira hayamfai basi anapaswa kuondoka lakini kama anaona sawa kukaa benchi anaweza pia kuamua kubakia katika timu.

Ila mtazamo wangu kwa yule kiungo raia wa Brazil kwa mazingira yaliyopo, namna ushindani wa soka la Tanzania ulivyo, pia gharama ambazo zinatumika kumhudumia kama mchezaji wa kigeni, ningekuwa kiongozi na niko katika kamati ya usajilin ningeamua kutomwongeza mkataba ikiwa mkataba wake wa awali umemalizika,” alisema Mwakingwe. basi nisingemuongezea mkataba.

Fraga amekuwa hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha Simba kwani amejikuta akisotea benchi katika idadi kubwa ya mechi huku akianza katika kikosi cha kwanza katika michezo 10 ya Ligi Kuu na kufunga mabao matatu wakati katika Kombe la Azam Sports ameanza katika michezo miwili na amepachika bao moja.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 alijiunga na Simba akitokea ATK inayoshiriki Ligi Kuu ya India na kabla ya hapo alichezea klabu za Mumbai City, Atlético Tubarão, Oeste na Gremio.

Kiungo huyo aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya vijana ya Brazili chini ya umri wa miaka 17 iliyoshiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zilizofanyika Nigeria na Brazil iliishia hatua ya makundi.

Katika kikosi hicho sambamba na mastaa kadhaa wanaotamba duniani kwa sasa ambao ni Alisson Becker (Liverpool), Phillipe Coutinho (Bayern Munich), Neymar (PSG), Casemiro, Wellington Nem (Shakhtar Donetski) na Wellington Silva (Fluminense).